Rafiki yangu mpendwa,
Madeni yamekuwa kaburi ambalo limezika ndoto za watu wengi kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao.
Hiyo ni kwa sababu madeni hayo huwa yanakuwa na gharama kubwa sana kwa watu, ambazo zimekuwa hazionekani waziwazi.
Gharama kubwa ya madeni ipo kwenye riba inayotozwa na tozo nyingine zinazoambatana na madeni hayo, kama pale mtu anaposhindwa kulipa.
Mwandishi Ramit Sethi kwenye kitabu chake cha I WILL TEACH YOU TO BE RICH ametushirikisha hatua tano za kuondoka kwenye madeni. Kwa kuzifanyia kazi hatua hizo kwa uhakika, kila mtu anaweza kuondoka kwenye madeni na akajenga utajiri mkubwa.

Karibu tujifunze kutoka kwenye kitabu hicho.
SURA YA 1; ONDOKA KWENYE MADENI.
Kuna madeni ya aina tatu ambayo watu wengi ndiyo wapo;
1. Madeni ya kadi za mikopo.
Haya ni madeni ambayo watu wanakuwa nayo kwenye kadi za manunuzi za mikopo (credit cards). Madeni haya huwa yana gharama kubwa pale mtu anaposhindwa kulipa kwa wakati.
2. Madeni ya mikopo ya fedha.
Haya ni madeni ambayo mtu unakuwa umekopa fedha au mali na kuhitajika kulipa. Kwa wengi madeni haya huwa ni makubwa na yanayolipwa kwa muda mrefu. Kadiri deni linavyolipwa kwa muda mrefu, ndivyo riba yake inakuwa kubwa na kumgharimu sana mtu.
3. Madeni ya mikopo ya elimu ya juu.
Haya ni madeni ambayo waliosoma elimu ya juu kwa mikopo wanakuwa wanadaiwa. Madeni haya huwa ni makubwa, yenye riba ndogo na yanayolipwa kwa muda mrefu. Kutokana na riba yake ndogo, madeni haya yanaweza yasiwe na gharama kubwa sana kwa mtu.
Hatua 5 za kuondoka kwenye madeni.
1. Jua jumla ya madeni unayodaiwa.
Ni jambo la kushangaza, lakini watu wengi walio kwenye madeni hawajui hata ni kiasi gani wanachodaiwa. Hatua ya kwanza ni wewe kujua jumla ya madeni yote unayodaiwa.
2. Chagua madeni utakayoanza kulipa.
Hapa kuna kambi mbili, moja inasema lipa madeni yenye riba kubwa kwanza huku nyingine ikisema lipa madeni madogo kwanza. Kulipa yenye riba kubwa ni kupunguza gharama. Kulipa madogo ni kupata ushindi pale unapojua umemaliza kulipa deni. Chagua itakayokufaa, muhimu ni ulipe.
3. Omba punguzo la riba, hasa unapolipa zaidi.
Kwa wale wanaokudai, kutana nao na waombe wakupunguzie riba, kwa kuahidi kulipa kwa kiasi kikubwa na kwa wakati. Wanaokudai wanataka sana uwalipe, hivyo kama ukionyesha uaminifu, watakuwa tayari kukupunguzia riba.
4. Jua pesa ya kulipa madeni utaitoa wapi.
Kuwa na mpango wa kulipa madeni hautafanya kazi kama hujapanga wapi unatoa pesa za kulipa madeni. Hatua ya kwanza ni kuangalia matumizi ambayo utayapunguza na pesa yake kupeleka kulipa madeni. Hatua ya pili ni kuongeza kipato chako ili uweze kulipa madeni. Fanyia kazi hatua zote mbili.
5. Anza kutekeleza mpango wako mara moja.
Wengi wanapanga sana kutoka kwenye madeni, ila hawafanyii kazi mipango yao na hivyo kubaki pale walipo. Wewe usiwe hivyo, ukishaweka mpango, anza kuufanyia kazi mara moja.
SOMA; Jifunze Kujenga Utajiri, Hatua Sita (06) Za Uhakika.
SURA YA 2; FUNGUA AKAUNTI SAHIHI ZA BENKI.
Kuna aina tatu za akaunti za benki ambazo kila anayesimamia vizuri fedha zake ili kujenga utajiri na uhuru wa kifedha anapaswa kuzijua na kuwa nazo.
1. Akaunti ya malipo.
Hii ni akaunti ambayo fedha zako zote zinapita. Kila fedha unayolipwa kwa benki inapita kwenye akaunti yako. Na ni kwenye akaunti hiyo ndiyo unasambaza fedha hizo kulingana na matumizi na mipango yako mingine.
Hakikisha unakuwa na akaunti hii kwenye benki ambayo ina sifa ya uaminifu na ina riba ndogo au hakuna riba kabisa. Epuka kosa la kufanya akaunti hii ya malipo kuwa ndiyo ya akiba, kwani utaishia kutumia na usiwe na akiba.
2. Akaunti ya akiba.
Hii ni akaunti ya kuweka akiba kwa malengo mbalimbali unayokuwa nayo. Akaunti hiyo unaweza kuweka fedha, ila kutoa huwa siyo rahisi. Hilo linakusaidia usigeuze fedha za akiba kuwa fedha za matumizi.
Benki zina akaunti za aina hii ambazo unapaswa kuwa nazo ili kutimiza malengo yako yanayohitaji fedha. Mfano kuanzisha biashara, kujenga nyumba, kununua gari n.k.
3. Akaunti ya uwekezaji.
Hii ni akaunti ambayo unaweka fedha unazotenga kwa ajili ya uwekezaji. Akaunti hiyo ni muhimu kwa sababu uwekezaji ndiyo njia ya kujenga utajiri mkubwa.
Katika kuchagua benki ya kufungua akaunti zako, angalia sifa hizi; Uaminifu, Urahisi na Bidhaa zilizopo. Kubwa zaidi angalia benki isiwe na gharama za kuendesha akaunti au makato kwenye kufanya miamala mbalimbali.
Masomo yote ya kujenga utajiri kutoka kitabu kinachoitwa I WILL TEACH YOU TO BE RICH kilichoandikwa na Ramit Seth yanapatikana kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.
Hapo chini ni kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu somo hili. Fungua ujifunze kwa kina na kupata shuhuda za wengine.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.