Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya TANO.
Na kwenye kanuni ya TANO tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni mfanye mwingine ndiyo, ndiyo mapema.
Kwenye makubaliano na watu, usikimbilie kwenye yale mnayotofautiana, bali anzia kwenye yale mnayokubaliana kisha nenda taratibu ukipata ndiyo mpaka unafika kwenye yale mnayopingana na kuyapa ndiyo pia.
SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Tano
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi yetu ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya sita ambayo ni mpe mtu nafasi ya kuongea zaidi.
Mwandishi Dale Carnegie anatuambia kwamba, watu wamekuwa wanapoteza marafiki na kushindwa kuwashawishi watu kwa sababu wanapenda kuongea zaidi wao kuliko nafasi wanayowapa wengine ya kuongea.
Unapaswa kumpa mtu mwingine nafasi ya kuongea zaidi, na kwa kuwa watu huwa wanapenda kujieleza, wataeleza kila kitu na itakuwa rahisi kwako kujua namna gani ya kumshawishi akubaliane na wewe.

Hata kama hukubaliani na mtu kwenye kile anachoongea, usikimbilie kumkatisha, mwache ajieleze, muulize maswali ili ajieleze zaidi.
Na kwa njia hiyo, yeye mwenyewe ataona wapi hayuko sahihi na kuwa tayari kubadilika.
Pia, unapomkatisha mtu wakati anaongea na ukaongea wewe, jua kwa uhakika hata kusikiliza, badala yake ataendelea kupangilia hoja zake vizuri.
Hivyo, utakuwa umepoteza muda wako, mpe mtu nafasi ya kujieleza na utaona fursa nyingi za kumshawishi akubaliane na wewe.
Kitendo tu cha kumpa mtu nafasi ya kuongea, huku ukisikiliza kwa makini kinamfanya aone unamthamini na hivyo ataanza kukubaliana na wewe, hata kabla hujasema chochote.
Unapokuwa mtu wa kuongea zaidi na kuwanyima wengine nafasi ya kuongea, wengi watakuwa wanakukwepa. Wakikuona tu wanakukwepa, kama muuzaji, usiwe mwongeaji sana, bali mfanye mteja aongee zaidi kwa kumuuliza maswali zaidi.
Rafiki, hata kama mambo unayoongelea ni muhimu sana, tambua watu wanathamini zaidi kile walichonacho kuliko alichonacho mtu mwingine.
Kumbuka, asili ya binadamu ni wabinafsi, hivyo unapotaka sana wewe kuongea hawakupi kipaumbele, ila ukiwapa nafasi ya kuongea, itakuwa rahisi kwako kupata kile unachotaka kutoka kwao.
Kumpa nafasi ya kutoa alichonacho inamfanya ajione ni wa muhimu na hivyo kuwa tayari kukubaliana na wewe.
Kila wakati wewe kama muuzaji, unapaswa kujichukulia kama daktari ambaye yuko na mgonjwa.
Wewe unayeuza, ndiyo daktari, hupaswi kuongea sana, bali unapaswa kumuuliza mgonjwa wako ambaye ndiyo mteja wako kujua kile anachoumwa na uweze kumtibu.
Pata picha unaenda hospitali halafu daktari anakuwa anaongea yeye tu halafu hakupi wewe nafasi ya kuongea utajisikiaje? Lazima utajisikia vibaya. Kwa picha hiyo hiyo, chukulia unavyokuwa unaongea sana, ni kama vile unamkera mteja wako.
Dale anamnukuu mwanafalsa La Rochefoucauld ambaye amewahi kusema kama unataka maadui, fanikiwa kuliko marafiki zako na kama unataka marafiki waache marafiki zako wafanikiwe kuliko wewe.
Huwa tunaharibu urafiki na mahusiano yetu mengine kwa midomo yetu kuliko hata mafanikio tuliyopata. Pale tunapojisifia kila wakati kwa mafanikio yetu, huwa tunaibua wivu ndani ya watu watu hao.
Ondoa hilo kwa kuacha kuwa mtu wa kujisifia kwa mafanikio yako na wape watu nafasi ya kujieleza na kujisifia kwa mafanikio yao.
Hatua ya kuchukua leo; Wape watu nafasi ya kuongea zaidi, watajiona ni wa muhimu na unawathamini na hivyo kukubaliana na wewe.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504