Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi.

Lengo la CHUO CHA MAUZO ni kukufanya wewe kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Lakini kabla hujawa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Unakuwa mtu bora pale unapojifunza na kuchukua hatua kwenye eneo la maendeleo binafsi.

Na moja ya mambo unayopaswa kuwa vizuri kwenye maendeleo binafsi ni KUTUMIA VIKWAZO unavyokutana navyo kwenye safari yako ya maisha kufanikiwa zaidi.

Kwa walio wengi, wanapokutana na vikwazo unakuwa ndiyo mwisho wa safari. Lakini kwa wale wanaopata mafanikio makubwa, siyo kwamba hawakutani na vikwazo, bali wanavuka vikwazo hivyo.

Karibu kwenye somo hili, ujifunze jinsi ya kuvuka kila aina ya vikwazo unavyokutana navyo na kuwa muuzaji bora ambaye anafanya mauzo makubwa.

NI BAHATI KUWA KWENYE MAUZO.

Moja ya falsafa za CHUO CHA MAUZO ni mauzo ndiyo suluhisho la kila kitu kwenye maisha. Hakuna changamoto yoyote unayoweza kuwa nayo kwenye maisha yako na isiweze kutatuliwa na mauzo.

Una changamoto ya kipato kidogo na kisichotosheleza? Fanya mauzo zaidi, utaweza kutengeneza kipato zaidi.

Kuna kitu unataka watu wengine wakubaliane na wewe ila wanakuwa wagumu? Kuwa na ushawishi zaidi kupitia mbinu za mauzo na utaweza kukubalika.

Unakosa furaha kwenye maisha yako kwa sababu unaona kama yanakosa maana? Angalia watu wenye uhitaji wa kile unachouza, washawishi wanunue na wasaidie kuyabadili maisha yao. Wanapofurahia kile walichonunua kwako na kuonyesha kimewasaidia, utajisikia vizuri, kwamba maisha yako yana maana.

Ni bahati kubwa sana kwako wewe kuwa kwenye mauzo, kwa sababu unakuwa na uwanja mpana wa kuyaboresha maisha yako katika kila nyanja. Ni wewe tu uchague kuwa muuzaji bora na kwa kila unalokutana nalo kuliangalia kwa upande wa uuze nini zaidi ili kuweza kulitatua.

VIKWAZO BINAFSI.

Kuna vikwazo vingi binafsi unavyokuwa unapitia kwenye maisha yako, ambavyo kwa kutumia mbinu za mauzo unaweza kuvitatua na ukawa na maisha bora.

1. Maana ya maisha.

Watu wengi wamekuwa wanasumbuka na maana ya maisha, wasijue wako hapa duniani kufanya nini. Kwa kutumia misingi ya mauzo, chagua kufanya kitu ambacho kinaongeza thamani kwenye maisha ya wengine na utayaona maisha yako kuwa na maana. Wauzie watu kitu chenye manufaa kwao na maisha yako yatakuwa bora.

2. Mahusiano yako na wengine.

Sisi binadamu ni viumbe wa mahusiano, ubora wa maisha yetu unategemea sana ubora wa mahusiano yetu. Mbinu za mauzo ni muhimu kwenye kujenga mahusiano yetu na wengine, kuanzia mahusiano binafsi mpaka ya kibiashara.

Kwa kuweka mbele maslahi ya wengine, kutabasamu, kusikiliza, kuwa waaminifu na kuwapa watu thamani kubwa, mahusiano yetu yanakuwa bora na imara. Hilo linapelekea maisha yetu kwa ujumla kuwa bora.

3. Kipato kisicho na ukomo.

Mauzo ndiyo kazi pekee ambayo haina ukomo wa kipato. Kazi nyingi huwa zina ukomo wa kipato ambacho mtu anaweza kuingiza au kulipwa. Lakini kwenye mauzo, ukishakuwa bora, unakuwa huna ukomo wa kipato. Kwa sababu kadiri unavyoweza kuuza zaidi, ndivyo unavyoingiza kipato kikubwa zaidi.

Kama unamiliki biashara yako mwenyewe, kwa kuuza zaidi unaongeza zaidi mapato na faida kwenye biashara hiyo.

Na kama umeajiriwa kama muuzaji kwenye biashara, kwa kuuza zaidi unapata nafasi ya kulipwa kamisheni kubwa zaidi. Ukiwa muuzaji bora, utataka kulipwa kwa kamisheni ili unapokazana na kuuza zaidi, kipato chako kiweze kuwa kikubwa pia.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuvuka Vikwazo Na Changamoto Kwenye Safari Yako Ya Mafanikio.

VIKWAZO KWENYE MAUZO.

Kwenye mauzo, huwa kuna vikwazo mbalimbali ambavyo vinawakwamisha wengi na kukata tamaa. Wengi wanapoingia kwenye mauzo, huwa wanadhani ni kitu rahisi. Lakini wanapokutana na vikwazo, wanaona ni ngumu na kuacha.

Kufanikiwa kwenye mauzo ni lazima uweze kuvuka vikwazo vya mauzo ambavyo utakutana navyo. Baadhi ya vikwazo hivyo ni kama ifuatavyo;

1. Kukataliwa.

Kukataliwa ni sehemu ya mauzo. Unapowafikia wateja kwa mara ya kwanza, unakuwa mgeni kwao na hivyo wanakukataa. Wapo watakaokukataa wazi wazi na wapo ambao watakupuuza.

Kama utakubali kukataliwa kukukwamishe, hutaweza kufanikiwa kwenye mauzo. Wajibu wako ni kuendelea kuwafuatilia wateja bila ya kuchoka. Ukijua kwamba kila unapoendelea kuwafuatilia unazidi kuzoeleka na ile hali ya ugeni kuondoka. Mwisho unakubalika na kuweza kuwashawishi wanunue.

Unapokataliwa na wateja, endelea kuwafuatilia bila kuchoka, utakubalika na kuweza kuuza.

2. Mapingamizi ya wateja.

Hata kama wateja watakukubali, bado kukamilisha mauzo haitakuwa hatua rahisi. Kila unapowashawishi wateja kununua, watakupa mapingamizi mbalimbali. Wapo watakaokupa mapingamizi ya bei, kwamba bei yako ni kubwa. Wengine mapingamizi ya ubora, bajeti, kutokuwa na mahitaji au kukuambia tayari wananunua mahali pengine.

Unapokutana na mapingamizi ya wateja wakati unawashawishi kununua usikubaliane nayo na kuona huwezi kuuza. Badala yake yatumie mapingamizi hayo kukamilisha mauzo kwa wateja hao. Waonyeshe kwamba hayo mapingamizi waliyonayo ndiyo sababu ya wao kununua. Kama wanasema bei ni kubwa, waonyeshe jinsi wanavyokwenda kupata thamani kubwa zaidi kwa kulipa bei hiyo.

Ukiyatumia mapingamizi ya wateja kama sababu ya wao kununua, utaweza kufanya mauzo makubwa zaidi.

3. Ushindani sokoni.

Kwenye soko huwa kuna ushindani mkali. Kwa chochote unachouza, kuna wengine ambao pia wanauza. Wakati mwingine ushindani unakuwa mkali na wenye fujo, hasa pale unapohusisha kupunguza bei. Wauzaji wengi wanapoona ushindani ni mkali, wanaona hawawezi kuuza kwa ukubwa na hivyo kukata tamaa.

Wewe usiwe hivyo, badala yake tumia ushindani kama sababu ya kuuza zaidi. Pale ushindani unapokuwa mkali, furahia kwa sababu ni kitu ambacho tayari kina soko. Kama watu wengi wanafanya biashara ya aina fulani, maana yake soko lipo na inalipa. Hapo sasa ndipo wewe unapopaswa kuhakikisha unakuwa bora kuliko hao wengine wote. Wajibu wako ni kuhakikisha unawapa wateja kitu ambacho hawawezi kukipata kwa wauzaji wengine. Ukiweza kufanikisha hilo, utaweza kuwa mbele ya ushindani na kufanya mauzo makubwa.

Usihofie ushindani mkali, bali utumie kama kiashiria cha biashara kuwa nzuri na kukazana kuwa bora ili kuwa mbele ya ushindani.

Kwa kuvuka vikwazo hivi vya mauzo, utaweza kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

GEUZA VIKWAZO KUWA NJIA.

Muuzaji bora kuwahi kutokea, somo kuu la kuondoka nalo hapa na linalopaswa kuwa msingi mkuu wa maisha yako ni hili; HEUZA VIKWAZO KUWA NJIA.

Pale unapokuwa kwenye safari yoyote ile na kwenye njia yako ukakutana na vikwazo, usiache safari hiyo, badala yake geuza vikwazo hivyo kuwa njia.

Yaani badala ya kusema siwezi kuendelea kwa sababu ya hiki nilichokutana nacho, sema; ‘NITATUMIA HIKI KUPATA NINACHOTAKA’.

Ukiweza kuishi kwa msimamo huo, hakuna chochote kinachoweza kukuzuia kupata mafanikio unayoyataka. Kwa sababu vikwazo vingi unavyokutana navyo, nyuma yake kuna fursa kubwa zaidi.

Kwa sababu vikwazo vinawazuia wengi ambao hawajajitoa sana, wewe ukijitoa hasa na ukavuka kila aina ya kikwazo, utakuwa mbele sana ya wengine na kupata matokeo makubwa ambayo wengine hawayapati.

Geuza kila kikwazo kuwa fursa ya wewe kupata kile unachotaka na hakuna kitakachokuzuia kufanikiwa kwenye jambo lolote unalotaka.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.