3403; Muda mfupi na mrefu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mlendwa,
Mafanikio makubwa yanajengwa kwa mtu kufanya kazi kubwa na kwa muda mrefu.

Kazi na muda ni lazima viwekezwe kwa kiasi cha kutosha ili kuzalisha mafanikio makubwa yanayohitajika.
Na pia hivyo ndivyo vitu ambavyo watu wengi hawapo tayari kuviweka.

Wengi hawapo tayari kuweka kazi kubwa na kwa muda mrefu.
Wanachokuwa wanataka ni matokeo makubwa na ya haraka bila ya kuweka kazi.

Hicho ni kitu ambacho kinatunufaisha zaidi sisi.
Kwa sababu kwa huo mtazamo wao wa kutaka matokeo makubwa kwa haraka bila kuweka kazi, inawatoa kwenye mchezo haraka sana.

Wanaoweza kudumu kwenye mchezo kwa muda mrefu ni wale ambao wapo tayari kuweka kazi kubwa na kwa muda mrefu, hata kama matokeo siyo kama yalivyotegemewa.

Ushindani ni mdogo sana kuliko tunavyodhani, kwa sababu wengi hawajajipanga kwa kiasi cha kutosha.

Muda mrefu unaozungumziwa hapa ni kuanzia miaka kumi na kuendelea.
Mafanikio yoyote makubwa ambayo mtu anataka kuyapata ndani ya muda ambao ni chini ya miaka kumi, anajiandaa kushindwa vibaya.
Jambo lolote kubwa linataka muda wa kutosha kujengeka.

Kuna wakati unakuwa umekamilisha kila unachopaswa kufanya, lakini bado matokeo yasipatikane kwa haraka kiasi hicho.
Kwa sababu muda wa mafanikio kujengeka unakuwa unahitajika sana.
Subira inakuwa inahitajika sana kwenye safari ya mafanikio.

Wengi wanaoshindwa siyo kwa sababu ya ugumu wa kitu au ushindani mkali.
Bali ni kwa sababu ya kukosa subira ya mafanikio kujengeka.
Wewe jenga subira ya kutosha na utaweza kukabiliaba na chochote kinachokukabili kwenye safari yako.

Weka kazi kubwa na muda wa kutosha, hakuna kitakachoweza kukuzuia kupata mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe