Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye haya maisha huwezi kufanikiwa bila ya kubebwa. Mafanikio ni magumu na yenye changamoto nyingi, hivyo lazima kuwe na kitu kinachokubeba ili ufanikiwe.

Ugumu wa mafanikio huwa unaanzia ndani ya mtu na nje ya mtu. Ndani ya mtu ni hali ya kukata tamaa ambayo mtu anakutana nayo kwenye safari yake ya mafanikio. Na nje ya mtu ni hali ya ushindani na kukwamishwa na watu wengine.

Ili kuvuka ugumu huo wa ndani na wa nje, ni lazima uwe zaidi ya vile ulivyo kabla hujafanikiwa, lazima uwe na kitu cha kukubeba.

Watu wengi wanajua umuhimu wa kubebwa ili kufanikiwa, lakini wamekuwa wanafanya makosa makubwa kwenye kubebwa. Wanatafuta kubebwa na watu wengine, kitu ambacho huwa hakiishii vizuri. Kwani wale wanaokubeba, ndiyo hao hao huwa wanakuangusha.

Ukibebwa na watu, unakuwa kwenye hatari kubwa ya kuanguka, kwa sababu watu huwa wanabadilika sana kulingana na mafanikio yako. Ukiwa chini kabisa, watu wengi watakuwa tayari kukubeba upige hatua. Lakini unapoanza kupanda juu, hata wale waliokubeba wataanza kuonekana kuwa kikwazo kwako.

Ni asili ya binadamu kupata wivu pale mwingine anapofanya vizuri kuliko yeye. Wakati mwingine wivu unakuwa mzuri ambao unawasukuma watu kufanya kwa ukubwa zaidi. Lakini kuna wakati wivu unakuwa mbaya na watu kusukumwa kuwakwamisha wengine.

Unapobebwa na watu wengine, unajiweka kwenye hatari ya kukwamishwa pale unapokuwa umefanikiwa.

Kuna ambao huwa wanabebwa na bahati, mkumbo au mambo ya msimu. Hapa watu wanakuwa wanayatumia vizuri matukio mbalimbali wanayokutana nayo kwenye maisha. Matukio ya aina hiyo huwa yanatokea, lakini nayo huwa siyo ya kudumu. Hivyo wale wanaobebwa na matukio hayo, hawachukui muda wanashuka chini.

Kuna sifa moja pekee ambayo ukiweza kujijengea inakubeba kila mahali na kamwe haiwezi kukuangusha. Hii ni sifa ambayo unaijenga ndani yako hivyo hakuna yeyote anayeweza kukunyang’anya sifa hiyo.

Kwa kubebwa na sifa hiyo, huhitaji kujipendekeza kwa watu ili wakubebe, badala yake watu watakuwa wanakuja kwako wakitaka uwasaidie kwa kile ulichonacho.

Uzuri ni kwamba sifa hiyo iko ndani ya uwezo wako kujijengea, kwa hapo ulipo sasa na ukaweza kunufaika nayo. Haijalishi upo kwenye hali gani kwa sasa, ukiweka muda na juhudi kwenye kujenga sifa hii, itakubeba sana na kukupa chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeielezea kwa kina sifa hiyo na jinsi unavyoweza kujijengea ili kunufaika nayo sana. Fungua kipindi ujifunze na kwenda kuweka kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.