Habari njema Matajiri Wawekezaji,
Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU, tumechagua uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja kama njia kuu tunayofanyia kazi.
Hiyo ni kwa sababu kazi yetu kuu siyo uwekezaji, bali tuna shughuli zetu nyingine, ajira na biashara.
Tunachotaka ni umakini wetu tuuweke kwenye kutoa thamani kubwa kwenye shughuli tunazofanya, kisha kipato tunachoingiza tukiwekeze na kutuzalishia zaidi baadaye.
Aina nyingine za uwekezaji zinahitaji mtu kutumia muda mwingi kuelewa uwekezaji kwa kina na hata kupangilia na kufuatilia ili kupata faida.
Lakini uwekezaji wa mifuko ya pamoja, huhitaji kuwa na uelewa wowote mkubwa. Hiyo ni kwa sababu mifuko hiyo inakuwa na wataalamu wanaofanya yote hayo, kuchagua uwekezaji sahihi na kufuatilia ili kupata faida.
Hilo linatupa sisi fursa ya kuendelea na majukumu yetu mengine, huku uwekezaji wetu ukikua na kutunufaisha.

Kwa hapa Tanzania, mifuko ya pamoja inayofanya vizuri na ambayo ni rahisi kila mtu kuwekeza ni ya UTT AMIS.
Na hiyo ndiyo tumechagua kwenda nayo kwa sababu ya urahisi wake, kuanzia kujiandikisha kama mwekezaji, kuwekeza, kufuatilia uwekezaji na hata kuuza uwekezaji.
Unaweza kukamilisha hayo yote ukiwa mahali popote bila ya kulazimika kwenda kwenye ofisi zao. Na hayo ni muhimu sana kwenye uwekezaji, kwa sababu kukishakuwa na ugumu wowote kwenye mchakato, inaathiri sana msimamo wa uwekezaji.
UTT AMIS wana mifuko mingi, kuchagua mifuko sahihi kwa kila kipindi cha maisha bado ni changamoto kwa wengi. Kwenye somo la nyuma tulijifunza kuchagua mifuko ya uwekezaji kutokana na mahitaji mbalimbali ya mtu.
Lakini bado kigezo cha mahitaji pekee kinaweza kisitoshe kupangilia uwekezaji wa mtu. Maana mahitaji yanabadilika kadiri mtu anavyokwenda.
Kwenye somo hili tunakwenda kuangalia kigezo kingine cha kupangilia mifuko ya uwekezaji ambacho ni umri. Tutaona mifuko ya kuwa nayo kwenye kila umri ili kunufaika zaidi na uwekezaji unaokuwa unafanya.
SOMA; Mpangilio Sahihi Wa Mifuko Ya Uwekezaji Ya UTT AMIS Ili Kufikia Uhuru Wa Kifedha.
Kabla ya kuendelea, tujikumbushe kwamba UTT AMIS wana mifuko sita ya uwekezaji ambayo inatofautiana kwenye malengo na utaratibu wa uwekezaji. Mifuko hiyo ni UMOJA, WATOTO, WEKEZA MAISHA, JIKIMU, UKWASI na HATIFUNGANI.
Kwa kuzingatia kigezo cha umri, tutagawa kwenye vipindi vinne vya maisha;
KIPINDI CHA KWANZA; UTOTO (MIAKA 1 MPAKA 20)
Hiki ni kipindi ambacho mtu anakuwa tegemezi kwa wazazi, kwa sababu anakuwa hajawa na shughuli za kuingiza kipato.
Mfuko wa kuwa nao ni wa WATOTO, ambao atakuwa anachangiwa na wazazi wake.
Sababu za mfuko huo ni kumjengea tabia ya uwekezaji, kumsaidia kwenye masomo na maandalizi mengine ya baadaye.
KIPINDI CHA PILI; UJANA (MIAKA 21 MPAKA 40)
Hiki ni kipindi ambacho mtu anaanza maisha ya kujitegemea na kuanza kujenga familia. Katika kipindi hiki mtu anakuwa anajitafuta na kuanza kujipata.
Kipindi hiki wasiokuwa na uelewa huwa wanakipoteza sana na kuchelewa kuanza uwekezaji, kitu wanachokuja kujutia baadaye.
Mifuko ya kuwa nao kwenye kipindi hiki ni UMOJA, UKWASI na WATOTO (kama mtu anao).
Mfuko wa UMOJA ni kwa ajili ya uwekezaji endelevu ambao hakuna kutoa kwa kipindi chote ambacho mtu anafanya shughuli za kuingiza kipato. Ni mfuko wa kuwekeza na kusahau. Hapa angalau asilimia 10 ya kipato cha mtu inaingia huko kwa kipindi chote ambacho anafanya shughuli za kuingiza kipato. Na akishawekeza, hapaswi kutoa uwekezaji huo kwa sababu zozote.
Mfuko wa UKWASI ni kwa ajili ya malengo mbalimbali ambayo mtu anakuwa nayo na anayakusanyia fedha kwa kipindi fulani. Kama una lengo ambalo itakuchukua zaidi ya mwaka kukusanya fedha yake, badala ya kuweka benki ambapo riba ni ndogo na makato ni makubwa, weka kwenye mfuko wa UKWASI ambapo riba itakuwa kubwa na unapotaka fedha hizo unazipata kwa haraka. Katika kipindi hicho cha maisha ndiyo mtu anakuwa na malengo ya kuanzisha biashara, kujenga nyumba na kufanya manunuzi mengine makubwa kama gari na mali nyingine. Hivyo kuwa na mfuko wa UKWASI kwenye hiki kipindi ni muhimu.
Mfuko wa WATOTO ni kwa wale wenye watoto, ambapo kipindi hicho ndiyo wengi wanaanzisha familia. Hivyo ni muhimu kuwaanzishia watoto uwekezaji kulingana na manufaa ambayo tumeshayaona kwenye mfuko huo wa watoto.
KIPINDI CHA TATU; MAKAMO (MIAKA 41 MPAKA 60)
Hiki ni kipindi ambacho maisha ya mtu yanachanganya, majukumu ni mengi na makubwa. Lakini pia ni kipindi cha ukuaji mkubwa kwa wale ambao wameshajipata kwenye yale waliyochagua kufanya. Kwa wale waliochelewa kujipata, ndiyo huwa wanakuja kufunguka kwenye hiki kipindi. Kumbuka kauli maarufu na ya wazembe kwama LIFE BEGINS AT 40, ambayo ni ya kujifariji kwa wale waliopoteza vipindi vya nyuma. Wengi wanaopoteza vipindi vya nyuma, hujiona kama wamechelewa, lakini siyo, bado wana muda wa kutosha.
Kwenye kipindi hiki utaendeleza mifuko ya kipindi cha pili, yaani UMOJA, UKWASI na WATOTO. Baadaye utaongeza mfuko wa WEKEZA MAISHA.
Sababu za mifuko ya UMOJA, UKWASI na WATOTO ni kama kwenye kipindi cha pili cha maisha.
Kwenye miaka 50, mtu anapaswa kuanzisha mfuko wa WEKEZA MAISHA. Huu ni mfuko ambao pia una bima ya maisha na bima nyingine binafsi. Huu ni wakati mzuri wa kuwa na bima hiyo kwa sababu umri unakuwa umeshaenda kiasi, huku pia ukiwa na wategemezi. Hivyo chochote kinachokutokea, mfuko huu utatoa fidia kwako na/au wategemezi wako.
Japo mfuko wa WEKEZA MAISHA unaweza kuwa nao kwenye umri wowote kati ya miaka 18 mpaka 55, kuwa nao kwenye umri wa chini ya miaka 50 siyo mpango mzuri sana. Hiyo ni kwa sababu hatari siyo kubwa kwenye umri huo na ukiwekeza fedha zako kwa mpango mwingine wenye matokeo mazuri zaidi, itakuwa na manufaa.
Kipindi cha tatu cha maisha siyo cha kubahatisha, bali ni cha kujenga misingi imara ili kipindi cha nne kiwe na utulivu. Ni muhimu sana mtu upambane kujenga hali ya kustaafu kwenye kipindi hiki, yaani usilazimike kufanya kazi kwenye kipindi cha nne.
KIPINDI CHA NNE; UZEE (MIAKA 61 NA KUENDELEA)
Hiki ni kipindi ambacho uzee unaanza, japo mtu anakuwa na nguvu za kuweza kuendelea kuendesha maisha yake vile anavyotaka mwenyewe. Ni kipindi ambacho nguvu za mtu zinakuwa zimepungua kwa kiasi fulani, hawezi ile mikiki mikiki ya vipindi vya nyuma. Japo siyo kipindi cha kubweteka, lakini kinakuwa kizuri kama mtu alikuwa na maandalizi.
Kwenye kipindi hiki mtu anapaswa kuwa na uwekezaji kwenye mifuko miwili ya UTT, ambayo ni JIKIMU na HATIFUNGANI. Faida za mifuko hiyo ni kumpa mtu kipato cha kuweza kuendesha maisha yake bila ya kulazimika kufanya kazi moja kwa moja au kuuza uwekezaji wake. Mfuko mmoja kati ya hiyo miwili inatosha, wa HATIFUNGANI ukiwa bora zaidi kwa sababu ya kuweza kuingiza pato la kila mwezi.
Ili kuongeza kipato ambacho mtu anakuwa anapata kutokana na uwekezaji wake, mwekezaji anaweza kuhamisha uwekezaji kutoka mifuko mingine na kupeleka kwenye mfuko wa JIKIMU au HATIFUNGANI. Isipokuwa kwa mfuko wa WEKEZA MAISHA ambapo mtu atasubiri mpaka kipindi cha miaka 10 ya mfuko huo kiishe na kupata uwekezaji wake, ambao atapeleka kwenye mfuko aliochagua wa uzeeni.
Kwa kuwa umri unakuwa umeenda na kwa kuwa pia mtu anaweza kuishi mpaka hata miaka 100, maandalizi makubwa ya vipindi vya awali yanahitajika. Mtu kufanya uwekezaji ambao ili aweze kunufaika nao ni mpaka auuze ni kikwazo kwa maisha yanayokuwa yanaendelea, kwani akishauza uwekezaji, hawezi kunufaika nao tena.
Kwa kuwa na mfuko wa HATIFUNGANI, ambao unakupa gawio la kila mwezi, huku uwekezaji wako wa msingi ukiendelea kuwepo, unakuwa umejitengenezea mshahara wa maisha yako yote, huku ukiwa hulazimiki kufanya kazi moja kwa moja.
VIPI KAMA UMECHELEWA KWENYE KIPINDI HUSIKA?
Huenda unajiona umechelewa kwenye kipindi husika ambacho upo sasa. Lakini uzuri ni kwenye mambo ya fedha na uwekezaji, hata kama unaona umechelewa, unapaswa kuanza mara moja. Maana kibaya kabisa ni kutokufanya.
Kama unaona umechelewa, anza, lakini fanya kwa ukubwa kuliko wengine. Kwa mfano kama waliowahi walifanya uwekezaji wa asilimia 10 ya kipato na wakanufaika, wewe utapaswa kwenda zaidi ya hapo. Utalazimika kwenda mpaka hata asilimia 40, ili kuokoa kipindi ambacho umekipoteza.
Muhimu sana ni kupambana kuhakikisha unaendelea kuingiza kipato mpaka pale unapokuwa na uwekezaji ambao gawio la kila mwezi linatosha kuendesha maisha yako bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Kama hujafikia hapo, endelea kupambana na kuingiza kipato bila ya kujali upo kwenye umri gani.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili, kuthibitisha kwamba umesoma somo, umeelewa na unakwenda kufanyia kazi. Shiriki mjadala kwa kujibu maswali yafuatayo;
1. Kwa nini kwenye programu ya NGUVU YA BUKU tumechagua uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja na siyo uwekezaji mwingine? Kwa nini tumechagua mifuko ya pamoja ya UTT AMIS?
2. Kwa sasa upo kwenye kipindi kipi cha maisha? Na je uwekezaji unaofanya sasa unaendana na kipindi hicho? Maboresho gani unapaswa kufanya kwenye mpango wako wa uwekezaji?
3. Ili uweze kufikia hali ya kustaafu, yaani kuweza kuingiza kipato cha kutosha kuendesha maisha kupitia uwekezaji wako, unapaswa kuwa na uwekezaji kiasi gani kwenye mfuko wa HATIFUNGANI? (Kanuni rahisi, chukua kiasi unachohitaji kwa mwezi, kisha zidisha mara 100).
4. Shirikisha mkakati wako wa kufikia kiasi hicho unachopaswa kuwa nacho kwenye mfuko wa HATIFUNGANI kwa miaka 10 ijayo.
5. Karibu uulize swali lolote ulilonalo kwenye somo hili au programu nzima ya NGUVU YA BUKU.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kujifunza na kwenda kufanyia kazi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.