Safari ya maili elfu moja huwa inaanza na hatua moja. Hatua hizo moja moja zinapofanyika kwa kurudia rudia ndiyo zinaikamilisha safari inayoonekana kuwa ndefu.

Hata mtu ambaye anapanga kupanda mlima mrefu kama Kilimanjaro, haamki tu na kujikuta ameshafika kwenye kilele cha mlima. Bali anapiga hatua moja baada ya nyingine bila ya kuchoka mpaka anajikuta kwenye kilele cha mlima.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye mafanikio ya maisha yetu. Watu wengi huwa wanaangalia kile wanachotaka kupata, ambacho kinaonekana kuwa mbali na pale walipo sasa. Huwa wanafikiri kuna namna wataamka na kujikuta wameshafika kwenye kilele cha mafanikio yao.

Lakini sivyo ilivyo kwenye uhalisia, mafanikio kwenye maisha siyo kitu kinachotokea kama bahati au ajali, bali ni kitu kinachotengenezwa kwa hatua nyingi. Mafanikio kwenye maisha ni mkusanyiko wa siku nyingi ambazo mtu ameziishi kwa mafanikio.

Hiyo ina maana kwamba, mafanikio siyo siku moja ya ambali ambayo ukiifikia unakuwa umepata kila unachotaka kwenye maisha yako. Bali mafanikio ni kila siku, kila siku unavyoiishi ndiyo inayochangia kwenye mafanikio ambayo unayataka kwenye maisha yetu.

Kulijua hili ni ukombozi mkubwa sana kwenye maisha yako, kwani wengi wameshindwa kufanikiwa na hata kukosa furaha kwenye maisha yao kwa sababu wanaisubiri siku moja ya mafanikio, ambayo haipo, huku wakizipoteza siku nyingi ambazo ndizo zingechangia mafanikio wanayoyataka.

Kitu kimoja kikubwa na cha muhimu sana unachopaswa kuondoka nacho kwenye kitabu hiki, hata kama utasahau mengine yote basi kinapaswa kuwa hiki; MAFANIKIO NI KILA SIKU. Badala ya kusubiri siku moja ambayo utakuwa umeshapata kila kitu ndiyo ufurahie kwamba umeshafanikiwa, unapaswa kuiishi kila siku kwa mafanikio makubwa. Kwa sababu mkusanyiko wa siku ambazo umeishi kwa mafanikio ndiyo mafanikio ya maisha yako.

Changamoto kubwa ni namna ya kuiishi kila siku kwa mafanikio. Kwa sababu ni dhahiri kwa kila mtu kwamba siku zetu zimekuwa fupi na zenye mambo mengi ya kufanya. Kauli ya mambo ni mengi na muda ni mchache imekuwa maarufu kwa sababu za msingi kabisa. Kila siku mambo ya kufanya yanazidi kuongezeka, wakati muda wa siku umebaki ule ule ambao ni masaa 24.

Je unawezaje kuishi kwa mafanikio kwenye masaa 24 pekee uliyonayo kwenye siku yako? Hilo ndilo unalokwenda kujifunza kwenye kitabu hiki, uweze kuziishi siku zako kwa mafanikio na kuwa na maisha ya mafanikio makubwa.

Kwenye sayansi na hisabati huwa kuna kanuni mbalimbali na uzuri wa kanuni ni kwamba inapotumiwa kwa usahihi, matokeo huja yale yale bila ya kujali hali au mahali. Mfano 2 + 2 = 4, hiyo ni kanuni ya kujumlisha ambayo imekupa jibu. Ukitumia kanuni hiyo utapata jibu hilo mara zote, iwe uko Afrika, Ulaya au Amerika. Iwe ni wakati wa masika au kiangazi. Hiyo ndiyo nguvu ya kanuni, kuleta majibu yale yale pale inapotumika kwa usahihi.

Tatizo kubwa la watu ni kwamba huwa wanaziendesha siku zao kwa kubahatisha, hivyo matokeo ya siku hizo huwa hayafanani. Siku moja mtu anaweza kuwa na hamasa akafanya makubwa sana kwenye kazi au biashara yake. Siku inayofuata akawa amekata tamaa na akafanya hovyo. Mtu anayeenda kwa namna hii ni vigumu kufanikiwa, kwa sababu siku zake hazileti matokeo mazuri na ambayo ni sawa.

Hapo ndipo umuhimu wa kuwa na kanuni ya kuiendesha kila siku yako unapokuja. Kwa kuwa mafanikio kwenye maisha ni mkusanyiko wa siku zenye mafanikio, ni muhimu kila siku yako iwe ya mafanikio. Na ili kila siku yako iwe ya mafanikio, ni muhimu uwe na kanuni unayotumia kuendesha kila siku yako.

Hilo ndilo unalokwenda kujifunza kwenye kitabu hiki, siyo tu kwa nadharia, bali kwa vitendo kabisa, jinsi ya kutengeneza kanuni ya kuziendesha siku zako, ili zitoe matokeo mazuri na yanayofanana, ambayo yatakufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Wapo watu wanaosema na kuamini maisha hayana kanuni, hawa ndiyo wanahalalisha kujiendea tu kwenye kila siku yao kwa namna inavyowajia. Ni watu ambao hawawezi kutegemewa kwa jambo lolote kwa sababu hawatabiriki. Hawana muda maalumu wa kuamka wala kutekeleza majukumu yao. Watakuambia wana muda, lakini hawawezi kukamilisha chochote muhimu. Na pia watakuambia hawana muda, lakini utawaona muda wote mtandaoni wakibishana mambo yasiyo na tija.

Wewe usiwe mtu wa aina hiyo, usiwe mtu wa kuyaendesha maisha yako kwa kubahatisha, kuwa mtu unayeendesha kila siku yako kwa mpangilio maalumu, ambao unatokana na kanuni ambayo umejitengenezea wewe mwenyewe.

Kwenye sura tano za kitabu hiki, unakwenda kujifunza jinsi ya kuiishi kila siku kwa mafanikio makubwa ili maisha yako kwa ujumla yawe ya mafanikio makubwa.

Kwenye sura ya kwanza utajifunza kuhusu asubuhi ya miujiza. Asubuhi ndiyo muda muhimu zaidi kwenye siku yako, lakini ndiyo muda ambao wengi wamekuwa wanaupoteza kwa mambo yasiyokuwa na tija. Kwenye sura ya kwanza utajifunza jinsi ya kuidhibiti asubuhi yako ili kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako. Sura hiyo inakwenda kwa jina la asubuhi ya miujiza, kwani ukiweza kuitumia vizuri asubuhi yako, utaleta mapinduzi makubwa kwenye maisha yako. Soma sura hiyo ya kitabu ili ujue mambo ya kuzingatia kwenye asubuhi yako kuifanya siku yako kuwa ya mafanikio.

Sura ya pili ni ya klabu ya saa kumi na moja alfajiri. Kuna jambo moja la kushangaza kidogo, ukiangalia historia za maisha ya watu wote ambao wamefanya makubwa kwenye maisha yao, karibu wote wamekuwa ni watu wa kuamka asubuhi na mapema. Watu hao jua halijawahi kuwakuta kitandani. Huwa wanaamka asubuhi na mapema, wakati bado dunia imelala na wanapata muda tulivu wa kufanya mambo ya msingi na muhimu kabisa. Kwenye sura hii utajifunza kanuni ya 20/20/20 ya kuigawa saa moja muhimu ya asubuhi yako kwa namna ambayo utanufaika kwa siku nzima. Lakini pia kuamka asubuhi na mapema imekuwa changamoto kwa wengi. Wengi wanapanga kuamka mapema lakini muda wa kuamka unapofika wanashindwa kufanya hivyo. Licha ya kuweka alamu ya kuwaamsha mapema, wanaishia kuizima na kuendelea kulala. Sura hii itakupa mbinu za kukuwezesha kuamka asubuhi na mapema kama unavyopanga.

Sura ya tatu ni kuhusu tabia za siku ya mafanikio. Zaidi ya asilimia 60 ya mambo tunayofanya kila siku, tunayafanya kwa tabia. Yaani tunafanya bila ya kufikiria kabisa, ni mazoea ambayo yamekuwa tabia ndiyo yanatusukuma kwenye kufanya. Hiyo ina maana kwamba kama huna tabia sahihi, ni rahisi sana kupoteza siku zako na hatimaye kuyaharibu maisha yako. Hivyo kwenye sura hii unapata nafasi ya kujifunza jinsi ya kujenga tabia sahihi za kuishi kwenye siku yako ya mafanikio ili uwe na maisha ya mafanikio. Pia kama una tabia zozote mbaya zinazokuwa kikwazo kwako, utajifunza jinsi ya kuzivunja kwenye sura hii.

Sura ya nne ni ya utulivu kwenye siku yako ya mafanikio. Iko wazi kwamba zama tunazoishi ni zama zenye usumbufu wa kila aina. Na mbaya zaidi, kifaa chenye usumbufu mkuu tunatembea nacho kila mahali, maana ni simu zetu za mikononi. Bila ya kuwa na njia ya kupata utulivu kwenye siku yako, utashangaa siku inaanza na kuisha, umechoka kweli kweli lakini hakuna chochote kikubwa umekifanya. Sura hiyo inakufundisha nguvu kubwa iliyopo kwenye utulivu na jinsi ya kuupata utulivu huo na kuutumia kufanya makubwa.

Sura ya tano inajumuisha yote uliyojifunza na kupata kanuni sahihi ya siku ya mafanikio. Kanuni hiyo inagusa maeneo matatu, ambayo ni kudhibiti asubuhi yako, kushinda mchana wako na kuweka umakini kwenye jioni yako. Sura hii inaorodhesha yale unayopaswa kufanya kwenye asubuhi yako, mchana wako na jioni yako ili siku yako iwe ya mafanikio makubwa. Kwa kusoma sura hii, utaondoka ukijua mambo gani ya msingi kabisa kuzingatia ili siku yako isipotee tu kama inavyotokea kwa wengi.

Karibu sana usome kitabu hiki cha KANUNI YA SIKU YA MAFANIKIO, ili uweze kuwa na udhibiti kwenye kila siku yako na kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Kumbuka, mafanikio ni kila siku, iheshimu sana kila siku unayoipata, itumie vizuri ili upate matokeo bora na rudia hivyo kila siku ili kuweza kuwa na maisha yenye mafanikio makubwa.

Ukiweka umakini wako wote kwenye kuiishi siku yako moja kwa mafanikio makubwa, huna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu siku zijazo za maisha yako. Maana unachohitaji ni kurudia tu jinsi ulivyoiishi siku yako moja na kuweza kujenga maisha ya mafanikio.

Kupata kitabu hiki cha KANUNI YA SIKU YA MAFANIKIO, wasiliana na namba 06789 77 00 7.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekupa ufafanuzi zaidi kuhusu kitabu hiki. Fungua uweze kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.