Rafiki yangu mpendwa,

Najua unajua kuhusu ugonjwa wa UKIMWI, ugonjwa ambao ni hatari na hauna dawa ya kutibu. Mtu akishapata ugonjwa huo, anakuwa kwenye hatari ya kufa kwa magonjwa mengine nyemelezi.

Kwenye biashara pia kuna UKIMWI wake, lakini huo unaitwa UKIBI ambapo ni kifupisho cha UPUNGUFU WA KINGA KWENYE BIASHARA. Biashara yenye UKIBI huwa inakuwa kwenye hatari ya kufa wakati wowote.

Watu wengi ambao biashara zao zimekufa, huwa wanasingizia vitu kama ushindani, hali ya uchumi, kukosa mtaji na mengine. Lakini ukweli ni hayo ni nyemelezi tu, kinachoua biashara yoyote ile ni UKIBI. Biashara inakuwa imekosa kinga, hivyo kitu chochote cha nje kinaweza kuiua.

Kama bado huamini jiulize kwa nini uchumi unakuwa mgumu kwa wote, lakini kuna biashara zinakufa na nyingine hazifi? Kwa nini ushindani mkali unaondoa baadhi ya biashara sokoni na kuacha nyingine?

Kama hali ya nje inafanana kwa biashara zote, lakini matokeo yanatofautiana, maana yake hali ya ndani ni tofauti. Na hali ya ndani ya biashara inaathiriwa na UKIBI.

Biashara yenye UKIBI, inakosa kinga zifuatazo na hivyo kuifanya kuwa rahisi kufa;

1. MFUMO IMARA.

Mfumo wa kuendesha biashara ndiyo nguzo kuu ya mafanikio ya biashara yoyote ile. Biashara ambazo hazina mfumo huwa zinamtegemea mwanzilishi wake kutoa maelekezo ya mambo ya kufanya na jinsi yanavyopaswa kufanyika. Biashara hizo hufanya vizuri mwanzilishi akiwepo. Lakini anapopata changamoto au kutokuwepo, biashara inashindwa kuendelea.

Kuijengea biashara yako kinga ili isife, hakikisha unaweka mfumo imara wa kuiendesha. Mfumo unapaswa kuandikwa kwa lugha rahisi na inayoeleweka, ukieleza majukumu yote ya biashara na jinsi yanavyofanyika. Kila kitu kwenye biashara kinapaswa kuweza kufanyika hata kama wewe mwanzilishi haupo.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Vitabu Just Run It Na 101 Crucial Lessons They Don’t Teach You In Business School; Mfumo Bora Wa Kuendesha Biashara Na Siri 101 Za Mafanikio Kwenye Biashara.

2. TIMU BORA.

Mafanikio ya biashara yanategemea sana timu kuliko mtu mmoja mmoja. Biashara inayoendeshwa na timu bora inakuwa na nguvu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali. Uwepo wa timu unaondoa ile hali ya majukumu fulani kumtegemea mtu mmoja, ambaye asipokuwepo biashara inatikisika sana.

Kuijengea kinga biashara yako, hakikisha unajenga timu imara ya kuendesha biashara hiyo. Na hapo unapaswa kuwa tayari una mfumo, ili timu inapokuja inafanyia kazi mfumo ambao umeuweka. Ajiri watu ambao wana uwezo wa kutekeleza majukumu unayowapa kwa viwango vya juu ili biashara iweze kupiga hatua.

3. WATEJA WAAMINIFU.

Wafanyabiashara wengi huwa wanadhani lengo la biashara ni kufanya mauzo. Na hivyo huhangaika kutengeneza wateja ili kuwauzia. Kinachotokea ni wakishawauzia wateja mara moja inakuwa ndiyo imetoka, hawarudi tena. Hilo linafanya biashara kuwa kama mnada, kila wakati inatafuta wateja wapya wa kuwauzia. Kumuuzia mteja kwa mara ya kwanza huwa ni vigumu kuliko kumuuzia mteja ambaye alishanunua tena. Biashara ambazo hazijatengeneza wateja waaminifu na wanaorudi kununua huwa zinakuwa dhaifu na kuweza kufa kwa haraka.

Kuijengea kinga biashara yako, jua lengo la biashara ni kutengeneza wateja waaminifu. Hivyo kila mauzo unayofanya, lengo lake linapaswa kuwa ni kuwabakiza wateja hao kwenye biashara. Jenga mahusiano mazuri na wateja wa biashara yako kupitia ufuatiliaji endelevu ili kuwafanya warudi kununua tena na tena na hata kuwaleta wateja wengine nao wanunue.

Kwa kujenga kinga hizo kwenye biashara yako, itaweza kuvuka magumu na changamoto za kila aina na kubaki imara kwenye nyakati zote.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua zaidi kuhusu hali hiyo ya UKIBI wa biashara na jinsi ya kuhakikisha biashara yako haipotezwi na huo ugonjwa. Fungua hapo chini ujifunze ili uweze kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.