Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye sehemu ya kwanza ya sheria za kujenga utajiri kutoka kitabu cha THE RULES OF MONEY kilichoandikwa na Richard Templar tulipata sheria ya 20 mpaka sheria ya 45.
Kwenye sheria hizo tumejifunza mambo ya kuzingatia kwenye kujenga utajiri, ambayo kila mtu anaweza kuyafanya ila wengi hawafanyi.
Kwenye sehemu hii ya pili ya sheria za kujenga utajiri, tunaenda kupata sheria nyingine ambazo zimejikita kwenye kuweka akiba na kuwekeza. Hayo ni maeneo muhimu sana ambayo wengi huyazembea na kushindwa kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao.

Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili kujenga utajiri wa uhakika kwenye maisha yako.
SEHEMU YA II; KUJENGA UTAJIRI.
Sheria ya 46; Weka akiba kiwango kikubwa.
Pamoja na kuweka akiba kwa viwango vidogo vidogo kwenye kila kipato unachoingiza, unapaswa kukazana kukuza sana kipato chako na kisha kuweka akiba kwa kiwango kikubwa. Unapoweka akiba kubwa kwa pamoja, unafidia muda uliochelewa kuweka akiba.
Sheria ya 47; Usikodi, bali nunua.
Kwa vitu ambavyo unatumia kwa muda mrefu, kama nyumba na gari, kukodi unapoteza fedha nyingi kuliko kununua au kujenga. Pale unapomiliki mali unayotumia kwa muda mrefu, unaokoa gharama nyingi.
Sheria ya 48; Elewa maana ya uwekezaji.
Uwekezaji una faida mbili; kuingiza kipato (kupata gawio au marejesho) na kuongezeka thamani. Hivyo unapofanya uwekezaji, angalia nafasi ya kupata hizo faida mbili. Tambua pia kila uwekezaji huwa una hatari zake.
Sheria ya 49; Jenga mtaji kisha wekeza vyema.
Watu wengi hawatajiriki kwa sababu wanatumia kipato chao chote na hivyo hawawekezi. Kwa kila kipato unachoingiza, unapaswa kuweka akiba na kisha kuiwekeza vizuri ili kujenga utajiri.
Sheria ya 50; Elewa kwamba uwekezaji wa mali kwa muda mrefu hauzidi uwekezaji wa hisa.
Aina kubwa mbili za uwekezaji ni kwenye mali (ardhi na majengo) na kwenye hisa. Watu wengi huona uwekezaji wa mali ndiyo wenye ukuaji mkubwa. Lakini ukiangalia kwa muda mrefu, uwekezaji wa hisa huwa na ukuaji mkubwa kuliko uwekezaji wa mali. Japo pia kila uwekezaji bado una hatari zake. Hakikisha unafanya uwekezaji maeneo yote ili kunufaika na kupunguza hatari.
Sheria ya 51; Bobea kwenye sanaa ya uuzaji.
Kuuza ndiyo kazi ya kwanza ya kila mtu. Kila mmoja wetu ni muuzaji na kitu cha kwanza tunachofanya ni kujiuza sisi wenyewe ili tukubalike na watu wengine. Huwezi kupata pesa bila kuuza, ukaijiriwa unauza muda, ujuzi na uzoefu wako kwa wengine. Ukiwa kwenye biashara unauza bidhaa na huduma ulizonazo. Bobea kwenye mauzo na utaweza kutengeneza kipato kikubwa kadiri utakavyo.
Sheria ya 52; Jione kama wengine wanavyokuona.
Wajibu wako mkubwa ni kuwashawishi watu wengine wakubaliane na wewe. Watu watakubaliana na wewe kama wanakuamini na watu wanakuamini kulingana na vile unavyoonekana kwao. Wajibu wako ni kujenga mwonekano ambao watu wanategemea kuuona kwako, kwa vile unavyojiweka na kile unachofanya. Onyesha sehemu za haiba yako ambazo watu wanataka kuziona.
Sheria ya 53; Usiamini unaweza kushinda mara zote.
Kuna vitu ambavyo huwezi kuvishinda kwenye maisha yako. Hivyo unapaswa kuachana navyo na kuhangaika na yale ambayo unaweza kushinda. Pia jua kwenye maeneo mengi hakuna haki wala usawa, hivyo kuwa na tahadhari ili usiishie kuumia au kupoteza.
Sheria ya 54; Usichague hisa mwenyewe kama hujui.
Kama huna uelewa wa uwekezaji kwenye hisa, usifanye uwekezaji huo, kwa sababu utafanya maamuzi mabovu. Jifunze kwanza uwekezaji kabla ya kuanza na anza kidogo kidogo kisha kua. Wakati ambapo bado hujaelewa uwekezaji wa hisa, wekeza kwenye mifuko ya pamoja ambayo inawekeza kwa niaba yako.
Sheria ya 55; Elewa jinsi soko la hisa linavyofanya kazi.
Kwenye soko la hisa, watu wananunua na kuuza hisa wanazomiliki kwenye makampuni mbalimbali. Kanuni ya mafanikio kwenye hisa ni kununua kwa bei ndogo na kuuza kwa bei kubwa. Hiyo inakutaka uweze kuchagua vizuri makampuni kwa kuangalia thamani yake na kukaa na uwekezaji kwa muda mrefu. Epuka kufuata mkumbo au kuvizia soko, ni hatari na hatari na hasara ni kubwa.
SOMA; Sheria Za Fedha; Sheria Za Kujenga Utajiri – Sehemu Ya Kwanza.
Sheria ya 56; Nunua hisa unazozielewa.
Kununua hisa kwa ajili ya kuziuza baadaye kwa bei ya juu zaidi ya uliyonunulia ni kucheza kamari na hatari ya kupoteza ni kubwa. Nunua hisa ambazo unazielewa kampuni na unaelewa thamani inayotolewa.
Sheria ya 57; Tumia kichwa chako.
Fanya maamuzi ya uwekezaji kwa kufikiri (kichwa) na siyo kwa hisia (moyo). Fanya ukokotozi wa kifedha kabla ya kuwekeza na siyo kusukumwa na tamaa au mkumbo.
Sheria ya 58; Tumia wataalamu wa uwekezaji.
Kama huna uelewa wa jinsi ya kuwekeza, tumia wataalamu wa uwekezaji ambao tayari wana ujuzi na uzoefu wa kufanya uwekezaji. Hapa unapaswa kuwa na tahadhari wakati wa kuchagua wataalamu, maana kuna ambao siyo waaminifu na hivyo kukushauri isivyo sahihi. Kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja ni njia nzuri ya kutumia wataalamu kunufaika na uwekezaji.
Sheria ya 59; Ukitaka ushauri mzuri wa fedha, lipia.
Watu wengi wapo tayari kukupa ushauri wa bure kuhusu fedha na utajiri, lakini ni ushauri ambao utakugharimu sana. Kupata ushauri sahihi wa kifedha, walipe wale wenye utaalamu kwenye eneo hilo. Na ambao wananufaika na ada unayowalipa na siyo kutegemea kupata kamisheni kwa yale wanayokushauri. Kama mshauri atapata kamisheni kwa kukushauri uwekeze sehemu fulani, unajua kabisa huo ushauri hauwezi kuwa mzuri kwako bali kwake yeye. Nje ya wataalamu wa fedha na uwekezaji, chukua ushauri wa fedha na utajiri kwa watu ambao tayari wameweza kujenga utajiri kwa njia sahihi na siyo waliorithi au kushinda bahati nasibu. Wengine nje ya makundi hayo hawana cha kukushauri kuhusu fedha na utajiri.
Sheria ya 60; Usivuruge mkakati unaofanya kazi.
Baada ya kuweka mkakati wako wa fedha na uwekezaji na ukawa unafanya kazi, usiuvuruge, badala yake endelea kunufaika nao. Ni tabia yetu binadamu kupenda kuboresha vitu hata kama havihitaji maboresho. Kuwa na subira ili uweze kunufaika na mkakati wowote unaokuwa umejiwekea.
Sheria ya 61; Fikiri kwa muda mrefu.
Kwenye uwekezaji, usicheze mchezo wa muda mfupi, faida ya uwekezaji ipo kwenye muda mrefu. Kadiri uwekezaji unavyofanyika kwa muda mrefu bila kuingiliwa, ndivyo faida inavyokuwa kubwa. Kutengeneza utajiri mkubwa ni kitu kinachohitaji muda mrefu, jipe muda huo.
Sheria ya 62; Panga muda wa siku ambapo utafanyia kazi mkakati wako wa utajiri.
Unapaswa kufanyia kazi mkakati wako wa utajiri kila siku. Ili hilo liwezekane, panga kabisa muda wa siku ambao utakuwa unafanya hilo. Uwe muda ambao akili yako ina nguvu na una utulivu mkubwa.
Sheria ya 63; Weka umakini kwenye maelezo.
Kwa kila maamuzi unayofanya, weka umakini kwenye maelezo yote yaliyopo. Kutokuzingatia maelezo
Sheria ya 64; Tengeneza vyanzo vipya vya kipato.
Kudhibiti matumizi yako ili kuweza kuweka akiba na kuwekeza ni mkakati mzuri. Lakini fedha kubwa inapatikana kwa kuongeza vyanzo vya kuingiza kipato. Matajiri wote wana vyanzo vingi vya kuingiza kipato. Tumia fursa zinazokuzunguka na ujuzi ulionao kuongeza vyanzo vya kipato.
Sheria ya 65; Jifunze kucheza, “Vipi kama … ?”
Kwenye kila maamuzi unayofanya, jiulize swali la Vipi kama … ? Ili uweze kuangalia pande zote kabla ya kuamua. Jiulize kama mambo yataenda tofauti na ulivyotarajia, itakuwaje? Lengo siyo usifanye, bali kuwa na maandalizi sahihi pale matokeo yanapokuwa tofauti.
Sheria ya 66; Dhibiti matumizi unayofanya kwa hisia.
Njia ya uhakika ya kupoteza utajiri wako ni kutumia kipato chako chote. Hilo linatokea pale mtu anaposukumwa na hisia zake kufanya matumizi. Unapaswa kudhibiti hisia zako ili uweze kujenga utajiri.
Sheria ya 67; Achana na matangazo ya kupata utajiri kwa haraka.
Kuna utapeli mwingi kwenye kupata utajiri kwa haraka. Watu pekee wanaopata utajiri kwa haraka ni wanaoendesha hiyo michezo ya kitapeli. Hakuna njia ya kujenga utajiri kwa haraka bila ya kufanya kazi. Mpumbavu hutenganishwa na fedha zake haraka sana, hivyo usiwe mpumbavu.
Sheria ya 68; Hakuna siri.
Kamwe usije kulipia kitu unaambiwa ni siri ya kujenga utajiri, hakuna siri. Anayekuuzia siri ya kujenga utajiri anataka kukutapeli. Tambua hakuna mtu yeyote anayeweza kukufanya wewe uwe tajiri isipokuwa wewe mwenyewe. Kujenga utajiri; NUNUA KWA BEI CHINI NA UZA KWA BEI JUU. Ni hivyo tu.
Sheria ya 69; Usisome tu, FANYA kitu.
Kusoma ni hatua moja, lakini haitakuwa na maana kama hautafanyia kazi yale unayojifunza. Huenda vitu vingi unavyojifunza unajiambia tayari unavijua, lakini je unafanya nini? Anza kwa kuchukua hatua ndogo ndogo na kukua. Mabadiliko ya kweli yanatokana na kuchukua hatua za tofauti.
Hizo ndizo sheria za kujenga utajiri kutoka kwenye kitabu cha THE RULES OF MONEY. Zingatia sheria hizi na zifanyie kazi ili uweze kuongeza kipato chako na kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.
Masomo yote ya kitabu cha THE RULES OF MONEY kilichoandikwa na Richard Templar, ambayo yana sheria zote za fedha za kujenga na kutunza utajiri, yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mzuri juu ya sheria hizi za kufikiri kitajiri. Fungua na ujifunze ili uweze kufikiri kwa usahihi hasa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.