Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Ndani ya programu hii tunajifunza na kufanya kwa vitendo uwekezaji kwa msimamo bila kuacha. Lengo ni kuweka kujenga utajiri na uhuru wa kifedha ili kuweza kuishi maisha kwa namna tunavyotaka wewe.

Kwenye programu yetu, lengo letu la chini kabisa ni kuwekeza kwa angalau miaka 10 kwa msimamo bila kuacha wala kutoa uwekezaji huo. Hiyo ni kwa sababu ili kuyaona matunda makubwa ya uwekezaji, angalau miaka kumi inahitajika.

Swali ambalo wengi wamekuwa nalo ni je nini kinatokea baada ya hiyo miaka kumi? Pia ni wakati gani wa kuanza kula matunda ya uwekezaji tunaofanya? Kwenye somo hili tunakwenda kupata majibu ya kutuongoza kwenye safari yetu nzima.

MWISHO WA UWEKEZAJI.

Tukianza na swali la mwisho wa uwekezaji ni lini, jibu ni HAKUNA MWISHO. Kwa jinsi ambavyo tumejifunza uwekezaji unavyofanya kazi, hatuhitaji kuwa na mwisho wa kuwekeza. Zoezi la uwekezaji litaendelea kuwa endelevu kwa kipindi chote cha maisha yetu.

Kitakachobadilika ni kiwango na aina ya uwekezaji. Kama ambavyo tumejifunza kwenye aina mbalimbali za uwekezaji na mifuko, kadiri umri unavyokwenda ndivyo mtu anapaswa kuwekeza sehemu ambazo usalama wake ni mkubwa hata kama marejesho ni madogo.

Hivyo kwenye mifuko ya uwekezaji ya pamoja, kadiri umri unavyokwenda, uwekezaji unapaswa kuwa zaidi kwenye mifuko ambayo inawekeza zaidi kwenye hatifungani kuliko hisa. Hiyo ni kwa sababu hatifungani zina usalama mkubwa kuliko hisa, japo faida yake ni ndogo.

Kwenye programu ya NGUVU YA BUKU, miaka 10 ya kwanza ni ya kufanya uwekezaji bila ya kutoa kabisa. Kisha baada ya hapo uwekezaji utaendelea na kutoa kutategemea hali ya kifedha ya mtu na mipango aliyonayo. Ila uwekezaji hautakuwa umefika tamati, utaendelea bila kukoma.

Utafanya uwekezaji kwa kipindi chote cha maisha yako bila kuacha. Hata pale utakapokuwa unaishi kwa kutegemea uwekezaji huo, bado sehemu ya matunda ya huo uwekezaji utapaswa kurudisha kuwekeza.

SOMA; Dhana Ya Riba Mkusanyiko Na Nguvu Yake Kwenye Uwekezaji.

KITAKACHOTOKEA UKIFA.

Kama tunawekeza kwa kipindi chote cha maisha yetu bila kuacha, nini kitatokea kwenye uwekezaji wetu pale tutakapokufa? Hilo ni swali ambalo kila mtu anakuwa nalo.

Jibu lake ni kile ambacho unaamua sasa ukiwa hai. Tunapofanya uwekezaji siyo tu kwa ajili yetu binafsi. Kwanza tunafanya ili tuweze kuwa na uhuru wa kipato, hasa umri unapokwenda na nguvu za kufanya kazi kupungua, tuweze kuwa na kipato cha kuyaendesha maisha yetu kwa namna tunavyotaka.

Lakini lazima tupange wakati bado tupo hai uwekezaji wetu utumikeje pale tunapofariki dunia. Tunapaswa kuandika wosia wa jinsi uwekezaji tuliofanya utakavyopaswa kutumika. Unaweza kuamua uwekezaji wako urithiwe na watu wa karibu yako. Pia unaweza kuamua kutoa msaada kwa taasisi mbalimbali kulingana na yale unayojali zaidi.

Hayo yote yapange yafanyike baada ya kifo chako, ili wakati upo hai uwekezaji wako ukupe uhuru wa kuyaishi maisha yako bila ya kuwa tegemezi kwa mtu yeyote.

KULA MATUNDA YA UWEKEZAJI.

Tumeshajifunza jinsi riba mkusanyiko inavyofanya kazi na kuzalisha matunda makubwa kama itafanyika kwa muda mrefu na bila kuingiliwa. Hivyo swali linakuwa ni lini tunaanza kula matunda ya uwekezaji ambao tunaufanya, yaani kutumia uwekezaji huo?

Jibu ni kuna njia mbili za kufanya maamuzi ya kuanza kula matunda ya uwekezaji wako.

Njia ya kwanza ni pale unapokuwa umefikia lengo lako la kustaafu. Lengo la kustaafu ni kiasi cha uwekezaji unachokuwa unapaswa kufikia ili marajesho unayopata kwenye uwekezaji yakuwezeshe kuendesha maisha yako bila kulazimika kufanya kazi moja kwa moja.

Kuna kanuni nyingi za kukokotoa lengo la uwekezaji, lakini ambayo ni rahisi ni kuanza na matumizi yako ya msingi, kisha kuwa na uwekezaji ambao marejesho yake ya chini yanatosha kukidhi mahitaji hayo.

Kwa mfano kama unakadiria matumizi yako kwa mwezi yatakuwa wastani wa Tsh milioni 5, kwa mwaka itakuwa Tsh milioni 60. Kama uwekezaji unaofanya unakupa rejesho la asilimia 10 kwa mwaka, inabidi uwe na uwekezaji ambao ni mara 10 ya matumizi yako. Hivyo kwa hesabu hizo, uwekezaji wako unapaswa kuwa siyo chini ya Tsh milioni 600.

Hii hesabu imerahisishwa, kuna mengine ya kuzingatia hapo kama mfumuko wa bei ambao unapelekea gharama za maisha kupanda na mabadiliko ya uchumi yanayoweza kuathiri rejesho la uwekezaji.

Kwa mifuko ya UTT AMIS ambayo ndiyo msingi wetu mkuu wa uwekezaji, mfuko wa Hatifungani ndiyo mzuri kwenye lengo la kustaafu. Mfuko huo una utaratibu wa kupokea gawio la uwekezaji kila mwezi huku uwekezaji ukiendelea kukua thamani kadiri muda unavyokwenda.

Hivyo kwa lengo la uwekezaji, ni kuhakikisha unafikisha kiasi ambacho gawio la kila mwezi linatosha kuyaendesha maisha yako bila ya kugusa msingi wako mkuu wa uwekezaji. Kwa njia hiyo maisha yataweza kwenda vizuri huku uwekezaji wako ukiendelea kukua thamani.

Njia ya pili ya kufanya maamuzi ya kutumia uwekezaji ni pale unapokuwa na mahitaji makubwa ya kufanya hivyo. Hili ni baada ya kipindi cha miaka 10 ya awali ambayo tunawekeza bila kutoa. Baada ya hapo, kulingana na mahitaji unayokuwa nayo, unaweza kutoa kwenye sehemu ya uwekezaji wako. Muhimu ni ukitoa uweze kurudisha kiasi hicho ulichotoa au kuendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa.

Ni muhimu kufanya hivyo pale ambapo unakuwa bado hujafikia kustaafu, yaani pale unapokuwa unaendelea na shughuli zinazokuingizia kipato cha moja kwa moja.

SOMA; Wekeza Na Sahau, Kanuni Bora Ya Uwekezaji Kwenye Kujenga Utajiri.

KUWA NA AKIBA ILI KUTOKUINGILIA UWEKEZAJI.

Kuepuka kulazimika kutumia uwekezaji wako mara kwa mara, hasa pale unapokabiliwa na changamoto mbalimbali, hakikisha unakuwa na akiba ambayo ni tofauti na uwekezaji.

Kama ambavyo tayari tunajua, nguvu ya riba mkusanyiko ipo kwenye muda na kutokuingiliwa. Kama tutakuwa tunaingilia uwekezaji kwa sababu tunalazimika kufanya hivyo, hatutanufaika nayo.

Hivyo pamoja na kufanya uwekezaji, tunapaswa kuwa na mfuko wa akiba ya dharura ili pale mambo tusiyotegemea yanapotokea tusilazimike kuingilia uwekezaji wetu.

Wengi huwa tunaweka mipango yetu kama vile mambo yataenda tunavyopanga sisi. Tunajisahau kuwa na fungu la dharura. Na mara zote dharura huwa zinatokea. Pale dharura zinapotokea na hatuna maandalizi yoyote, macho yetu yanaenda kwenye uwekezaji ambao tumefanya.

Tunaweza kujihalalishia kwamba hayo ndiyo matumizi ya uwekezaji wetu, lakini ukweli ni kukosa maandalizi sahihi. Uwekezaji wako siyo mfuko wako a dharura, bali ni njia ya fedha kukufanyia wewe kazi na kukuzalishia faida. Ukigeuza uwekezaji wako kuwa mfuko wa dharura, hautachukua muda, utaumaliza, maana dharura huwa haziishi.

TUSISAHAU LENGO KUU NI UHURU.

Tuwe na mtazamo sahihi kuhusu uwekezaji, kwamba hatuufanyi sasa ili tuje kuanza kuutumia kama kufidia tunayojinyima sasa. Bali tunaufanya uwekezaji kuhakikisha kwa kipindi chote ambacho tupo hai, tunakuwa huru. Na uhuru ndiyo kitu tunachopaswa kukilinda kwa kipindi chote cha uhai wetu.

Uhuru wa kitu unakuwa nao pale unapokuwa nacho, ukishakipoteza huna tena uhuru wa kukitumia. Kwa sababu hatujui kwa hakika ni siku gani tutaondoka hapa duniani, mpango mzuri ni kuhakikisha kwa kipindi chote cha uhai wetu tunakuwa na huo uhuru.

Kitu muhimu zaidi kukumbuka ni zama hizi watu wanaishi miaka mingi kuliko vipindi vingine. Idadi ya watu wanaishi miaka zaidi ya 80 ni kubwa na wanaofikisha miaka 100 pia ni kubwa. Hivyo unapokuwa unaweka mipango yako ya fedha, chukulia utaishi kwa angalau miaka 100. Hivyo jiulize utawezaje kuwa huru kwa miaka inayokuwa imebaki tangu kustaafu kwako kufanya shughuli za moja kwa moja mpaka kifo chako?

Kama utastaafu shughuli zako ukiwa na miaka 60, maana yake una miaka 40 mbele yako. Unapaswa kuhakikisha uwekezaji unaokuwa nao na marejesho unayopata vinaweza kukupeleka kwa miaka inayokuwa mbele yako, hata kama hutafanya shughuli ya kuingiza kipato moja kwa moja.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Kwa nini tunapaswa kufanya uwekezaji kwa uendelevu bila kuacha kwa miaka yetu yote?

2. Ni nyakati gani za kufanya maamuzi ya kutumia uwekezaji uliofanya?

3. Kokotoa kiasi cha uwekezaji unachopaswa kuwa nacho ili marejesho yake yaweze kukidhi matumizi yako bila ya kuingilia msingi uliowekezwa.

4. Karibu kwa maswali uliyonayo kuhusu somo hili au programu nzima ya NGUVU YA BUKU.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.