Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Kabla hujawa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Unakuwa mtu bora pale unapojifunza na kuchukua hatua kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kwa kujitambua wewe mwenyewe na kufanya yale yaliyo sahihi, ndiyo unaweza kupata mafanikio kwenye kila eneo la maisha yako.

Kabla ya kufanikiwa, ni lazima mtu uwe na malengo na mipango ya kufanyia kazi ili kufikia malengo hayo. Walio wengi huwa wanadhani kazi ya kuweka malengo na mipango ni kubwa na wakishafanya hivyo basi inatosha.

Ukweli ni kwamba kwenye mafanikio, kuweka malengo na kupanga mipango ina mchango wa asilimia 1 tu ya mafanikio. Hamasa kubwa ya kufikia malengo hayo ina mchango wa asilimia 9. Asilimia 90 inayobaki ya kufikia malengo yoyote yale iko kwenye kuweka KAZI hasa. Kazi ambayo ni kubwa na isiyo na kuchoka wala kukata tamaa.

Watu wengi wamekuwa ni wa maneno kuliko vitendo. Wakisema sana, kuahidi na kulalamika, lakini hakuna hatua ambazo wanachukua. Kwenye maisha, hakuna kitu chochote kinachoweza kutokea kama hakuna hatua inayochukuliwa. Hivyo kama unataka mafanikio kwenye eneo lolote, unapaswa kuacha kuwa mtu wa maneno na uwe mtu wa vitendo.

Kinachofanya maneno yasiwe na mchango kwenye mafanikio ni urahisi wake. Ukishaona kitu ni rahisi na kila mtu anaweza kukifanya, basi jua hakiwezi kuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio. Utafanya maamuzi bora sana ya kimafanikio kama utaacha kuhangaika na yale ambayo wengi wanafanya, kwa sababu hayawezi kukupa mafanikio makubwa unayoyataka.

Sehemu ya maneno ambayo imewakwamisha wengi kufanikiwa ni kulalamika. Pale watu wanapokutana na vikwazo na changamoto mbalimbali kwenye safari yao ya mafanikio, huwa wanatafuta cha kulalamikia. Kulalamika ni rahisi, lakini hakujawahi kubadili chochote. Vitu vinabadilishwa kwa kuchukua hatua. Hivyo wewe unapokutana na vikwazo na changamoto, angalia nini unaweza kufanya ili kubadili yale unayokuwa umekutana nayo.

SOMA; 3374; Uvivu na kushindwa.

VITENDO UNAVYOPASWA KUONYESHA ILI KUFANIKIWA KWENYE MAUZO.

Kama ambavyo tumekuwa tunajifunza, ushindi kwenye mauzo ni pale unapoweza kukamilisha mauzo. Ni labda unauza au unauziwa, unauza pale mteja anapokubali kununua na unauziwa pale mteja anapokataa kununua na wewe ukakubaliana naye.

Unachotaka wewe ni ushindi kwa kukamilisha mauzo, kuwafanya wateja wakubali kununua. Ili kufanikisha hilo, unahitaji kuwa mtu wa vitendo na siyo maneno tu. Vitendo vya msingi unavyopaswa kuwa navyo ni kama ifuatavyo;

1. Kuziishi tabia za mafanikio.

Umejifunza tabia nyingi za mafanikio, hazitakuwa na manufaa kwako kama hutaziishi kwa vitendo. Kuamka asubuhi na mapema, kujifunza, kuwa na mtazamo chanya, kuwa mwaminifu na tabia nyingine ni muhimu kwako kufanikiwa.

Kwa kujua tu hizo tabia haitakuwa na manufaa kwako, ni lazima uziweke kwenye matendo. Katika kuziishi tabia za mafanikio kwa matendo hutakuwa mkamilifu, kuna wakati utateleza kwenye hayo. Hupaswi kukata tamaa pale hayo yanapotokea, badala yake unapaswa kurudi kwenye kuziishi tabia hizo.

Ni bora kufanya kidogo kuliko kutokufanya kabisa, kwa sababu chochote unachofanya huwa kinaleta mchango kwenye matokeo unayoyapata.

2. Kutekeleza mchakato wa mauzo.

Una mchakato wa mauzo ambao unatakiwa kuutekeleza ili kuweza kutekeleza majukumu yako ya mauzo na kupata matokeo mazuri. Mchakato huwa unafanya kazi pale unapofanyiwa kazi. Lakini wengi hawafanyii kazi na hivyo hawapati matokeo mazuri na mwishowe kuona mchakato haufai.

Kabla hujasema kitu hakifai, au kutaka kukibadili, kwanza unatakiwa ukifanyie kazi kwa ukubwa kabisa. Kwa sababu kila kitu huwa ni kigumu mwanzoni na matokeo yake kuchelewa. Kama hutaweka juhudi kubwa kwenye kitu na kwa muda, hutaweza kupata matokeo makubwa unayoyataka.

Na hiyo ndiyo sababu kwa nini watu wengi huishia kufanya vitu vingi na bado hawafanikiwi. Kwa sababu huwa hawaweki juhudi za kutosha na muda kwenye kitu. Wanategemea vitu viwe rahisi na matokeo ya haraka. Pale wanapokutana na ugumu na matokeo kuchelewa, wanakosa uvumilivu na kuacha, kisha kwenda kwenye vitu vingine.

Mchakato wako wa mauzo ufanyie kazi kwa ukubwa na kuupa muda kwanza kabla ya kutaka kuubadili au kuachana nao. Kwa hatua zozote utakazochukua, kuna matokeo utakayoyazalisha na hayo yatakupa funzo zaidi.

Kwa kufanya utajifunza zaidi kuliko kutokufanya. Hata kama matokeo utakayoyapata kwenye kufanya siyo uliyokuwa unayategemea, yatakupa funzo ambalo usingeweza kulipata kama usingefanya.

3. Kutekeleza yote unayoahidi.

Kuahidi huwa ni rahisi, kutekeleza ndipo ugumu huanzia. Ili kupata kile wanachotaka, watu huwa tayari kuahidi chochote. Lakini unapofika wakati wa kutekeleza ahadi zao, huanza kutafuta sababu na visingizio.

Unaweza kutoa sababu na visingizio vizuri na ambavyo vinaeleweka kwa nini umeshindwa kutekeleza yale uliyoahidi, lakini jua hutaaminika. Hata kama ni kweli umekutana na mambo ambayo yamekuzuia kabisa kutekeleza, bado watu hawatakuamini kwenye ahadi zako nyingine.

Hivyo kama unataka kuwa mtu unayeaminika, ambayo ni nguzo muhimu sana kwenye mauzo, tekeleza yote unayoahidi. Utaweza kutekeleza yote unayoahidi kama utakuwa mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno. Hata kama hutaweza kutekeleza kwa asilimia 100, kitendo cha kuchukua hatua, kinawafanya watu waone jinsi ambavyo umedhamiria na kujitoa juu ya kitu na hilo linafanya uaminike zaidi.

Kwa kila unachoahidi, anza kuchukua hatua mara moja, fanya kwa vitendo. Hata kama utashindwa, kwa kuwa umefanya, watu wataona, watakuelewa na kuendelea kukuamini. Lakini kama utakuja mikono mitupu na kuanza kutoa sababu ambazo zinatia huruma, watu watakuonyesha huruma, lakini hawatakuwa na imani na wewe tena.

Poteza kila kitu lakini siyo kuaminika, maana imani ikishapotea huwa ni vigumu kujengeka tena. Imani ikishapotea mambo mengine yanakuwa magumu sana kufanikisha.

Kwenye zama hizi ambazo watu wanaahidi lakini hawatekelezi, ukiwa mtu wa kutekeleza kwenye yote unayoahidi, utajitofautisha sana na wengine na hilo litaleta fursa nzuri kwako.

Kuwa mtu wa vitendo hakuhitaji uwe na uwezo wowote mkubwa zaidi ya ulionao sasa. Bali kunakutaka uwe na ari ya kuchukua hatua kwenye kila lililopo mbele yako. Jijengee tabia hii kwa kuanza na mambo madogo madogo na kukuza hilo zaidi.

Wauzaji wote bora ni watu wa kuchukua hatua kwenye malengo na mipango wanayoweka, kuwa hivyo pia na utaweza kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.