Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mauzo ni watu, hivyo popote pale ambapo kuna watu, kuna fursa ya kufanya mauzo. Ndiyo maana njia zote za usakaji wa wateja kwenye biashara, zinahusisha kuwafikia watu kwa wingi zaidi.

Matukio na shughuli za kijamii huwa vinawakusanya watu wengi kwa pamoja na hivyo kutoa fursa kwetu wauzaji kuwafikia watu hao kwa pamoja.

MATUKIO YA KIJAMII YANAYOWALETA WATU PAMOJA.

Baadhi ya matukio ya kijamii yanayowaleta watu wengi pamoja ni kama ifuatavyo;

1. Sherehe ambazo zinahudhuriwa na watu wengi.

2. Misiba ambayo inahudhuriwa na watu wengi.

3. Majanga yanayowagusa watu wengi kwenye jamii na kuungana pamoja.

4. Mikutano inayowaleta pamoja watu kwenye jamii.

5. Mashindano mbalimbali yanayokuwa yanaendeshwa kwenye jamii.

Chochote ambacho kinawafanya watu kwenye jamii fulani kukusanyika pamoja, kinaleta fursa ya kuwafikia watu hao kwa pamoja na urahisi.

NJIA ZA KUWAFIKIA WENGI ZAIDI KWENYE MATUKIO YA KIJAMII.

Pamoja na matukio ya kijamii kuwaleta watu pamoja, bado unahitaji kufanya kazi kama muuzaji ili uweze kuwafikia wengi, wajue kuhusu uwepo wako na biashara yako.

Kwa sababu matukio hayo ya kijamii siyo kwa ajili ya kuuza, huwezi kufanya mauzo moja kwa moja au kujitangaza moja kwa moja. Badala yake unapaswa kutumia fursa zilizopo kuonekana na kueleweka bila ya kujitangaza moja kwa moja.

Njia za kufanya hivyo ni kama ifuatavyo;

1. Kuvaa mavazi yenye nembo, rangi na jina la biashara yako. Kupitia mavazi watu wanakuona na kujua kuhusu biashara yako bila hata ya kuwaambia.

2. Kupata fursa ya kuzungumza kwenye tukio husika na kujitambulisha wakati wa mazungumzo, ukitaja biashara yako.

3. Kuwa na kadi za biashara ambazo unazigawa kwa wale unaokutana nao kwenye tukio husika.

4. Kusalimiana na watu unaokutana nao kwenye tukio hilo, huku ukijitambulisha jina na biashara yako.

5. Kwenye matukio yanayotoa nafasi ya biashara kuweka mabango na kufanya maonyesho, hiyo ni fursa nyingine nzuri ya kutumia.

Kwa kila tukio la kijamii unaloshiriki, hakikisha watu wanajua kuhusu wewe na biashara yako ili uweze kuwafikia wengi na kutengeneza wateja wapya tarajiwa.

SOMA; Njia 10 Za Kujenga Mtandao Wako Bila Kwenda Baa.

FAIDA ZA KUTUMIA MATUKIO YA KIJAMII KUWAFIKIA WENGI.

Kama ambavyo tumeona, matukio ya kijamii yanawakusanya watu wengi kwa pamoja na hivyo kutoa fursa ya kuwafikia watu wengi kwa pamoja.

Faida zaidi za kutumia matukio ya kijamii kuwafikia wengi ni kama ifuatavyo;

1. Kurahisisha zoezi la kukutana na watu ana kwa ana. Kuwafikia mtu mmoja mmoja ana kwa ana inachukua muda. Kuweza kukutana nao wengi kwa pamoja inarahisisha zoezi hilo.

2. Kuwafikia kirahisi watu ambao ni vigumu kuwafikia. Kuna watu ambao kwa hali ya kawaida ni vigumu sana kuwafikia. Lakini wanapokuwa kwenye matukio ya kijamii, inakuwa rahisi kuwafikia na kuweza kupata nao miadi. Mfano mtu ambaye ana wadhifa wa juu na kumfikia lazima upitie watu wa chini ambao hawakupi nafasi, kwenye matukio ya kijamii watu hao wa chini wanakuwa hawawezi kukuzuia kuwafikia.

3. Kukuza mtandao wako wa wale unaowajua na wanaokujua wewe. Kwenye mauzo, ukubwa wa mtandao wako ndiyo ukubwa wa kipato chako. Kwa kushiriki matukio ya kijamii, unakuza zaidi mtandao wako na hivyo kuweza kufanya mauzo makubwa zaidi.

4. Kuweza kupata rufaa za moja kwa moja. Kwa kushiriki kwenye matukio ya kijamii, unaweza kuwatumia wale unaojuana nao kukutambulisha kwa wengine waliopo kwenye shughuli hizo ambao hawakujui. Na hapo unaaminika kwa urahisi na wale wapya uliounganishwa nao.

5. Kujifunza kwa wafanyabiashara wengine jinsi wanavyotumia matukio ya kijamii kuwafikia wengi na kuwa na ushawishi. Kwa kuwa kwenye kila tukio kunakuwa na wafanyabiashara wengi na wenye mbinu mbalimbali ni njia pia ya kujifunza kutoka kwao.

Wajibu wako kama muuzaji ni kujua matukio na shughuli za kijamii zinazokuwa zinaendelea kwenye jamii inayokuzunguka na kuhakikisha unashiriki. Unaposhiriki hakikisha unafanya yale ambayo yanakuwezesha kuwafikia watu wengi zaidi na kutengeneza wateja tarajiwa utakaoweza kuwauzia.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.