3409; Fikra, Hisia na Matendo.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Hatuwezi kudhibiti matokeo tunayoyapata, lakini tunaweza kudhibiti hatua tunazochukua.
Hivyo basi, wajibu wetu namba moja ni kuchukua hatua sahihi mara zote, hata kama hatupati matokeo tuliyotarajia.
Tunachokuwa na uhakika nacho ni kwa kurudia rudia kufanya, kwa ukubwa na ubora, tunajiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata matokeo tunayoyataka.
Licha ya hatua tunazochukua kuwa ndani ya udhibiti wetu, bado siyo rahisi kufanya kile tunachopaswa kufanya.
Mara nyingi huwa tunajua kabisa nini tunapaswa kufanya.
Na tunajua jinsi ya kufanya.
Lakini bado hatufanyi.
Kikubwa hapo kinakuwa ni hisia tunazokuwa nazo.
Kama mtu utakuwa na hisia hasi juu ya kitu, hupati msukumo wa kukifanya.
Lakini ukiwa na hisia chanya, utaweza kufanya bila hata ya kusukumwa.
Kwa kuwa hisia ndiyo zinazoathiri hatua ambazo mtu anachukua, tunapaswa kuziathiri na zenyewe pia.
Lakini hapo tunagundua kwamba hatuna udhibiti wa moja kwa moja wa hisia zetu.
Tunapoziangalia hisia, tunagundua kwamba zinachochewa na fikra ambazo mtu unakuwa nazo.
Na uzuri ni fikra zipo ndani ya uwezo wetu wa kudhibiti.
Tunaweza kufikiri juu ya chochote tunachotaka.
Kwa mtiririko huu, tunapata kanuni rahisi ambayo tukiifanyia kazi, matokeo yanakuwa mazuri.
Kanuni hiyo inakwenda;
Dhibiti fikra zako na utakuwa umedhibiti hisia zako.
Dhibiti hisia zako na utakuwa umedhibiti hatua unazochukua.
Dhibiti hatua unazochukua na utakuwa umedhibiti matokeo unayopata.
Kanuni ndiyo hiyo;
Fikra zinachochea hisia na hisia ndiyo zinasukuma hatua unazochukua huku hatua hizo zikiamua ni matokeo gani yapatikane.
Wewe ndiye mwenye ufunguo wa akili yako, hivyo hakikisha kila fikra unayokuwa nayo, unaidhibiti wewe mwenyewe.
Watu wasioelewa hiyo kanuni na mtiririko wako, watahangaika sana kuiga yale unayofanya. Lakini bado hawataweza kupata matokeo bora kama unayopata wewe.
Kupata ushindi mkubwa na wa uhakika kwenye chochote unachofanya, kuwa ‘bize’ na kudhibiti fikra zako, ili hisia na matendo viwe sawa na upate matokeo mazuri.
Ukiweza kudhibiti fikra zako muda wote, hisia na vitendo vitakuwa sawa na matokeo yataweza hata kutabirika kwa uhakika.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana.
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe