Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Mafanikio kwenye mauzo, kama ilivyo kwenye kila eneo la maisha yetu, huwa siyo kitu rahisi. Safari ya mafanikio huwa ina vikwazo na changamoto za kila aina.

Na sehemu kubwa ya vikwazo na changamoto hizo inatokana na kulazimika kufanya vitu ambavyo hatujazoea kufanya. Kufanya vitu vipya ambavyo hatujazoea, huwa inatuweka kwenye hali ya hofu.

Tunapata hofu pale tunapohitajika kufanya vitu vipya, kwa sababu tunakuwa hatuna uhakika wa matokeo tunayokwenda kupata. Tunapenda kufanya vitu tulivyozoea kufanya kwa sababu ya uhakika wa matokeo. Tunapohitajika kufanya vitu vya tofauti, ambavyo hatuna uhakika wa matokeo, tunapatwa na hofu.

Hofu ya kutokuwa na uhakika imekuwa ndiyo kikwazo kikubwa kwa watu wengi kufanikiwa. Na kwenye mauzo, hofu hiyo imewazuia wengi kuwa wauzaji bora na kuweza kufanya makubwa.

Isingekuwa hofu ya kufanya vitu vipya, watu wengi sana wangekuwa wamefanya makubwa. Lakini wengi wamekwamishwa na hofu hiyo.

Tukiweza kupata dawa ya hiyo hofu, tutaweza kufanya makubwa sana.

Na kwa bahati nzuri sana, dawa hiyo ipo, ambayo ni kufanya.

Yaani dawa ya HOFU ni kufanya kile unachohofia kufanya.

Hofu inakuwa na nguvu pale mtu unapoacha kufanya, kwa sababu unakuwa hujui ni matokeo gani ungepata na yangekuwa kikwazo kwako kiasi gani. Unaposhindwa kufanya, hofu inapata nguvu zaidi ya kukuzuia.

Lakini pale unapofanya yale unayohofia, hofu inakosa nguvu. Hiyo ni kwa sababu matokeo unayoyapata, huwa ni tofauti na ulivyokuwa unahofia. Hata kama utakuwa umeshindwa, utagundua kushindwa huko hakuumizi kama ulivyokuwa unategemea.

Kwa kufanya mara moja, utaweza kufanya tena mara nyingine na nyingine. Na kadiri unavyofanya, ndiyo unajisogeza karibu zaidi na kupata matokeo mazuri unayoyataka.

Ili kufanikiwa kwenye mauzo na kwenye maeneo mengine ya maisha yako, ongozwa na hofu. Yaani pale unapohofia kufanya kitu, hapo hapo jiambie ndiyo utakifanya.

Kwa kutumia mwongozo huo rahisi, utajikuta unafanya mengi na kujisogeza karibu zaidi na matokeo unayoyataka. Kwa kufanya unayohofia, unavuka kile ambacho kinawakwamisha wengi na hivyo kuwa mbele ya wengine.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuitumia Hofu Inayokuzuia Kufanikiwa Kupata Mafanikio Makubwa Zaidi.

HOFU ZA KUVUKA KWENYE MAUZO.

Kwenye mauzo, kuna vitu vingi ambavyo huwa vinawapa wauzaji hofu, ambavyo ukiweza kuvivuka utaweza kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

1. Kusaka Wateja Wapya.

Kusaka wateja wapya, kwa njia yoyote ile huwa ni kitu ambacho wengi huwa wanahofia. Wanachohofia ni kukataliwa na watu hao kwa sababu hawawajui.

Wewe unapaswa kusaka wateja wapya mara zote, kwa sababu hata ukikataliwa, hakuna unachokuwa umepoteza. Na pale unaposaka bila kuacha, unapata wateja wapya wengi.

2. Kukamilisha Mauzo.

Kwenye mchakato mzima wa mauzo, mtu anaweza kuongea na mteja vizuri kabisa na kwa ushawishi. Lakini inapofika wakati wa kumwambia mteja afanye malipo ili kupata kile ambacho anauziwa, wengi huingiwa na hofu. Hivyo mazungumzo mengi ya mauzo yamekuwa yanaishia njiani, kwa sababu tu wauzaji wanahofia kuwaambia wateja walipie ili kupata kile wanachowauzia.

Wewe kuwa mkamilishaji, ukianza mapema kabisa kwenye hatua za mchakato wa mauzo. Mara kwa mara mwambie mteja alipie ili kupata kile unachomuuzia. Usihofie atakuambia hana fedha au hajawa tayari, wewe mwambie na kwa msisitizo, wengi watafanya hivyo.

3. Kufanya Mauzo Ya Ziada.

Baada ya mteja kufanya manunuzi makuu ambayo ndiyo alikuwa anataka, huwa kuna fursa ya kumshawishi anunue zaidi ya alivyokuwa amepanga. Kinachohitajika ni muuzaji kumwambia mteja anunue zaidi. Lakini wauzaji wengi huwa wanahofia kuwaambia wateja wanunue zaidi, kwa sababu wadhani wataonekana wana tamaa au wanajiambia mteja hana tena fedha. Kwa hofu hiyo wanajinyima mauzo ya ziada ambayo wangeweza kuyapata.

Wewe panga kufanya mauzo ya ziada kila baada ya kukamilisha mauzo makuu. Andaa kabila nini cha ziada utakachomuuzia mtu baada ya kuwa amekamilisha mauzo makuu. Na haijalishi unajishawishi kiasi gani kwamba hatakubali mauzo ya ziada, wewe mwambie. Wajibu wako ni kumwambia mteja afanye manunuzi ya ziada, halafu yeye ndiyo atakujibu kama anafanya au la. Hata kama atasema hapana, hakuna unachokuwa umepoteza, maana mauzo makuu umeshayapata.

4. Kuomba Rufaa.

Wateja ambao wameshanunua kwenye biashara huwa ni chanzo kizuri cha kupata wateja wengine. Kwa sababu hao wanakuwa ni mashuhuda wazuri wa thamani inayopatikana. Wateja wapya huwa wanakuwa na wasiwasi kwa sababu hawajawahi kununua, hivyo wanakosa uhakika. Kila biashara ikiweza kuwatumia wateja waliopo kupata wateja wapya, itapata wateja wengi, ambao wanakuwa ni wa uhakika na kwa gharama kidogo kabisa. Yaani njia ya kupata wateja kutoka kwa wateja, ambayo inaitwa rufaa, ndiyo njia yenye nguvu kuliko njia nyingine zote. Na ili wateja watoe wateja, lazima waombwe, kitu ambacho wauzaji wengi huwa wanahofia kufanya. Wanaona wakiwaomba wateja wao kuwapa wateja wataonekana kama wanataka kujinufaisha zaidi, au watakataliwa. Zote hizo ni hofu tu na hata zikiwa kweli, hazina madhara yoyote.

Wewe kama muuzaji bora, unapaswa kuomba rufaa kwa kila mteja ambaye unaye. Na ukimwomba leo akakuambia hana, hauwi mwisho wa kumwomba. Bali utaendelea kumwomba na kuna wakati atakupa wateja wa rufaa. Omba rufaa bila kuhofia na utapata wateja wengi wazuri kutoka kwa wateja wako.

5. Kufuatilia Bila Ukomo.

Kumfuatilia mteja mara moja au chache huwa haina nguvu ya kumshawishi. Kwa mteja ambaye haijui biashara, ufuatiliaji unapaswa kuwa wa mara nyingi na muda mrefu. Na hata kwa wateja ambao tayari wanaijua biashara, ufuatiliaji unapaswa kuwa wa mara kwa mara kwa sababu watu wanasahau haraka sana. Kwa usumbufu ambao unawazunguka watu, ni rahisi sana kukusahau. Lakini wauzaji wengi huwa wanahofia kuwafuatilia wateja mara kwa mara kwa kuona wanawasumbua. Lakini hiyo imekuwa ni hofu tu, hasa kwa wavivu ambao hawana ubunifu kwenye ufuatiliaji.

Wewe kuwa na ufuatiliaji endelevu wa wateja wako bila ya kuhofia kuwasumbua. Unachohitaji ni kuwa na ubunifu kwenye ufuatiliaji wako kiasi kwamba wateja wanapata thamani kwenye kila ufuatiliaji. Kwa njia hiyo wateja hawatakusahau na wala wewe hutawasahau.

Muuzaji bora kuwahi kutokea, umejifunza jinsi ya kutumia hofu kama kiashiria cha nini ufanye. Nenda katumie huu mwongozo ili uweze kufanya makubwa zaidi kwenye mauzo, ufanye ambayo wengi hawafanyi na uweze kuuza zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.