Rafiki yangu mpendwa,
Watu wawili, ambao wanafanya biashara au kazi ya aina moja na kwenye eneo moja, wanaweza kutofautiana sana kwenye utajiri na mafanikio wanayoyapata.
Licha ya kuwa eneo moja na kukutana na fursa zinazofanana, wachache wanazitumia fursa hizo vizuri na kunufaika. Wakati wengi wanashindwa kutumia fursa hizo na hivyo kubaki chini.

Kwenye kitabu cha THE MILLIONAIRE NEXT DOOR, waandishi walifanya tafiti nyingi kwa walioweza kujenga utajiri na wanaobaki kwenye umasikini. Kupitia tafiti hizo, kwenye eneo la kazi na biashara, waliona vitu viwili vinavyowatofautisha matajiri na masikini.
KITU CHA KWANZA; KUCHANGAMKIA FURSA.
Waandishi waliona moja ya sababu zinazopelekea wengi kutokupata utajiri ni kushindwa kuchangamkia fursa nzuri zilizopo kwenye soko walipo.
Na fursa kubwa kabisa ni kuwalenga wateja ambao tayari ni matajiri. Matajiri wamekuwa wanafanya biashara zinazowalenga matajiri wengine, ambao tayari wana fedha za kutumia. Kwa njia hiyo, inakuwa rahisi kwao kukuza biashara zao.
Wanaobaki kwenye umasikini huwa wanashindwa kuwalenga matajiri na kuwauzia. Wanashindwa kuyaelewa mahitaji yao na kuweza kuyatimiza kwa viwango vya juu ambavyo wanataka. Maana matajiri huwa wanataka kupata thamani kubwa, kwa sababu bei siyo tatizo sana kwao.
Wafanyabiashara wanaobaki kwenye umasikini huwa wanatoa thamani ndogo na kulenga wale wanaotaka kwa bei rahisi. Wanakuwa wanakazana sana, lakini bado hawajengi utajiri, kwa sababu wateja wanaowalenga wanakuwa siyo sahihi.
Ili kujenga utajiri, anza kwa kulenga wateja sahihi. Ipo kauli ya IFUATE PESA au USIPISHANE NA GARI LA MSHAHARA. Wajibu wako ni kuangalia watu gani wenye matatizo unayoweza kuyatatua na gharama kwao siyo tatizo. Wape thamani kubwa sana ambayo hawawezi kupata mahali pengine na utaweza kufanya mauzo makubwa, kujenga biashara na kupata utajiri.
Hilo linawezekana kwa kila aina ya biashara ambayo inatatua matatizo ambayo watu wanayo au kutimiza mahitaji yao. Anza na tatizo, angalia wenye uwezo wa kumudu, wape thamani kubwa na fikia wengi wa aina hiyo. Utaweza kujenga biashara kubwa na kupata utajiri.
SOMA; Urithi Ni Kikwazo Kwenye Kujenga Utajiri Mkubwa.
KITU CHA PILI; MAPENZI KWENYE KILE WANACHOFANYA.
sehemu kubwa ya matajiri wamejiajiri au wanamiliki biashara zao wenyewe. Kile wanachofanya kinakuwa na mafanikio makubwa kwa sababu ya tabia ambazo wao wanakuwa nazo. Wanakuwa wameweka viwango vikubwa sana kwenye biashara zao ambavyo ni tofauti na kwingine.
Matajiri wamekuwa wanapenda sana biashara au kazi wanazofanya na wanajivunia kuweza kujenga mafanikio makubwa waliyofikia. Kwao kile wanachofanya ni muhimu kuliko kitu kingine chochote. Biashara au kazi zao ndiyo kipaumbele cha kwanza kwao.
Wanakuwa hawatafuti njia ya kutoroka kwenye shughuli zao au kuacha kufanya. Muda pekee ambao wanakuwa hawapo kwenye shughuli zao ni ule wa mapumziko ya lazima, kama kula, kulala, muda wa familia n.k. Nje ya hayo muhimu, hutawakuta sehemu nyingine isipokuwa kwenye shughuli zao.
Kupenda sana kile ambacho wanafanya kimekuwa na faida kubwa mbili kwa matajiri.
Faida ya kwanza ni kukifanya kitu kwa ukubwa na ubora sana kwa sababu umakini wao wote upo kwenye kile wanachofanya. Chochote ambacho kinapewa umakini mkubwa, huwa kinakua sana.
Faida ya pili ni kuwa na matumizi madogo na hivyo kuweza kujenga utajiri mkubwa. Kwa sababu matajiri hao wanakuwa hawana starehe yoyote nje ya shughuli zao, hawana matumizi ya anasa kama kufanya starehe au kununua vitu vya kujionyesha. Hilo linawafanya wawekeze zaidi kipato chao na kukuza utajiri wao.
Ili kujenga utajiri, chagua kazi au biashara ambayo unaipenda kweli kutoka ndani ya moyo wako. Ambayo una msukumo mkubwa wa kuifanya kutoka ndani yako na husubiri kusukumwa ili kuifanya. Muda wako mwingi uweke kwenye shughuli zako na siyo nje ya hapo. Fanya kwa ukubwa na ubora na usiwe na matumizi mengi nje ya biashara au kazi yako.
Kwa kufanya hivyo, utaweza kujenga utajiri mkubwa na ambao unaufurahia, tofauti na wale wanaohangaika na starehe ambazo hazidumu kwa muda mrefu.
Fanyia kazi mambo haya mawili; kuchagua fursa zinazowalenga matajiri na kufanya kile unachopenda na kwa hakika utajenga mafanikio na utajiri mkubwa.
Kwa muhtasari;
1. Anza na kile unachopenda.
2. Angalia tatizo ambalo unatatua kwa unachopenda kufanya.
3. Angalia wenye uwezo mkubwa wa kifedha na wana tatizo hilo, walio tayari kulitatua.
4. Wape suluhisho la tatizo hilo kwa namna ambayo wanapata thamani kubwa na wasiyoweza kuipata mahali pengine.
5. Wafikie wengi ambao wana uwezo wa kumudu kulipa kile unachotoza na wape thamani kubwa huku ukiboresha nao mahusiano.
Fanyia kazi mwongozo huo na utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Somo hili ni mwendelezo wa mfululizo wa masomo kutoka kitabu The Millionaire Next Door: The Surprising Secrets of America’s Wealthy kilichoandikwa na Thomas J. Stanley na William D. Danko. Masomo yote kutoka kwenye kitabu hicho yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mpana juu ya somo hili la fursa za kutumia ili kujenga utajiri mkubwa. Fungua hapo chini kujifunza.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.