3411; Vitu visivyowezekana.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Jinsi tunavyotumia dhana ya kutokuwezekana siyo sahihi na imekuwa inatukwamisha.
Tunaangalia yale ambayo tunayataka na tunapokutana na vikwazo, tunaona haiwezekani kupata yale tunayotaka.
Kitu ambacho siyo kweli kabisa.
Vitu visivyowezekana kwa uhalisia ni kinyume kabisa na yale ambayo sisi tunaona hayawezekani.
Wakati unaona haiwezekani kufanikiwa, ukweli ni kwamba hauwezi kutokufanikiwa kabisa.
Kwa jinsi mafanikio yalivyo, haiwezekani kabisa wewe ukashindwa kabisa kufanikiwa.
Haiwezekani wewe kumaliza kabisa juhudi zako ambazo unaweza kuziweka kwenye kitu.
Juhudi ni kitu ambacho huwa hakiishi, zinaendelea kuwepo kwako milele.
Hivyo kila wakati unaweza kuendelea kuweka juhudi.
Na kama utaweka juhudi bila kukwama, lazima utaweza kufanya makubwa.
Haiwezekani wewe kumaliza kutumia uwezo wako wote ulio ndani yako.
Unao uwezo mkubwa sana ndani yako kiasi kwamba huwezi kumaliza kuutumia wote.
Haijalishi ni makubwa kiasi gani umeshafanya, bado unaweza kufanya makubwa zaidi ya hayo.
Uwezo wako ni kitu ambacho hakina ukomo na wakati wowote unaweza kutumia zaidi na zaidi.
Haiwezekani kumaliza nafasi zako za kujaribu.
Pale unapofanya kitu na ukashindwa, siyo mwisho wa wewe kufanya.
Hakuna mahali utaambiwa wewe umeshajaribu sana na umemaliza nafasi zako za kujaribu.
Una nafasi zisizo na ukomo za kuendelea kujaribu yale unayofanya ili upate kile unachotaka.
Mara zote huwa kuna siku nyingine, nafasi nyingine na watu wengine.
Kamwe huwezi kumaliza kabisa.
Haiwezekani kumaliza uvumilivu na ung’ang’anizi ulionao.
Bado unaweza kuendelea kuwa na uvumilivu na ung’ang’anizi kwenye mambo yote unayofanya.
Hilo lipo ndani ya udhibiti wako kabisa.
Haijalishi unapitia nini, bado unaweza kuendelea kuwa na uvumilivu na ung’ang’anizi zaidi na zaidi.
Na hayo yatakuweka wewe kwenye nafasi nzuri ya kuweza kufanya makubwa baadaye.
Kama hakuna okomo kabis kwenye safari yako ya mafanikio, kwa nini usijitoa mazima ili kufanikiwa.
Kwa nini usifumbe mdomo na kuziba masikio ili uweke juhudi kubwa kwenye kile ulichochagua kufanikiwa?
Kama mengi ambayo umekuwa unaona yana ukomo hayana, ni nini kinachoweza kukuzuia kufanikiwa?
Jibu unalijua, ni wewe mwenyewe ndiye unayejikwamisha kufanikiwa.
Kama ukiondoa huko kujizuia kufanikiwa ambapo umekuwa nako, hakuna chochote kinachoweza kukuzuia.
Mafanikio kwako linakuwa ni swala la muda tu, kama utayaendea kwa mtazamo wa hakuna kisichowezekana.
Endelea kuweka juhudi bila ya kufikiria kutokuwezekana na utaweza kufanya makubwa sana.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe