Rafiki yangu mpendwa,

Kuna watu ambao huwa wanaanzia chini kabisa kifedha, wakiwa kwenye umasikini mkubwa.

Wanapambana sana kutoka kwenye umasikini huo na kufanikiwa kuenga utajiri.

Lakini inatokea changamoto ambayo iko nje ya uwezo wao na kuwapelekea kupoteza utajiri wao.

Inaweza kuwa ni kuyumba kwa uchumi kunapoteza uwekezaji wao au hasara kuua biashara zao.

Mambo tusiyotegemea huwa yanatokea, lakini pia huwa tunafanya makosa mbalimbali kwenye maisha yetu.

Swali ni kwa nini baadhi ya watu wanaopitia mambo hayo wanabaki imara wakati wengine wanapotea kabisa?

Na jibu lipo kwenye nafasi ya kukosea ambayo watu wanakuwa wamejiwekea kwenye mipango yao.

Mwandishi Morgan Housel kwenye kitabu chake kinachoitwa THE PSYCHOLOGY OF MONEY anatufundisha jinsi ya kuongeza nafasi ya kukosea ili tuweze kudumu kwenye utajiri tunaoujenga.

Kwenye kitabu hicho, Housel ametupa masomo 20 ya msingi kuhusu fedha, utajiri, tamaa na furaha. Kupitia masomo hayo tunapata nafasi ya kujifunza mambo ya kuzingatia ili kufanya maamuzi bora kifedha kwetu na kujenga utajiri na furaha.

Kwenye makala ziliyopita, tumepata masomo 12 kati ya hayo 20. Kwenye makala hii tunakwenda kupata masomo mengine manne na hatua za kuchukua ili tujenge na kudumu kwenye utajiri.

13. Uwanja Wa Kukosea.

Huwa tunaweka mipango, lakini mambo huwa hayaendi kama tulivyopanga.

Hivyo sehemu muhimu ya kila mpango ni kuwa na mpango wa mpango kutokwenda kama ulivyopanga.

Unapaswa kujipa uwanja mpana wa kukosea ili chochote kinachotokea kisikuondoe kabisa kwenye mchezo. Kwa sababu ushindi wa mchezo ni kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Kwenye biashara na uwekezaji unapaswa kuwa na akiba ya kutosha ili hata ukipata hasara uweze kuendelea na siyo kutoka kabisa kwenye mchezo.

Kwenye fedha binafsi, uwanja mpana wa kukosea ni kuwa na vyanzo vingi vya kipato na akiba kubwa ya kukuwezesha kuendesha maisha yako hata kama hutakuwa na kipato kabisa.

Hatua ya kuchukua;

Kwa mipango unayoweka, jua kuna nafasi ya mambo kwenda tofauti na unavyopanga, hivyo hakikisha kwa matokeo yoyote utakayoyapata bado utabaki kwenye mchezo. Kuwa na akiba na uwekezaji wa kutosha ili changamoto yoyote ya kipato isikuondoe kwenye mchezo.

14. Utabadilika.

Sisi wenyewe huwa siyo watabiri wazuri juu ya maisha yetu. Maamuzi mengi ambayo huwa tunayafanya tukidhani ndiyo mwisho, huwa tunaishia kuyabadili. Hiyo ni kwa sababu malengo na matamanio yetu huwa yanabadilika kadiri tunavyokwenda.

Huwa hatupendi mabadiliko ya kila mara kwa sababu inaonyesha tunakosa msimamo. Lakini zipo nyakati ambazo mabadiliko ni ya lazima, kutokana na hali ambazo unakuwa unapitia.

Unapofanya maamuzi yoyote, usijiweke kwenye nafasi ambayo mabadiliko yatakuwa magumu kwako huko mbele. Badala yake acha nafasi ambapo mabadiliko yakihitajika utaweza kuyafanya.

Hatua ya kuchukua;

Kwa kila maamuzi unayofanya, weka nafasi ya kubadilika na pale mabadiliko yanapohitajika, yafanye bila ya kujali mapenzi yako ya awali. Fanya maamuzi yako kwa kuepuka majuto ambayo utakuwa nayo baadaye kama hutafanya kwa usahihi.

15. Hakuna Cha Bure.

Kila kitu kwenye maisha huwa kina gharama. Na kadiri kitu kinavyokuwa cha thamani, ndivyo gharama yake inavyokuwa kubwa.

Kwa bahati mbaya sana, gharama za vitu vingi huwa hazipo wazi na unadaiwa baada ya muda wa kulipa kupita. Changamoto nyingi ambazo watu wanakutana nazo kwenye maisha ni kwa sababu ya kutokulipa gharama ambazo walipaswa kulipa.

Kwenye kujenga utajiri, gharama kubwa ambayo mtu unapaswa kulipa siyo fedha pekee, bali ni hofu, wasiwasi, kukosa uhakika na majuto.

Kujaribu kujenga utajiri bila ya kulipa gharama, kunapelekea mtu uje kulipa gharama kubwa zaidi

Hatua ya kuchukua;

Kwa kila unachotaka kwenye maisha yako, jua gharama unayopaswa kuilipa ili kukipata na kisha lipa gharama hiyo. Usihangaike na njia za mkato za kupata kitu bila kulipa gharama, utaishia kulipa gharama kubwa zaidi.

16. Mimi Na Wewe.

Uchumi huwa unapitia hali ya kukua na kuanguka. Sababu kubwa ni hali ya watu kuigana, ambapo kunatokana na tamaa.

Anguko la uchumi huwa linatokea pale wawekezaji wa muda mrefu wanapowaiga wawekezaji wa muda mfupi kutokana na faida kubwa wanayokuwa wanaipata.

Ni vigumu sana watu kutulia pale wanapoona wengine wanapata faida kubwa. Ni pale kila mtu anapokimbilia faida kubwa ndiyo anguko la uchumi hutokea na wote kupoteza.

Unachopaswa kujua ni kwamba kwenye maisha kila mtu anacheza mchezo wake, ambao ni tofauti kabisa na michezo wanayocheza wengine. Kuiga wengine kwenye michezo yao ni kujipoteza mwenyewe.

Hatua ya kuchukua;

Jua mchezo unaocheza wewe na hakikisha hatua unazochukua ni za mchezo huo badala ya kuiga mchezo wa wengine. Usiige yale wanayofanya wengine kwa sababu yana manufaa kwao, yanaweza yasiwe na manufaa kwako kwa sababu mnatofautiana sana.

Hapa tumepata masomo mengine manne ya utajiri na furaha kutoka kitabu THE PSYCHOLOGY OF MONEY kilichoandikwa na Morgan Housel. Masomo yapo 20, kwenye makala inayofuata tutaendelea kuyapata masomo haya. Usikose.

Hapo chini kuna mjadala mzuri ambao tumekuwa nao juu ya masomo haya kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Fungua kipindi uweze kujifunza kutoka kwa mifano na shuhuda za wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.