3412; Uchovu na njaa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Unapokuwa unaanzia chini kabisa, yaani huna chochote, juhudi zako binafsi ndiyo zinakutoa.
Unapokuwa chini, kuna mambo mengi binafsi yanayokuwa yamekukwamisha, ambayo ukiweza kuyavuka, unapiga hatua kubwa.
Baana ya kupiga hatua kiasi peke yako na kuweza kutoka chini kabisa, kupiga hatua kubwa zaidi ya hizo, juhudi zako binafsi hazitoshi.
Katika ngazi hiyo, ukuaji unategemea zaidi timu kuliko juhudi zako binafsi au za mtu mmoja.
Kwenye maisha na mafanikio, timu ya watu unaoshirikiana nao ni muhimu kuliko kitu kingine chochote.
Hivyo wajibu wako mkubwa ni kutengeneza timu sahih na bora, ambayo itaweza kuvuka vikwazo mbalimbali vilivyopo kwenye safari.
Kuna sifa na vigezo vingi ambavyo unaweza kuangalia kwenye kuchagua watu wa kuwaweka kwenye timu yako.
Lakini kigezo kikuu unachopaswa kutumia, hasa pale unapokuwa unahitaji ukuaji mkubwa ni uchapakazi.
Unataka watu ambao wanapenda na wapo tayari kuweka juhudi kubwa sana.
Watu ambao wanalala wakiwa wamechoka na kuamka wakiwa na njaa kali.
Ni njaa hiyo kali wanayokuwa nayo muda wote ndiyo inawasukuma kujituma sana.
Wakati uchapa kazi ukiwa kama tiketi ya kuchuja walio sahihi na wasio sahihi, kuna vigezo vingine zaidi vya kuzingatia katika kuruhusu watu utakaoshirikiana nao kwenye safari yako.
Unahitaji watu ambao wanafanya kwa ubora wa hali ya juu sana, ni waaminifu kwa matendo yao na wengi ari kubwa ya kuwasukuma kufanya kilicho.
Ubora unajieleza, unataka watu ambao wamejiwekea viwango vya juu sana na mara zote wanapambana kufikia viwango hivyo walivyojiwekea.
Uaminifu ni muhimu, maana unaposhirikiana na mtu ambaye anajiangalia mwenyewe na kutojali kuhusu wengine, hata kama watakupa matokeo, wataharibu sana utamaduni unaokazana kuujenga.
Ari ndiyo kitu ambacho unapaswa kukiona kabisa na kikushawishi kwamba mtu ataweza kufanya makubwa ndani ya mfumo ambao umeshaujenga.
Unahitaji watu ambao kila siku ya kazi kwao ni siku mpya kabisa.
Wanaiona ni siku mpya ya kudhihirisha kwamba wanastahili kuendelea kuwepo.
Hawaridhiki na matokeo yoyote ya jana, maana wanajua matokeo hayo ya jana hayatakuwa na maana kama matokeo ya leo siyo mazuri.
Pata watu hao ambao wanapambana kuonyesha wanaweza kufanya kwa ukubwa zaidi ya ilivyozoeleka na utaweza kufanya makubwa zaidi na zaidi.
Juhudi za mtu mmoja ni rahisi kuzishinda, lakini juhudi za timu yenye msukumo mkubwa, ni ngumu sana kuzishinda.
Hasa pale timu inapokuwa na ushirikiano mkubwa na njaa kuwa kubwa zaidi.
Ukishaanzia chini na kuweza kudhihirisha kwa juhudi zako binafsi kwamba unaweza kubadili hali, kinachofuata ni kujenga timu yenye uwezo wa kufanya makubwa sana na kwenda nayo.
Huhitaji timu ya watu ambao wanasubiri kwa hamu muda wa kazi uishe ili wakaendelee na mambo yao na wanaochelewa hata kwenye muda wa kuanza.
Unawataka wale ambao kinawafanya wakamilishe siku ya kazi ni uchovu hasa wanaokua nao kiasi kwamba hawawezi kuendelea kufanya.
Lakini pia wanapoenda kupumzika, baada ya mapumziko wanarudi wakiwa na niaa kubwa zaidi, ambayo inawasukuma zaidi.
Njaa hiyo ndiyo inawafanya wawahi kuanza majukumu yao kuliko wengine wote.
Jenga timu sahihi na imara na hakuna kitakachokuzuia usifanye makubwa unayoyataka.
Vigezo unavyotumia kuchukua watu kwenye timu, ndiyo hivyo hivyo unapaswa kutumia kuwaondoa kwenye timu wale wasiofaa kuendelea.
Yeyote ambaye hafikii vigezo vya ubora, uaminifu na ari, hapaswi kupata nafasi.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe