3396; Pesa ndogo na kubwa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanachukulia pesa zote sawa na hilo kuwa kikwazo kwao kupata utajiri mkubwa wanaokuwa wanautaka.
Unapokuwa unaanzia chini kabisa, yaani ukiwa huna pesa ya kuendesha maisha, unakuwa tayari kufanya chochote halali ili kupata pesa.
Kinachokuwa muhimu kwako ni kupata pesa kwanza kabla ya mengine yote.
Sasa kwa sababu njia za kuingiza pesa ni nyingi, unapata ambayo inakuingizia pesa ya kukuwezesha kuendesha maisha yako.
Hapo ndipo wengi wanaporidhika na kujizuia kupata utajiri mkubwa.
Pale unapofanya chochote ili kupata pesa ya kuendesha maisha yako, unakuwa unapata pesa ndogo.
Pesa hiyo ndogo itakuwezesha kuendesha maisha na kukidhi mahitaji yako mengine.
Lakini kamwe haiwezi kukupa utajiri mkubwa ambao ndiyo unauhitaji kwenye maisha yako.
Watu wengi sana huwa hawajui hili, hawajui kuna tofauti ya pesa wanazopata na hawajui kuna pesa wakipata inaweza kuwa kikwazo kwao kufika mbali zaidi.
Pesa ndogo huwa ni kikwazo kwa mtu kupata pesa kubwa, kwa sababu zoezi la kupata pesa hiyo ndogo linawatinga sana na kuweza kukidhi mahitaji ya msingi kubawaridhisha haraka.
Kanuni ya kujenga utajiri mkubwa inaenda kwa hatua zifuatazo;
1. Fanya chochote kilicho halali ili kupata pesa ndogo ya kuendesha maisha yako.
2. Jenga maisha yenye uhuru kwa kuanza na pesa ndogo unayopata kwa kuwa na akiba na uwekezaji.
3. Tumia uhuru unaoupata kudanya kile ambacho ndiyo unapenda zaidi kukipata.
4. Kwa kupenda unachofanya, utaweza kukifanya kwa ukubwa na kwa muda mrefu zaidi kuliko wengine wote.
5. Kwa kufanya kitu kwa ukubwa na muda mrefu, unakuwa bora sana kwenye kukifanya na kuzalisha matokeo bora, makubwa na ya kipekee sana.
6. Ni matokeo hayo ya kipekee ndiyo yanayokuletea pesa kubwa sana na hizo ndiyo zinakujengea utajiri mkubwa kwenye maisha yako.
Rafiki, wewe umwekwama wapi kwenye kitendawili cha pesa ndogo na kubwa?
Ni hatua zipi unazokwenda kuchukua kutoka hapo ulipokwama ili uweze kupata pesa kubwa na utajiri mkubwa?
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr. Makirita Amani
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe