Rafiki yangu mpendwa,
Kuna kitu ambacho tumekuwa tunakiona kwa watu wengi. Wanakuwa wanaanzia chini kabisa, wakiwa masikini, wanapambana sana na kuweza kujenga utajiri. Lakini baada ya kuupata utajiri, wanaishia kupoteza kila kitu na kurudi kwenye umasikini.
Hili limekuwa jambo linalowasumbua wengi, kushindwa kujua inakuwaje mtu aliyeweza kujenga utajiri anaishia kuupoteza wote. Ambacho wengi wamekuwa hawaelewi ni kwamba kujenga utajiri na kutunza utajiri ni ujuzi wa aina mbili tofauti.

Mwandishi Morgan Housel kwenye kitabu chake kinachoitwa THE PSYCHOLOGY OF MONEY anatufundisha mambo ya kuzingatia wakati wa kujenga utajiri na yale ya kuzingatia ili kuulinda ili tuweze kudumu na utajiri tunaoupata.
Kwenye kitabu hicho, Housel ametupa masomo 20 ya msingi kuhusu fedha, utajiri, tamaa na furaha. Kupitia masomo hayo tunapata nafasi ya kujifunza mambo ya kuzingatia ili kufanya maamuzi bora kifedha kwetu na kujenga utajiri na furaha.
Kwenye makala iliyopita, tulipata masomo manne kati ya hayo 20. Kwenye makala hii tunakwenda kupata masomo mengine manne na hatua za kuchukua ili tujenge na kudumu kwenye utajiri.
5. Kupata Utajiri Na Kutunza Utajiri.
Vitabu vingi vimeandikwa na mafunzo mengi yanafundishwa kuhusu kupata utajiri. Hii ni mada maarufu na inayopendwa na watu wengi. Lakini wengi wa wanaopata utajiri, huwa wanaishia kuupoteza ndani ya muda mfupi.
Pamoja na uwepo wa changamoto hiyo ya watu kupoteza utajiri, bado kumekuwa hakuna mafunzo kuhusu kutunza utajiri. Wengi huendelea kufanya yale waliokuwa wanafanya wakati wa kujenga utajiri na matokeo yake wanaupoteza.
Kujenga utajiri kunamtaka mtu achukue hatua za hatari, awe na matumaini na kujitoa kwa kila namna. Hayo ni mambo ambayo mtu anayeanzia chini anaweza kuyafanya na yakampa nafasi kubwa ya kujenga utajiri.
Kutunza utajiri kunamtaka mtu apunguze hatari, awe na wasiwasi na kuwa mnyenyekevu. Utaona haya ya kutunza utajiri ni kinyume kabisa na kujenga utajiri. Na hapo utaona kwa nini wengi wanapoteza utajiri waliojenga, kwa sababu wanaendelea kufanya yale waliyoanza nayo, ambayo yanawaweka kwenye nafasi kubwa ya kupoteza.
Hatua ya kuchukua;
Jua hali uliyopo sasa na chukua hatua sahihi. Kama unajenga utajiri, chukua hatua za hatari, kuwa na matumaini na jitume sana. Na kama umeshajenga utajiri, punguza hatari unazochukua, kuwa na wasiwasi na kuwa mnyenyekevu.
6. Ushindi Kupitia Kushindwa.
Watu wengi wamekuwa hawafanikiwi kwenye maisha kwa sababu maana yao ya kufanikiwa siyo sahihi. Watu wanapoanza kitu mara moja na kushindwa, wanaona huo ndiyo mwisho wao, kwamba hawawezi tena kufanikiwa.
Lakini hivyo sivyo ushindi unavyopatikana. Ushindi huwa unatokana na kushindwa. Kila hatua ambayo mtu anachukua na akashindwa, inakuwa imechangia kwenye ushindi wake kama ataendelea kufanya.
Kwa maana hiyo, kushindwa ni pale mtu anapoacha kufanya. Kama mtu ataendelea kufanya, hata kama matokeo anayopata siyo mazuri, inamweka kwenye nafasi ya kufanikiwa. Kwa kupitia kushindwa kwingi, ndiyo pia mtu anajiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa.
Mafanikio makubwa kwenye maisha huwa yanatokana na matokeo mazuri machache tu kati ya mengi ambayo yanakuwa siyo mazuri. Unahitaji kuwa sahihi mara chache tu ili kufanikiwa. Na ili uweze kufikia mara hizo chache sahihi, lazima upitie mara nyingi ambazo hautakuwa sahihi.
Hatua ya kuchukua;
Kamwe usiache kufanya kwa sababu umepata matokeo ambayo hukutarajia. Badala yake endelea kufanya kwa sababu unahitaji kuwa sahihi mara chache ili kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
SOMA; Mtego Wa Ukwasi Na Jinsi Ya Kuuvuka Ili Kujenga Utajiri Unaokupa Uhuru.
7. Uhuru.
Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba utajiri hauleti furaha. Wanapambana sana kupata utajiri, lakini wakishaupata wanagundua hawana furaha kama walivyodhani.
Ambacho watu wanachanganya na hivyo kujikwamisha ni utajiri na furaha havihusiani moja kwa moja. Bali furaha inatokana na uhuru. Njia pekee ya utajiri kumpa mtu furaha, ni kama unampa mtu huyo uhuru. Mtu hawezi kuwa na furaha kama hana uhuru.
Ukiangalia njia nyingi zinazowapa watu utajiri, haziwapi furaha. Labda ni mtu kwenye ajira ambaye licha ya kuwa na kipato kikubwa, analazimika kufanya kazi masaa mengi. Au mtu mwenye biashara kubwa lakini asipokuwepo basi biashara haiwezi kujiendesha yenyewe.
Unachohitaji ili uwe na furaha ni kuwa huru. Na uhuru kamili kwenye maisha ni kuweza kuamua NINI ufanye, WAKATI gani ufanye, ufanyie WAPI na ufanye na NANI. Utajiri unaojenga unapaswa kukuletea huo uhuru ili uweze kuwa na furaha.
Hatua ya kuchukua;
Kwa hatua unazochukua ili kujenga utajiri, hakikisha unaweka nafasi ya kuwa huru pale unapofikia utajiri. Wakati unaanzia chini uhuru unaweza usiwe lengo lako kubwa, lakini kwa baadaye, lazima hilo uliwezeshe. Usijikwamishe mwenyewe kwa kushindwa kupata uhuru baada ya kujenga utajiri.
8. Kitendawili Cha Mtu Ndani Ya Gari.
Huwa tunasukumwa kununua vitu vya kifahari ili tuonekane na watu wengine kwamba tuna vitu hivyo. Lakini jambo la kushangaza ni pale wengine wanapotuangalia, wanavutiwa zaidi na vitu vya kifahari tulivyonavyo na siyo sisi ambao tunavyo.
Yaani kama umenunua gari la kifahari ili watu wakuone una gari hilo, watu wanapoliona gari wanajifikiria wao wenyewe kulipata na hawakufikirii sana wewe ambaye una gari hilo.
Hii inatupa funzo kubwa sana kwamba pale tunapotumia fedha ili kuonekana na wengine, haileti matokeo hayo. Badala yake tunawafanya watu wakumbuke ndoto zao.
Wale wanaojali sana kuhusu wewe hawatajali sana una nini. Wakati wale unaotaka kuwaonyesha ulivyonavyo, hawajali sana kuhusu wewe. Elewa somo hili na utakuwa na utulivu mkubwa.
Hatua ya kuchukua;
Kamwe usifanye matumizi makubwa kwa sababu ya kutaka kuonekana na wengine. Watu hawajali sana kuhusu wewe, hata kama watavutiwa na matumizi uliyofanya. Ishi maisha yaliyo sahihi kwako na wanaojali kuhusu wewe watakuelewa.
Hapa tumepata masomo mengine manne ya utajiri na furaha kutoka kitabu THE PSYCHOLOGY OF MONEY kilichoandikwa na Morgan Housel. Masomo yapo 20, kwenye makala inayofuata tutaendelea kuyapata masomo haya. Usikose.
Hapo chini kuna mjadala mzuri ambao tumekuwa nao juu ya masomo haya kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Fungua kipindi uweze kujifunza kutoka kwa mifano na shuhuda za wengine.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.