Rafiki yangu mpendwa,

Wakati unaishi maisha ya kawaida, yaani kabla hujaamua kupambana ili kufanikiwa, utawaona watu wengi wanaokuzunguka ni wema kwako.

Utaona watu hao wanakutakia mema kwenye maisha yako, wakitaka sana ufanikiwe kadiri ya unavyotaka. Wataonekana hata kukushauri na kukutia moyo ili uweze kufanikiwa.

Lakini pale utakapoanza kuyapa mafanikio umakini wako mkubwa, kwa kudhamiria kweli kufanikiwa, ndiyo utawajua watu hao kwa uhalisia wao.

Kwani wengi wanaokuzunguka hawatafurahishwa na maamuzi yako ya kutaka kupata mafanikio makubwa. Wanakuwa wanataka ufanikiwe, lakini ni kwa kiwango cha kawaida, kama ambacho wanacho wao.

Pale unapotaka kupata mafanikio makubwa kuliko yale ambayo wao wanayo, hawatakuacha ufanye hivyo. Bali watakuwa kikwazo kikubwa kwako kufanikiwa.

Kama unataka kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unapaswa kuwa na ujasiri wa kuwapuuza na kuwakataa watu wote ambao wanayapinga mafanikio hayo. Hilo linakutaka sana uwe na ujasiri kwa sababu halitakuwa rahisi, maana ni watu wa karibu kabisa kwako.

Wanaokukatisha tamaa usifanikiwe, huwa wanatumia njia mbalimbali ambazo unaweza usijue kama lengo lao ni kukukatisha tamaa.

Moja ni kukutaka uridhike na ulichonacho.

Pale unapotaka kupata mafanikio makubwa, wanaokuzunguka watakutaka uridhike na kile ulichonacho. Kwa sababu wao wameridhika na matokeo madogo, wanataka na wewe uridhike pia.

Wewe usikubali kuridhika, endelea kutaka makubwa zaidi ya yale uliyonayo. Hata kama umefika juu kiasi gani, jua unaweza kufika juu zaidi ya hapo.

Mbili ni kushawishi kwamba haiwezekani.

Pale unapotaka kupata mafanikio makubwa, wanaokuzunguka watakuonyesha ni jinsi gani mafanikio unayoyataka hayawezekani. Watakuambia hakuna mwingine amewahi kufanya na hata waliojaribu hawakuweza kupata waliyotaka. Wataonekana kutaka kukuzuia usiumie, lakini kote ni kukukwamisha.

Wewe usiwasikilize wengine kwamba nini kinawezekana na nini hakiwezekani, sikiliza nafsi yako, kile inachotaka ndicho kinachowezekana. Fanyia kazi chochote unachotaka na utakifanya kuwezekana.

SOMA; ONGEA NA COACH; Kitu Kimoja Muhimu Ninachotaka Wewe Ukijue Kila Siku.

Tatu ni kukuonyesha wale walioshindwa.

Wanaokuzunguka wakiona umeendelea kufanya licha ya kukuambia haiwezekani, wataenda hatua ya ziada kukuonyesha watu waliojaribu na kushindwa. Lengo ni kukujaza hofu ili uache na kubaki chini kama wao. Watakupa mifano ya wengi waliokuwa wanataka makubwa kama wewe na wakaishia kuanguka na kupoteza.

Wewe kataa kupata hofu kwa sababu kuna wengine walishindwa. Kushindwa wao haimaanishi na wewe utashindwa. Badala yake jua kwa nini walishindwa ili usirudie makosa yao.

Nne ni kukukwamisha makusudi.

Kama utaendelea licha ya kuonyeshwa walioshindwa, wanaokuzunguka bado hawatakuacha uendelee. Badala yake wanakukwamisha makusudi. Hapa watakuzuia usitumie vitu unavyohitaji au kuziba fursa mbalimbali zinazokuwa zinafunguka mbele yako. Wanahakikisha wanaharibu kila kinachokwenda vizuri kwako ili ushindwe na waonekane walikuwa sahihi.

Wewe hakikisha wale wote ambao hawana mchango wa wewe kupata mafanikio makubwa unayoyataka, hawapati nafasi ya kuwa karibu na wewe na kujua yale yanayoendelea kwenye maisha yako. Kuwa na tahadhari na kila mtu na unapoona mtu anakukwamisha, usiendelee kumpa nafasi. Unahitaji kushirikiana na wale wanaoyapambania mafanikio yako na siyo kuyakwamisha.

Tano ni kukusema vibaya.

Ukiwashinda kila mahali na ukafanikiwa, wale wanaokuzunguka hawatataka kukiri ushindi wako. Badala yake watakusema vibaya kwa yale uliyofanya na kufanikiwa. Watakuwa wakosoaji wa kila unachofanya. Makosa unayofanya, hata kama yanafanywa na wengine, kwako yataonekana ni mabaya zaidi.

Wewe jua unapofanikiwa utatengeneza maadui wengi ambao watataka sana kukuona unaanguka. Hakikisha huwapi nafasi ya kushuhudia hilo likitokea. Endelea kupambania kujenga na kulinda mafanikio yako ili usikwamishwe na yeyote.

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini uendelee kujifunza kwa kina kuhusu kuwapuuza wote ambao hawana mchango kwenye mafanikio yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.