Rafiki yangu mpendwa,

Inapokuja kwenye swala la fedha, wengi wetu tunajua vitu viwili tu; moja ni kupata pesa na mbili ni kutumia pesa. Tofauti na hapo, hakuna kingine tunajua au kufanya kuboresha hali zetu za kifedha.

Haishangazi kwa nini watu wengi sana wanabaki kwenye umasikini, licha ya kuwa na uwezo wa kujenga utajiri.

Rafiki, kila mtu mzima ambaye anafanya shughuli yoyote ya kumwingizia kipato, anao uwezo wa kujenga utajiri kwa uhakika.

Sikia nilichosema hapo rafiki, ni KILA MTU na kwa shughuli YOYOTE anayofanya, anaweza KUWA TAJIRI kwa uhakika kabisa.

Ukisema hilo siyo kweli, kwa sababu wengi unawaona hawana utajiri licha ya kuwa na shughuli za kufanya, nitakuuliza wanajua nini kuhusu fedha na utajiri?

Huenda utasema kinachowazuia watu wasijenge utajiri ni kwa sababu vipato wanavyoingiza ni vidogo sana, ambavyo haviwatoshi hata kuendesha maisha yao.

Na hilo litaashiria jinsi ambavyo wengi hawaelewi kuhusu USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI, somo muhimu sana ambalo limekuwa halifundishwi shuleni au nyumbani.

USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI ni zaidi ya kupata pesa na kutumia pesa. Ni kuwa na mpango wa kutengeneza kipato, kudhibiti matumizi, kuweka akiba na kuwekeza. Ni kupitia mpango wa usimamizi wa fedha binafsi ndiyo kila mtu anaweza kutumia kipato alichonacho, hata kama ni kidogo, kujenga utajiri mkubwa.

Wengi wanaposikia kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, huwa wanaona ni kitu kinachowahusu wale wenye fedha nyingi. Wanaona wakiwa na fedha ndogo hawahusiki. Lakini ukweli ni kwamba usimamizi wa fedha binafsi unamhusu kila mtu ambaye ana kipato na anataka kujenga utajiri.

Rafiki, wacha nikupe mfano mmoja dhahiri ili unielewe.

Kwenye ajira, mtu anapoajiriwa huwa anaambiwa mshahara ambao atalipwa. Lakini unapofika wakati wa kulipwa mshahara, huwa anaishia kupata pungufu kuliko kiasi alichoambiwa.

Hiyo ni kwa sababu kuna makato huwa yanaondolewa kwenye mshahara wa mtu kabla hata hajaupokea. Makato hayo ni kodi, mafao na mengine. Swali ni je watu wanaendeshaje maisha yao licha ya kipato chao kidogo kukatwa? Na jibu unalo, wanajifunza kuishi kwenye kile kilichobaki.

Huwezi kuwakuta wafanyakazi wanakataa kupokea pungufu ya mshahara kwa sababu ya makato ambayo yamefanyika. Wanajua hayo ni ya lazima na hivyo kujifunza kuishi kwenye kiasi kilichobaki.

Kama kila mshahara unakatwa, uwe mkubwa au mdogo, kwa nini inapokuja kwenye kujenga utajiri sababu ya kwanza inakuwa ni udogo wa kipato? Kama vipato vidogo vimekuwa vinakatwa tozo mbalimbali na bado watu wanaishi, ina maana kwamba vinaweza kutumika kujenga utajiri na watu wakajikwamua.

Mfano huo hapo juu unatudhihirishia vitu viwili ambavyo ni muhimu sana kwenye usimamizi wa fedha binafsi;

Moja ni kila kipato kinaweza kukatwa kiasi fulani na kuwekwa pembeni. Hivyo kila mwenye kipato, hata kama ni kidogo kiasi gani anaweza kuweka akiba.

Mbili ni kila mtu anaweza kuishi chini ya kipato chake na maisha yakaenda. Hivyo kila mwenye kipato anaweza kudhibiti matumizi yake ili asitumie kipato chote.

Rafiki, nikukaribishe kwenye mjadala wa USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI. Kwenye maoni hapo chini, shirikisha yafuatayo;

1. Elimu uliyonayo kuhusu fedha ulijifunza wapi?

2. Kama ungepata elimu sahihi ya fedha mapema, ni mambo gani ungeyafanya tofauti kwenye eneo la fedha?

3. Ni hatua gani za tofauti ambazo unachukua sasa kwenye eneo la usimamizi wa fedha binafsi?

4. Ni hatua gani unachukua kwa watoto wako na watu wengine wa karibu ili wasichelewe kujua kuhusu usimamizi wa fedha binafsi na kuchukua hatua?

Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini ili tuendelee kujifunza.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala wa aina hii na washiriki walikuwa na maoni mazuri waliyoshirikisha. Fungua kusikiliza mjadala huo ili uendelee kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.