Rafiki yangu mpendwa,
Watu wamekuwa wanahangaika na mambo mengi sana kwenye kujenga utajiri. Wamekuwa wanakimbizana na kila aina ya fursa ambazo zinasemekana kulipa sana.
Kuna baadhi wanapata fursa ambazo zinawalipa sana, lakini bado wanashindwa kujenga utajiri wanaoutaka. Kadiri kipato chao kinavyokuwa kikubwa, ndivyo pia na matumizi yao yanakuwa makubwa.
Hiyo ni kwa sababu watu wanasahau msingi mkuu wa kujenga utajiri ambao ni UBAHILI.

Waandishi wa kitabu cha THE MILLIONEAIRE NEXT DOOR wanasema matajiri wanaelezewa na maneno matatu tu; UBAHILI, UBAHILI, UBAHILI.
Kupitia tafiti ambazo walifanya, waliona kwamba matajiri wote walikuwa wanaishi chini ya kipato chao. Yaani matumizi yao yanakuwa ni madogo kuliko kipato wanachoingiza.
Kwa matumizi kuwa madogo kuliko kipato, mtu anakuwa na fedha ya kuweka akiba na hatimaye kuwekeza, kitu kinachomjengea utajiri.
Vyombo vya habari huwa vinapenda kupamba matumizi makubwa kama ndiyo utajiri, kwa sababu vinanufaika kwa njia hiyo kuliko kupamba utajiri.
Lakini ukweli ni hakuna mtu anayeweza kujenga utajiri mkubwa bila ya kuwa bahili.
Kwa bahati mbaya sana, ubahili umepewa mtazamo ambao siyo sahihi. Umekuwa unaonekana kama ni kujitesa wakati mtu una fedha.
Lakini ukweli ni ubahili siyo mateso, bali ni kuishi maisha kwa namna sahihi. Ubahili ni kutumia chini ya kipato chako, ambalo ni jambo la msingi kabisa.
Sasa kama kutumia chini ya kipato chako haitoshelezi mahitaji ya msingi ya maisha yako, unachopaswa siyo kutumia fedha ambayo huna, bali kuongeza kipato chako.
Hivyo unaweza kuwa bahili na bado ukawa na aina ya maisha unayoyataka. Muhimu ni kuhakikisha kwa kipato chochote unachoingiza, hutumii chote, badala yake sehemu ya kipato hicho unaiweka akiba na baadaye kuiwekeza ili kujenga utajiri.
Kwenye kujenga utajiri, kuna KUSHAMBULIA na KULINDA. Kushambulia ni pale unapochukua hatua za kuongeza kipato chako. Wakati kulinda ni pale unapodhibiti matumizi yako yasizidi kipato.
Ili ujenge utajiri mkubwa, ni lazima USHAMBULIE kwa kuongeza kipato chako na ULINDE kwa kudhibiti matumizi yako, vyote kwa wakati mmoja.
SOMA; Jinsi Ya Kujenga Utajiri Mkubwa Kwa Kuishi Maisha Ya Kawaida.
MASWALI MANNE YA KUPIMA KAMA UTAJENGA UTAJIRI.
Kwenye kufanya utafiti wao, waandishi walikuwa wanauliza maswali manne ambayo majibu yake yalikuwa yanafanana kwa matajiri huku masikini wakiwa na majibu ambayo ni kinyume na hayo.
Swali la kwanza; Je nyumba yako inaishi kwa bajeti ya mwaka?
Matajiri wana bajeti ambayo wanaifuata mara zote, wakati masikini hawana bajeti kabisa. Wao wanatumia chote wanachopata na hata ziada.
Hakikisha unakuwa na bajeti unayoifuata, ambayo ni chini ya kipato chako.
Swali la pili; Unajua ni kiasi gani familia yako inatumia kwa mwaka kwenye chakula, mavazi na malazi?
Matajiri wanaweka rekodi ya matumizi yote wanayofanya na kujua ni kiasi gani kinaenda kila mahali. Kwa njia hiyo wanaweza kuyadhibiti matumizi yao. Masikini hawana rekodi ya matumizi, wao wanatumia tu bila kujua ni kiasi gani kimeenda wapi.
Wewe weka rekodi ya matumizi yote unayofanya kisha jitathmini matumizi yapi siyo ya msingi sana kwako.
Swali la tatu; Je una malengo yanayoeleweka na yaliyogawanywa kwa siku, wiki, mwezi, mwaka na maisha?
Matajiri wana malengo waliyoyaandika na kuyagawa vizuri kisha wanayafanyia kazi ili kuyafikia. Masikini wanajiendea tu, wakirukia kila linalokuja mbele yao.
Wewe kuwa na malengo uliyoyaandika na yafanyie kazi ili kujenga utajiri.
Swali la nne; Je unatumia muda wako mwingi kupangilia kesho yako kifedha?
Matajiri wanaweka muda mwingi kwenye kujifunza na kujiboresha kwenye eneo la fedha na utajiri. Hilo linawafanya wawe na uelewa sahihi na kuchukua hatua sahihi pia. Masikini wanatumia muda wao mwingi kuhofia kuhusu fedha na hivyo hakuna hatua wanazochukua.
Wewe tenga muda wa kujifunza na kupangilia utajiri wako kisha chukua hatua kujenga utajiri.
Haijalishi unaingiza kipato kikubwa kiasi gani, kama unatumia chote, huwezi kujenga utajiri. Unaanza kujenga utajiri pale unapoishi chini ya kipato chako, kwa kuweka akiba sehemu ya kipato na kuiwekeza.
Iko ndani ya uwezo wako kabisa kuanza kuishi chini ya kipato chako. Chagua kupunguza matumizi ambayo siyo ya msingi kabisa ili sehemu kubwa ya kipato chako upeleke kwenye akiba na uwekezaji.
Somo hili ni mwendelezo wa mfululizo wa masomo kutoka kitabu The Millionaire Next Door: The Surprising Secrets of America’s Wealthy kilichoandikwa na Thomas J. Stanley na William D. Danko. Masomo yote kutoka kwenye kitabu hicho yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mpana juu ya somo hili la kuwa bahili ili kuweza kujenga utajiri mkubwa. Fungua hapo chini kujifunza.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.