Kila kiungo ambacho sisi binadamu tunacho kwenye miili yetu, kipo kwa wanyama pia.

Ukimwangalia mnyama kama mbuzi, ana ubongo ambao unao, ana macho ambayo unayo, ana moyo na vingine.

Lakini pia wanyama hao wana michakato kama tuliyonayo binadamu, wanakula na sisi tunakula, wanazaliana na sisi tunazaliana mpaka kifo pia tunafanana.

Swali la kujiuliza ni sisi binadamu tunatofautianaje na hao wanyama wengine? Nini kinatufanya sisi binadamu tuweze kuwawinda na kuwatawala hao wanyama wengine?

Hilo ni swali ambalo kwa kujua majibu yake na kuyafanyia kazi, kunatufanya sisi binadamu kuwa wa kipekee na kuweza kufanya makubwa kabisa.

Kuna vitu viwili vinatufanya sisi binadamu kuwa juu ya viumbe wengine wote. Vitu hivyo ni FIKRA na DHAMIRA.

Fikra ni uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi mbalimbali, kitu ambacho wanyama hawana. Wao wanafanya kile ambacho wamekuwa wanafanya, hawakai na kufikiri.

Dhamira ni kujua mema na mabaya na kufanya maamuzi kwa msingi huo, kitu ambacho wanyama hawana. Wanafanya kile ambacho ni asili yao na wanasukumwa kufanya, hawajiulizi kama ni wema au ubaya.

Ili kuwa bora kwenye maisha yetu kama binadamu, tunapaswa kuendeleza maeneo hayo mawili ambayo ndiyo yanatutofautisha. Hiyo ni kazi na wajibu wetu mkubwa hapa duniani.

Falsafa ya Ustoa inatupa misingi sahihi ya kufanyia kazi ili kuweza kujijenga vizuri kwenye eneo la fikra na dhamira.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu; How To Be A Stoic (Jinsi Ya Kuitumia Falsafa Ya Ustoa Kuwa Na Maisha Bora).

Mstoa Marcus Aurelius, kwenye kitabu chake cha nane cha Meditations, ametushirikisha jinsi tunavyoweza kujenga FIKRA SAHIHI na DHAMIRA SAFI na hivyo kupelekea kuwa bora kwenye maisha yetu.

Kwenye kitabu hicho kuna haya ya msingi sana aliyoshirikisha, tunayopaswa kufanyia kazi ili kupiga hatua.

1. Kitu chochote kinachokuzuia kufikiri kwa usahihi ni kikwazo kwako kuishi kwa asili yako. Hapa tunapaswa kuhakikisha tunaondoa vikwazo vyote vinavyoathiri fikra zetu, ikiwepo usumbufu na hisia kali. Tusipoweka udhibiti kwenye hisia, hatuwezi kufikiri kwa usahihi.

2. Kama hujawahi kuwaumiza wengine kwa makusudi, kwa nini unakuwa tayari kujiumiza mwenyewe? Mara nyingi huwa tunaepuka kuwaumiza wengine, lakini tunaishia kujiumiza sisi wenyewe. Tunapaswa kuacha hilo mara moja.

3. Watu huwa wanapendelea vitu mbalimbali, wajibu wetu ni kupendelea fikra sahihi na dhamira safi. Fikiri na kufanya maamuzi sahihi kwako na fanya yale yaliyo sahihi mara zote.

4. Ishi kwenye wakati uliopo na acha kujihangaisha na wakati ujao, kwa sababu hauna udhibiti nao. Kuhangaika na yajayo, ambayo bado hujayafikia ni kujizuia kuishi kwa usahihi kwenye wakati uliopo.

5. Haijalishi unapitia mambo gani, nafsi yako inapaswa kubaki kwenye utulivu mkubwa. Kuwa na misingi ambayo unaisimamia na mara zote baki kwenye misingi hiyo bila ya kujali ni nini unapitia.

6. Kila kinachotokea kwako, ni asili yako na una uwezo wa kukihimili. Asili haiwezi kuruhusu kitu kikutokee ambacho huwezi kukihimili au kukikabili. Pale unapopitia mambo ambayo unaona yanakuzidi, jikumbushe hili muhimu kwamba yote yanayotokea yapo ndani ya uwezo wako kuyabadili au kuyakubali.

7. Kama kuna kitu chochote kinachokusumbua, tambua kinachokusumbua siyo kitu hicho, bali maoni yako juu ya kitu hicho. Una nguvu ya kutokusumbuliwa na chochote kwa kuacha maoni yasiyo sahihi unayokuwa nayo juu ya vitu mbalimbali.

8. Akili yako inakuwa imara pale inaposimama kwenye misingi yake na kutokufanya yale ambayo haitaki kuyafanya. Kwa kuweza kudhibiti hisia, akili inakuwa ngome imara. Hakikisha akili yako inasimama kwenye misingi sahihi ili uweze kuwa imara kwenye maamuzi unayofanya.

9. Usiongeze chumvi kwenye vitu, hiyo ndiyo inayokuumiza. Kama umeambiwa mtu alikuwa anakusema, hicho ndiyo kimetokea. Wewe kutafsiri kwamba mtu kukusema ni vibaya na hivyo unapaswa kuumia, ni kuchagua kujiumiza mwenyewe. Ukiacha kuongeza chumvi kwenye mambo, hayawezi kuwa na nguvu ya kukusumbua.

10. Kama kuna kitu hukitaki, unapaswa kukibadili na kama huwezi kukibadili basi achana nacho au kivumilie. Inashangaza jinsi ambavyo watu wanatumia muda mwingi kulalamikia vitu ambavyo hawavitaki na hakuna hatua yoyote wanayochukua. Mwishowe ni maisha yao kuwa ya hovyo. Wewe usikubali kuyaharibu maisha yako kwa malalamiko yasiyo na tija, chukua hatua sahihi.

Haya ni baadhi ya mambo muhimu tunayojifunza kutoka falsafa ya Ustoa ya kutuwezesha kuwa na fikra sahihi na dhamira safi. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini kuna mambo mengine 10 zaidi na mjadala ambao tumekuwa nao juu ya kujenga fikra sahihi na dhamira safi. Karibu ujifunze zaidi kwenye kipindi hicho.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.