Rafiki yangu mpendwa,
Ili kujifunza kwa wale waliofanikiwa, hatupaswi kuyaangalia maisha yao ya sasa, bali tunapaswa kuangalia kule walikotoka.
Unapoyaangalia maisha ya wale waliofanikiwa, wakati ambapo wameshafanikiwa, kuna mengi unakuwa huyaoni, ambayo waliyapitia huko nyuma. Hayo ndiyo yanakuwa na funzo kubwa sana kwako kama unataka kufanikiwa.

Marshall Bruce Mathers III, maarufu kama Eminem ni mwanamuziki wa mtindo wa Rap wa nchini Marekani. Ameshinda tuzo nyingi za Grammy, ambazo ni tuzo za juu kabisa kwenye sanaa. Lakini pia anatajwa kama rapa bora kabisa wa nyakati zote.
Ukiwa unasoma maelezo ya mtu aliyefika ngazi za juu hivyo kwenye sanaa yake, unaweza kuona mambo yake yalikuwa rahisi. Lakini utakuwa umekosea sana, kwani Eminem alipitia magumu sana kabla hajafanikiwa kwenye muziki.
Picha linaanza baba yake mzazi anawakimbia akiwa na miezi mitatu tu. Hapo ndipo maisha ya mateso yalipoanzia, kwani mama yake hakuwa na kazi ya uhakika. Walilazimika kuhama miji kila baada ya miezi mitatu. Hilo lilimfanya asiweze kufanya vizuri shuleni na asiweze pia kuwa na marafiki.
Shuleni nako mambo hayakuwa mazuri, hakuwa anafanya vizuri na alikuwa anaonewa sana na wanafunzi wengine. Alirudia darasa la tisa kwa miaka mitatu bila kuweza kuvuka. Mpaka akaamua kuachana na shule kabisa.
Kilichomsaidia Eminem alikuwa anapenda kusoma vitabu vya hadithi na kamusi, alipenda kujua maana ya maneno mbalimbali. Zoezi hilo lilimpelekea kupenda fasihi ya Kiingereza na kumwezesha kuandika mashairi ya nyimbo zake.
Eminem alipotambulishwa kwenye muziki wa rap, aliona huo ndiyo ulimwengu wake. Kwani alitumia muda wake mwingi kuandika mashairi ya nyimbo na kushiriki mashindano mbalimbali ya kurap.
Alikutana na kikwazo cha ubaguzi, kwa sababu eneo walilokuwa wanakaa kulikuwa na Wamarekani weusi wengi huku yeye akiwa mweupe. Na hata muziki wa rap ulionekana ni wa watu weusi na siyo weupe.
Bado maisha ya Eminem yaliendelea kuwa magumu, na kama hayo hayakutosha, alijikuta pia amepata mtoto. Alilazimika kufanya kazi kwenye migahawa ili kupata fedha ya kuendesha maisha.
Alipambana kutoa albamu yake ya kwanza, akiona huo ndiyo utakuwa ufunguo wa ndoto na mafanikio yake. Lakini albamu hiyo ilikataliwa kabisa, watu hawakuielewa na walimkatisha tamaa kwamba hawezi kurap.
SOMA; Jifunze Ung’ang’anizi Wa Rambo Ili Uweze Kupata Mafanikio Makubwa.
Maisha yake yalizidi kuwa magumu maana hata kazi hakuwa nayo tena. Aliishia kwenye matumizi ya vilevi na madawa ya kulevya ili kupooza ukali wa maisha. Alifika hatua ya kukata tamaa na kutaka kujidhuru. Lakini aliamua kuweka kila kitu kwenye muziki wake ili kuona nini anaweza kupata.
Aliweka kazi kubwa sana na akatoa albamu yake ya pili. Hii ilikuwa na mapokeo mazuri na kuanzia hapo akajulikana na ukuaji wake mkubwa wa muziki na maisha kuanzia hapo.
Kuna mengi sana ya kujifunza kupitia safari hiyo ya maisha ya Eminem. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri wa kushirikishana hayo tunayojifunza. Karibu usikilize kipindi hicho ujifunze na kwenda kuyaweka kwenye maisha ili na wewe ufanikiwe.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.