Rafiki yangu mpendwa,

Watu ambao wanazaliwa kwenye familia masikini na kuhitajika kupambana ili kujenga utajiri, huwa wanajiona kama wameanzia kwenye bahati mbaya.

Wakiwaona wale ambao wamezaliwa kwenye familia tajiri, wanaona tayari kujenga utajiri ni rahisi kwao, maana wana mahali pazuri pa kuanzia.

Lakini uhalisia wa maisha umekuwa tofauti kabisa. Wale wanaozaliwa kwenye familia tajiri huwa wanashindwa kujenga utajiri mkubwa, licha ya kuwa na nafasi nzuri kabisa ya kufanya hivyo.

Huku wale waliozaliwa familia masikini wakiwa na msukumo wa kufanya makubwa na ambao umekuwa unawawezesha kujenga utajiri.

Wengi wamekuwa wanashindwa kuelewa hili linasababishwa na nini. Waandishi wa kitabu cha THE MILLIONAIRE NEXT DOOR, kupitia tafiti nyingi walizofanya, waliona tatizo linapoanzia.

Walichoona ni kwamba wazazi ambao walianzia chini bila ya msaada wowote wa kujenga utajiri, walipambana kufa na kupona ili kutajirika. Ni msukumo huo wa kupambana kufa na kupona ndiyo uliowawezesha kufika kwenye utajiri.

Lakini sasa, wakishapata utajiri, huwa hawataki watoto wao wapitie mateso ambayo walipitia wao. Hivyo wanakuwa wanawalinda na kuwasaidia sana, wakihakikisha hawapati shida kabisa.

Wanakuwa wanawasaidia watoto wao kwa nia njema, lakini matokeo yake yanakuwa ni kinyume na matarajio. Kwani watoto hao kwa kulindwa sana na kupata misaada, wanakuwa dhaifu na kushindwa kukabiliana na maisha ili kujenga utajiri. Kwa kuepushwa kupitia magumu, wanakosa kabisa uwezo wa kujenga utajiri mkubwa.

Matokeo yake ni watoto hao kuwa tegemezi kwa wazazi wao hata baada ya kuwa watu wazima wenye familia zao. Pale wazazi wao wanapokuwa hai, maisha yanaenda kwa sababu ya misaada wanayopata kwa wazazi. Ni pale wazazi wao wanapofariki dunia ndiyo maisha yao huwa magumu sana.

Wazazi ambao wamefanikiwa kujenga utajiri kutoa misaada na urithi kwa watoto wao huwa ina madhara ya aina mbili;

Moja ni kupunguza utajiri wa wazazi hao, kwa sababu ya matumizi kuwa makubwa.

Mbili ni kutengeneza watoto tegemezi ambao hawawezi kujenga utajiri kwenye maisha yake.

Kwa ujumla, mzazi mwenye utajiri kuwasaidia sana watoto wake anaishia kuumia yeye mwenyewe na watoto hao.

Swali ni unawezaje kuondokana na changamoto hiyo? Hapa tutaangalia pande mbili;

MTOTO ALIYEZALIWA KWENYE UTAJIRI.

Kama wewe ni mtoto ambaye umezaliwa na wazazi tajiri, kama unataka na wewe uje kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako, basi acha kuwategemea wazazi wako mapema sana.

Wategemee wazazi wako kipindi ambapo unasoma tu. Ukishahitimu masomo yako, ondoka nyumbani kwa wazazi wako na nenda kayaanze maisha yako. Nenda mbali kabisa na walipo wazazi wako na nenda kapambane kuyajenga maisha yako.

Wazazi wako hawatakubaliana na hilo, lakini usikubali kurudi nyuma. Watakuwa na hofu juu yako, wataona unaenda kujitesa bila ya sababu. Watakuonyesha mambo mazuri utakayoyapata kama utabaki nyumbani.

Lakini usikubali, huo ni mtego ambao ukiingia, unanasa moja kwa moja. Utaishia kuwa na maisha ya kawaida, lakini hutaweza kujenga utajiri mkubwa.

Kama unataka kuishi maisha ya kawaida na usifikie uwezo mkubwa ulio ndani yako, baki chini ya wazazi wako. Lakini kama una kiu ya mafanikio makubwa ndani yako, ondoka kwa wazazi wako na nenda kapambane kujenga maisha yako.

Utawaudhi wazazi wako kwa kufanya hivyo, lakini utakapofanikiwa, watakuelewa sana. Na usihofu kwamba vipi kama hutafanikiwa, kwa kupambana, utafanikiwa. Na hata kama hutafanikiwa, bado utabaki kuwa mtoto wao, utaweza kurudi na kuomba msamaha na ukasamehewa.

Usikubali kubaki kwenye hali ambayo umeshindwa kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako kwa sababu ya wazazi wako kukulinda. Nenda kapambane ufikie na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako.

SOMA; Wekeza Muda, Nguvu Na Fedha Kujenga Utajiri Mkubwa.

MZAZI TAJIRI KWA WATOTO WAKE.

Kama wewe ni mzazi tajiri na una watoto, hapa kuna sheria za kuzingatia ili utajiri wako usiwaharibu watoto wako na wakashindwa kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao.

1. Kamwe usiwaambie wala kuwaonyesha watoto wako una utajiri mkubwa. Waache waje wajue wenyewe wakiwa tayari ni watu wazima na wanaojitegemea.

2. Haijalishi una utajiri kiasi gani, wafundishe watoto wako nidhamu na ubahili, hivyo vitawasaidia sana.

3. Epuka kuwalinda watoto wako na changamoto, acha wapitie changamoto, ndiyo zinawakomaza.

4. Punguza mijadala ya nani atarithi nini kwenye mali zako. Kila mtoto ajue hana anachorithi hivyo akapambane kujenga mali zake.

5. Usitoe zawadi ya fedha au vitu vingine kwa watoto kama njia ya kuwafanya wakupende au kuwaridhisha.

6. Acha kuingilia maisha ya familia za watoto wako ambao ni watu wazima. Waache waishi vile wanavyoona inawafaa wao.

7. Usijaribu kushindana na watoto wako, kwa kuona labda wewe ulifanikiwa mapema kuliko wao. Waache watoto wakue kwa kasi yao wenyewe.

8. Mara zote kumbuka watoto wako ni watu binafsi na wanaotofautiana na watu wengine, usiwalinganishe na yeyote.

9. Weka mkazo kwenye mafanikio ambayo watoto wako wanapata, hata kama ni madogo, hilo litawasukuma kufanikiwa zaidi.

10. Wafundishe watoto wako kwamba fedha ni muhimu, lakini pia kuna vitu vingine muhimu kwenye maisha kama; afya, ustawi, maisha marefu, furaha, upendo, marafiki, sifa, heshima na uaminifu. Wawezeshe kujenga hayo muhimu na watakuwa na maisha bora.

Kama umezaliwa kwenye familia tajiri, ni wajibu wako kupambana sana ili usimezwe na utajiri wa wazazi wako. Hakikisha na wewe unaacha alama kwa kujenga utajiri ambao ni mkubwa kuliko wa wazazi wako. Hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako.

Kama ni mzazi ambaye umepambana na kuweza kujenga utajiri, epuka kuwaharibu watoto wako na utajiri huo. Nia njema unayokuwa nayo ya kuwasaidia watoto wako huwa inageuka kuwa madhara kwako. Walee kwa kuhakikisha wanapitia yale uliyopitia wewe ili nao waweze kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yao kufanya makubwa kama wewe. Usitumie utajiri wako kuwadhulumu watoto wako nafasi ya kuishi maisha yao.

Somo hili ni mwendelezo wa mfululizo wa masomo kutoka kitabu The Millionaire Next Door: The Surprising Secrets of America’s Wealthy kilichoandikwa na Thomas J. Stanley na William D. Danko. Masomo yote kutoka kwenye kitabu hicho yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mpana juu ya somo hili la urithi unavyokuwa kikwazo kwenye kujenga utajiri mkubwa. Fungua hapo chini kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.