Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye #HadithiZaKocha ambapo leo tunakwenda kupata kisa cha farasi aliyepotea. Soma kwa makini na upate somo lililo nyuma ya hadithi hii na kisha kushirikisha kile ulichojifunza.
Kwenye kijiji kimoja, aliishi mkulima mmoja ambaye alizungukwa na majirani waliokuwa wanashirikiana kwenye mambo mengi.

Mkulima huyo alikuwa na farasi ambaye alikuwa anamtumia kwenye majukumu mbalimbali ya shambani.
Siku moja farasi yule aliondoka na hakurudi tena. Mkulima alishindwa kutekeleza sehemu kubwa ya majukumu yake. Jirani zake walikuja kumpa pole na mazungumzo yao yalienda hivi;
Majirani; Pole sana jirani kwa bahati mbaya uliyopata ya kupotelewa na farasi wako.
Mkulima; Asanteni sana majirani.
Majirani; Kwa hiyo utafanyaje sasa kwa hii bahati mbaya uliyokutana nayo?
Mkulima; Tunaona jinsi itakavyokuwa.
Baada ya siku tatu, yule farasi alirudi, akiwa ameongozana na farasi wengine wawili. Mkulima alimfunga farasi wote kwenye banda lake. Majirani waliposikia habari hizo walikuja kumpa pongezi kwa kupata farasi wa ziada. Mazungumzo yakawa hivi;
Majirani; Hongera sana jirani kwa bahati nzuri ya kupata farasi wa ziada.
Mkulima; Asanteni sana majirani.
Majirani; Kwa hiyo unakwenda kuwatumiaje hawa farasi wa ziada uliowapata?
Mkulima; Tutaona jinsi itakavyokuwa.
Siku iliyofuata, kijana wa mkulima alikuwa anawafunga wale farasi wengine na akapigwa teke na kwenda kuangukia mbali. Hilo lilipelekea kuvunjika mguu na hivyo kushindwa kufanya kazi. Majirani walipopata taarifa hizo walikuja kumpa pole. Mazungumzo yakawa;
Majirani; Pole sana jirani kwa bahati mbaya ya kijana wako kuvunjwa mguu na farasi.
Mkulima; Asanteni majirani.
Majirani; Kwa hiyo unakwenda kufanyaje sasa kwa hii bahati mbaya ya kijana wako kuvunjika mguu?
Mkulima; Tutaona jinsi itakavyokuwa.
SOMA; #HadithiZaKocha; Kisa Cha Kuku Anayetaga Mayai Ya Dhahabu.
Wiki moja baadaye nchi iliingia kwenye vita, amri ikatolewa kwa vijana wote kwenda kupigana vita. Kijana wa mkulima kwa sababu alikuwa amevunjika, hakuchukuliwa kwenda vitani. Majirani walipopata habari hizo wakaja kumpongeza. Mazungumzo yakawa;
Majirani; Hongera jirani kwa bahati nzuri ya kijana wako kutokwenda vitani, hayupo kwenye hatari ya kifo kama wengine.
Mkulima; Asanteni majirani.
Majirani; Kwa hiyo unakwenda kutumiaje bahati hii nzuri ya kijana wako kutokuwa kwenye hatari ya kifo?
Mkulima; Tutaona jinsi itakavyokuwa.
Majirani hawakuwa wanaweza kumwelewa kabisa mkulimo huyo, lakini waliona maisha yake yakienda vizuri sana.
Karibu ushirikishe nini umejifunza kwenye kisa hiki na unakwendaje kutumia hayo uliyojifunza kwenye maisha yako ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio makubwa. Weka maoni yako kwa kile ambacho umejifunza.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA pia nimesimulia kisa hiki, unaweza kuangalia hapo chini na kushirikisha yale uliyojifunza. Karibu sana.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.