Rafiki yangu mpendwa,

Mpaka mteja anafika kwenye biashara na kununua kwa mara ya kwanza, kuna gharama nyingi sana zinazokuwa zimetumika.

Tukijaribu kuziainisha gharama hizo, unaweza kupata picha ambayo siyo rahisi kuiona.

1. Eneo ambapo biashara ipo linachangia kwenye gharama ya kumpata mteja. Eneo ambalo lina mzunguko wa watu wengi, kodi yake huwa ni kubwa kuliko eneo lenye mzunguko mdogo. Hivyo kodi kubwa unayolipa kwenye eneo lenye mzunguko wa watu wengi inahusisha gharama ya kumpata mteja kwa urahisi.

2. Matangazo unayolipia ili wateja wajue kuhusu biashara yako yanakuwa na gharama. Hizo pia zinaingia kwenye gharama ya kumpata mteja.

3. Unapotoa ofa, punguzo au zawadi kwenye manunuzi ya kwanza ya mteja ni faida unaipunguza au kuiondoa kabisa. Hiyo ni gharama ya kumpate mteja kwa mara ya kwanza.

4. Kuwalipa kamisheni au kuwapa zawadi wale wanaokuletea wateja ni gharama nyingine unayoingia kupata wateja.

Ukiangalia hiyo orodha, unaweza kuona jinsi ambavyo kila biashara inaingia gharama kwenye kuwapata wateja wake. Kwa gharama hizo, manunuzi ya kwanza ya wateja huwa hayana faida kabisa. Wakati mwingine manunuzi hayo ya kwanza huwa yanakuwa ni ya hasara kabisa.

Kwa sababu hiyo, mteja akinunua mara moja kwenye biashara na asirudi tena, inakuwa ni hasara kubwa sana kwenye biashara. Kama ambavyo tumeshaona, mauzo ya kwanza yanakuwa yamekidhi tu gharama za kumpata mteja.

Faida kwa mteja huwa inapatikana kwenye manunuzi ya kujirudia rudia anayoyafanya. Hivyo wajibu wako kama mfanyabiashara au muuzaji ni kuhakikisha unapowauzia wateja, wanarudi tena kununua.

Hakikisha kile mtaje anayenunua kwenye biashara yako mara moja, anarudi tena kununua na tena na tena. Na zaidi, hakikisha mteja anayerudi kununua mara kwa mara anawaleta wateja wengine nao waje kununua.

Kuwabakisha wateja kwenye biashara kwa muda mrefu ni moja ya njia bora ya kukuza mauzo kwenye biashara yoyote ile. Hiyo ni kwa sababu wateja ambao wameshanunua ni rahisi kuwauzia kuliko wateja ambao ni wapya kabisa.

Wafanyabiashara na wauzaji wengi wamekuwa hawawezi juhudi kubwa kwenye kuhakikisha wanawauzia wateja kwa muda mrefu ili kunufaika nao. Kutokufanya hivyo kumekuwa kunapelekea biashara zao kuwa kama mnada, ambapo watu wananunua mara moja tu. Hilo limekuwa linapelekea biashara kuwa kama inaanza upya kila wakati.

Kwa biashara ambayo imeshauzia wateja, haipaswi kuwa vigumu kwake kufanya mauzo kwa msimamo. Inachohitaji ni kuwashawishi wateja ambao walishanunua warudi tena kununua na walete wateja wengine.

Changamoto kubwa ni wafanyabiashara na wauzaji wengi wamekuwa hawajui mambo ya kufanya ili kuwabakisha wateja kwenye biashara. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekushirikisha hatua za kuchukua ili uweze kuwabakisha wateja kwenye biashara yako kwa muda mrefu. Karibu ufungue kipindi, ujifunze na kuchukua hatua ili kuuza kwa faida kwa wateja wa biashara yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.