Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Kila biashara na kwa kila wakati inakuwa inahitaji wateja zaidi na mauzo zaidi. Vitu hivyo viwili vipo kwenye kila biashara na vinapofanyiwa kazi ndiyo biashara inafanikiwa.

Ili kutekeleza mahitaji hayo mawili, kila biashara inapaswa kuwa na mchakato wake sahihi na unaofanyiwa kazi na watu wote waliopo kwenye biashara. Mchakato unapaswa kuhusisha kutengeneza wateja wapya tarajiwa na kuwafuatilia wateja wote bila ya kukoma.

Zipo njia mbalimbali za biashara kuwafikia wateja walengwa na moja ya njia hizo ni MATANGAZO YA KUCHAPA.

Matangazo ya kuchapa ni maelezo kuhusu biashara ambayo yanawafikia wateja kwa njia ya kuchapwa. Matangazo hayo yanawafikia wateja kupitia vitu ambavyo huwa wanavisoma na hivyo kupata taarifa za biashara husika.

NJIA ZA MATANGAZO YA KUCHAPA KUWAFIKIA WATEJA.

Zipo njia mbalimbali za matangazo ya kuchapa kuwafikia wateja wanaolengwa. Njia kuu tano ni kama ifuatavyo;

Moja; Magazeti.

Hapa matangazo yanakuwa yamechapwa kwenye magazeti na hivyo wasomaji kukutana nayo wakati wa kusoma magazeti hayo. Kwa kuwa watu huwa wanatumia muda mwingi kusoma magazeti, huwa wanapata muda mrefu pia wa kuliona tangazo husika na hivyo kuwa na ushawishi zaidi.

Tangazo la gazeti linapokuwa kubwa, mfano kujaza ukurasa mzima na kuwa na picha nzuri, linakuwa na ushawishi zaidi.

Mbili; Majarida.

Majarida ni machapisho ambayo huwa yanasomwa kwa muda mrefu zaidi kuliko magazeti. Majarida huwa yanakuwa yanalenga watu wa aina fulani na eneo fulani. Watu hukaa na majarida kwa muda mrefu zaidi. Pia majarida huwa yanachapwa kwa rangi kurasa zake zote, huku zikiwa na ubora mkubwa na hivyo kudumu zaidi. Hayo yote yanafanya tangazo kuonekana kwa wasomaji wa jarida kwa muda mrefu na hivyo kuongeza ushawishi.

Tatu; Posta.

Hapa matangazo yanachapwa kama vipeperushi na kisha kutumwa kwa walengwa kwa njia ya posta. Kwa njia hii matangazo yanawafikia walengwa moja kwa moja. Kwa watu ambao bado wanapokea mawasiliano yao kwa njia ya posta, hasa ambao wana uwezo mzuri kifedha, njia hiyo huwa na ushawishi mkubwa kwao. Japo matangazo mengi hutupwa, pale tangazo linapokuwa la tofauti, linapata nafasi ya kuonekana.

Nne; Mabango.

Mabango makubwa yanayowekwa kwenye maeneo mbalimbali, kama barabarani huwa ni njia nyingine ya matangazo ya kulipia kuwafikia walengwa. Mabango yana nguvu ya kuwafikia watu wanaokuwa kwenye eneo ambalo bango husika lipo. Kwa mfano kwenye mabango ya barabarani, hasa maeneo yenye makutano, kituo au foleni, matangazo yanaonekana kwa wengi zaidi na kwa muda mrefu.

Tano; Ana kwa ana.

Matangazo pia yanaweza kutolewa kwa watu ana kwa ana na hivyo kuwafikia watu kwa uhakika zaidi. Hapa matangazo yanakuwa yamechapwa kama vipeperushi au njia nyingine kisha watu kupewa. Wanaweza kupewa nyumba kwa nyumba, ofisini, njiani au kwenye mikusanyiko mikubwa. Japo wengi wanaweza kutupa matangazo hayo, pale yanapokuwa yameandaliwa vizuri, watu huvutiwa kuyachukua.

Njia hizo mbalimbali za matangazo ya kuchapa kuwafikia watu zina nguvu na ushawishi, hasa pale tangazo linapokuwa limeandaliwa vizuri kwa njia ambayo linakuwa na ushawishi mkubwa.

SOMA; Kufikia Wateja Wengi Kwa Kutumia Vipeperushi.

FAIDA ZA MATANGAZO YA KUCHAPA.

Pamoja na kuwa kwenye zama za kidijitali na mambo mengi kwenda kwa mfumo huo, bado matangazo ya kuchapa yana faida kubwa kwa upande wa kuwafikia watu na kuwa na ushawishi mkubwa kwao.

Zifuatazo ni faida kubwa za kutumia matangazo ya kuchapa kuwafikia wateja wengi zaidi.

1. Kuwafikia wateja kwa njia za kipekee.

Matangazo ya kuchapa, ambayo yanawafikia wateja kwa njia ya machapisho, huwa yanawafikia kwa njia ya kipekee ambayo ni tofauti na matangazo mengine. Matangazo yanayowafikia kwa magazeti na majarida huwa yanawakuta wakiwa na utulivu mkubwa wakati wa kusoma na hivyo kutumia muda mwingi kwenye tangazo husika. Hilo linafanya matangazo ya kuchapa kuwa na ushawishi mkubwa zaidi.

2. Wateja kutumia muda mwingi kuangalia tangazo.

Matangazo ya kuchapa yanakaa na watu kwa muda mrefu kuliko matangazo ya aina nyingine. Matangazo ya mitandaoni au ya TV na redio huwa yanasikika kwa muda na nguvu yake huwa ni kwenye kurudia rudia. Lakini tangazo kwenye gazeti, jarida au lililomfika mtu moja kwa moja, anakuwa nalo kwa muda mrefu, kwa sababu anakuwa na chapisho kwa muda mrefu. Kadiri mteja anavyokuwa analiona tangazo kwa muda mrefu, ndivyo anavyoshawishika zaidi.

3. Wateja kupata taarifa nyingi zaidi.

Matangazo ya kuchapa yanaweza kubeba taarifa nyingi zaidi. Taarifa zinaweza kuwa upande wa maelezo yanayokuwepo kwenye tangazo. Lakini zaidi ni kwa picha na rangi zinazotumika kwenye tangazo husika. Kama ambavyo husemwa, picha moja ni sawa na maneno elfu moja, hivyo matumizi ya picha zinazosadifu vitu vingi inawafanya wateja wanaopata matangazo ya kuchapa kupokea taarifa nyingi zaidi. Taarifa nyingi na zenye ushawishi huwa zinakuwa na nguvu ya kuwafanya wateja kuchukua hatua.

4. Bidhaa/huduma kuonekana ya thamani kubwa zaidi.

Tangazo linapokuwa limewekwa kwenye gazeti au jarida, linawafanya watu waone kitu hicho ni cha thamani kubwa zaidi. Hiyo ni kwa sababu watu huchukulia magazeti na majarida kama vyanzo sahihi zaidi vya habari. Hivyo wanapokutana na matangazo huko, wanaona ni sahihi pia. Kadhalika matangazo ya kwenye mabango makubwa ya barabarani, yanawafanya watu waone biashara ni ya hadhi ya juu mpaka kuweza kumudu kutangaza kwenye maeneo ambayo ni biashara chache zinazoweza kufanya hivyo.

5. Kuwafikia wateja wa aina fulani au eneo fulani.

Matangazo ya kuchapa yana nguvu ya kuwafikia watu wa aina au eneo fulani. Kwenye magazeti na majarida, huwa yanalenga watu au eneo. Majarida yapo ya aina mbalimbali na yanayolenga watu mbalimbali, kadhalika kwa magazeti. Kuna ambayo yanalenga vijana, wanawake, watu wazima, wapenda michezo, majarida ya kitaalamu na kadhalika. Kwa njia hiyo tangazo linaweza kuwafikia wale wanaolengwa. Kadhalika kwa kusambaza matangazo ya kuchapa kwa njia ya posta na ana kwa ana, eneo fulani linaweza kulengwa ambalo ndiyo lina wateja walengwa zaidi. Kuweza kuwalenga wateja wa aina fulani huwa inaongeza ufanisi na kupunguza gharama za matangazo ukilinganisha na yale ambayo yanawafikia watu wote, hata ambao siyo wateja walengwa.

Pamoja na kutumia njia za kidijitali kuwafikia wateja wengi, matangazo ya kuchapa bado ni njia yenye nguvu na inayopaswa kutumika vizuri ili kuwafikia watu wengi kwa uhakika na kuwa na ushawishi mkubwa kwao.

Tufanyie kazi njia hii ya matangazo ya kulipia kwa namna ambayo ina manufaa kwenye biashara na kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi na kuwashawishi kununua ili kukuza mauzo ya biashara.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.