
Kiasili binadamu ni wavivu kufanya maamuzi, hasa yanayohusiana kutoa pesa. Ndiyo maana, tabia ya kughairisha mambo imeendelea kuwepo miongoni mwetu.
Unakumbuka 2019, serikali walipotangaza kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura. Kukawa na muda mrefu wa kujiandikisha.
Hukujisumbua kutumia siku za awali kukamilisha zoezi hilo, kwa sababu uliona bado siku zipo. Lakini ilipokaribia kufika siku za mwisho za zoezi, ulisukumwa kulikamilisha, maana hakukuwa na nafasi nyingine.
Uliacha mengine yote na hata kukaa kwenye foleni ndefu ili tu kukamilisha zoezi.
Kilichofanya uache mambo mengine, na kukamilisha zoezi hilo ni hofu ya kupoteza haki yako kama mtanzania wakati wa kupiga kura.
Linapokuja suala la mauzo, wateja hawafanyi maamuzi sio kwa sababu ni wagumu, bali hatujaweza kuwapa sababu ya kuwafanya wachukue hatua. Hii ni kwa sababu;
Moja; Hatujaelewa ni kwa kiasi gani wana haraka na huduma yetu.
Mbili; Hatujaweka ofa zetu katika hali ya kumfanya aseme ndiyo.
Tatu; Hatujajua nafasi ya mteja katika kufanya maamuzi.
Ndiyo maana, haya mambo matatu ni kuyazingatia wakati wa mazungumzo na mteja ili kumsaidia kufanya maamuzi;
Moja; Elewa matarajio yake.
Hii itakusaidia kumpatia pendekezo lililo sahihi. Utajua kama uwezo wa kukamilisha upo au la.
Mbili; Elewa biashara yako vema
Hii itakusaidia kujibu mapingamizi ya mteja na kumpatia hatua zinazofuata.
Tatu; Uliza, ni kwa namna gani wanafanya maamuzi. Hili ni swali la mtego, wakati mwingine unaweza kuwa unazungumza na mtu mwingine na mfanya maamuzi ni mwingine.
Mambo yanayokwamisha wateja kuchukua hatua au kufanya maamuzi;
Moja; Kukosa uaminifu.
Hawajaweza kuwa na imani kuu ya biashara yako.
Mbili; Wasi wasi wa kupoteza pesa.
Ndiyo maana tunasema, watu hawapendi kutoa pesa yao kulipia kitu. Hii ni kwa sababu wakiitoa pesa hiyo hawataweza kuituma tena katika mambo mengine.
Tatu; Kukosa vichocheo kama tamaa, uhakika, haraka au ofa.
Kwahiyo, mteja anayeonyesha hali za namna hiyo usimlazimishe kufanya maamuzi. Bali msaidie kuamua.
Mweleze juu ya matokeo anayoenda kupata hii itamjengea hali mbili. Moja hofu ya kupoteza na tamaa ya kupata mwishowe atafanya maamuzi.
Hatua za kuchukua leo; Andaa mkakati wako unaoenda kuwafanya wateja kufanya maamuzi.
Ikiwa huna njia ya kuwasukuma watu kufanya maamuzi, utaongea na wateja wengi, watakuelewa na wote watakwambia, “nikiwa tayari nitakutafuta”. Ndiyo utalavyozidi kuwapoteza wateja wengi.
Je, ni wateja wangapi wanaokutafuta au kurudi baada ya kukupa kisogo?
Wako wa daima
Lackius Robert
Mkufunzi Msaidizi CHUO CHA MAUZO
0767702659 |mkufunzi@mauzo.tz
Karibu tujifunze zaidi