3402; Ujasiri na Mafanikio.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna njia kuu tatu za kuingiza kipato kama ifuatavyo;

Moja ni kufanya MAUZO, ambapo mtu unahusika moja kwa moja kwenye ufanyaji.

Mbili ni kujenga BIASHARA, ambapo mtu unawatumia wengine kwenye ufanyaji.

Na tatu ni kufanya UWEKEZAJI, ambapo fedha inakufanyia kazi na kukuingizia kipato.

Kuna mengi ambayo watu hufanya kwenye kuingiza kipato, lakini msingi wake unakuwa kati ya njia hizo kuu tatu.

Mafanikio kwenye jambo lolote kwenye maisha, yanataka sana mtu kuwa jasiri.

Ujasiri ni utayari wa mtu kufanya kile ambacho ni hatari na wengi wanakikwepa.
Kwa kuwa tayari kufanya hayo ambayo ni hatari, mtu anajitofautisha na wengi wanaokwepa kuyafanya.

Kufanya yale ambayo wachache sana ndiyo wanayafanya, kunakuweka kwenye nafasi kubwa ya kupata mafanikio makubwa.

Ujasiri ni kitu ambacho huwezi kufundishwa au kununua.
Bali ni kitu ambacho unakijenga kupitia hatua mbalimbali ambazo mtu unachukua.

Kwa kuwa tumeona ujasiri ni kuweza kufanya yale ambayo mtu unahofia, hata kujenga ujasiri kunatokana na mtu kufanya ambayo yanahofiwa.
Kwa sababu njia pekee ya kuishinda hofu, ni kufanya yale unayohofia kufanya.

Kwenye njia kuu tatu za kuingiza kipato, hivi ndivyo unavyojenga ujasiri unaokupa mafanikio makubwa.

Kujenga ujasiri kwenye mauzo; wauzie wasiokujua.

Kwenye mauzo, kuwauzia watu wanaokujua ni rahisi na haina hofu yoyote.
Lakini kuuzia watu wasiokujua ni ngumu na kuna hofu ya kukataliwa.
Kujenga ujasiri, wauzie watu wengi ambao hawakujui.
Kutana na wasiliana na watu ambao hawakujui kabisa na washawishi kununua.

Kwa kufanya hivyo utakataliwa na wengi, lakini pia utakubaliwa na wengi kama utaendelea bila ya kuacha.

Kuimarisha ujasiri wako ili kufanikiwa, uzia watu wengi wasiokujua. Endelea licha ya kukutana na kukataliwa.
Kuchagua watu sahihi wa kufanya nao kazi, angalia ambao wamewahi kuwauzia watu wengi wasiowajua kabisa.

Kujenga ujasiri kwenye biashara; tumia nyenzo.

Nyenzo ni kutumia rasilimali za wengine ili kuzalisha matokeo makubwa kwako mwenyewe.
Kutumia rasilimali zako mwenyewe haina ugumu sana, lakini zina ukomo.
Ili ufanye makubwa zaidi, lazima utumie rasilimali za wengine.

Kuna kukataliwa na hata kukosea kwingi wakati mtu unapotaka kutumia rasilimali za wengine.
Ni wale wenye ujasiri ndiyo huwa wanaweza kutumia rasilimali za wengine kwa manufaa.
Rasilimali hizo ni fedha, muda, ujuzi n.k.

Kujenga ujasiri wako ili kufanikiwa, hakikisha kila mara unatumia nyenzo kwenye biashara yako.
Kuwa na wafanyakazi na kuwa na mikopo ambayo biashara inalipa. Hayo yanakupa uwajibikaji mkubwa kwenye kuiendesha biashara yako vizuri maana kuna wengine wanaohusika na siyo wewe peke yako.
Ukikosea hujikwamishi wewe mwenyewe, bali unawakwamisha na wengine. Hilo linakupa nidhamu kali zaidi.

Kuchagua biashara sahihi za kushirikiana nazo, angalia ambazo zina matumizi ya nyenzo.
Epuka sana biashara ambazo wamiliki hawana nyenzo yoyote, uwajibikaji wao unakuwa mdogo.

Kujenga ujasiri kwenye uwekezaji; nenda kinyume na kundi kubwa la watu.

Kwenye uwekezaji, watu wengi huwa wanafanya maamuzi kwa kufuata mkumbo.
Kile ambacho watu wengi wanafanya, ndiyo kinaonekana salama kufanya.
Lakini ukienda hivyo, unapata hasara kubwa.

Pale bei ya uwekezaji inapokuwa inapanda, watu wanaona ndiyo uwekezaji sahihi na hivyo kununua kwa wingi. Hilo linafanya uwekezaji huo kuzidi kuongezeka bei.

Pale bei ya uwekesaji inaposhuka, watu wanaona ni uwekezaji mbaya na hivyo kuuza kwa wingi. Hilo linafanya uwekezaji huo kuzidi kushuka bei.

Matokeo yake ni watu wananunua uwekezaji kwa bei ya juu na kuuza kwa bei ya chini, kitu ambacho ni hasara.

Kujenga ujasiri kwenye uwekezaji, nenda kinyume na kundi kubwa la watu. Pale ambapo kila mtu anakimbilia kuuza na bei inashuka, wewe nunua. Utaweza kununua kwa bei ya chini sana.
Na pale ambapo kila mtu anakimbilia kununua, wewe uza. Utaweza kuuza kwa bei ya juu zaidi.
Matokeo yake ni faida.

Inahitaji ujasiri sana kununua wakati kila mtu anauza na kuuza wakati kila mtu ananunua, lakini ndipo faida ilipo.

Ujasiri mwingine kwenye uwekezaji ni kuwekeza kwa msimamo, kwa muda mrefu bila kuacha wala kutoa uwekezaji wako.
Iwe bei inapanda au kushuka, wewe unaendelea kuwekeza.
Matokeo yake kwa muda mrefu yanakuwa ni ukuaji mkubwa wa uwekezaji huo.

Kuchagua watu sahihi wa kujihusisha nao kwenye uwekezaji, angalia ambao wanawekeza kwa vitendo na kwa muda mrefu, kwa msimamo bila kuacha.
Usiangalie wanaopanga au kusema, hayo ni rahisi. Angalia wale wanaofanya kabisa na hao ndiyo watakuwa sahihi kwako.

Ukiweza kujenga ujasiri kwenye haya maeneo matatu tuliyojadili hapa, hakuna chochote kinachoweza kukuzuia kupata mafanikio makubwa.
Chukua hatua kwenye haya uliyojifunza ili uweze kufanya makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe