Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya saba ambayo ni mfanye mtu aone ni wazo lake.
Na kwenye kanuni ya saba tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni hakuna mtu anayependa kuambiwa au kupangiwa kitu cha kufanya. Kwa sababu kila mtu huwa anaamini anajua anachopaswa kufanya.
Hivyo kama kuna kitu unataka mtu afanye, kumwambia moja kwa moja afanye haitakupa matokeo mazuri, kwa sababu ataona unamlazimisha.
Badala yake, unapaswa kumfanya aone ni wazo lake kufanya kitu hicho.
Na unaweza kufanya hivyo kwa kujua mahitaji halisi ya mtu na kisha kupendekeza ni jinsi gani anaweza kufikia mahitaji hayo.
Hapo mtu ataona amechagua mwenyewe na hivyo kuwa tayari kufanyia kazi.
SOMA HAPA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Saba
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi yetu ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya nane ambayo ni jiweke kwenye nafasi ya mtu mwingine.
Muuzaji bora kuwahi kutokea, kama kuna mtu ambaye mnatofautiana kwa sababu fulani, hutaweza kumshawishi akubaliane na wewe kwa kumpa hoja zako. Bali utaweza kufanya hivyo kwa kujiweka kwenye nafasi yake, kwa kuvaa viatu vyake, na kuona vitu kwa mtazamo alionao yeye.
Kila mtu huwa anafikiri na kufanya kile anachofanya kwa sababu fulani, ambayo ni sahihi kwake. Hata kama anachofanya anakosea, kuna sababu sahihi kwake kufanya hivyo. Badala ya kukimbilia kumkosoa kwa kufanya anachofanya, kwa nini kwanza usijue sababu inayomsukuma kufanya hivyo?
Utaweza kujua sababu hiyo kwa kujiweka kwenye nafasi yake, kuangalia jambo kwa mtazamo wake na siyo mtazamo wako. Kwa kujiweka kwenye nafasi yako, na kuwa kwenye hali anayopitia pamoja na mtazamo alionao, utaona kwa nini anafanya anavyofanya na hapo utaweza kumshawishi kufanya kilicho sahihi.

Mwandishi wa kitabu cha How To Win Friends and Influence People Dale Carnegie anamnukuu Kenneth M.Goode aliyekua mwandishi kwenye eneo la mahusiano ambaye anasema kabla hujamkabili mtu unayetofautiana naye, jiulize ni kwa kiasi gani unathamini mawazo yako na maamuzi yako, jua hivyo pia ndivyo mtu mwingine anavyothamini mawazo na maamuzi yake. Kwa kujua hilo na kujaribu kujiweka kwenye nafasi ya mwingine, utaweza kujua njia sahihi ya kumkabili na akakubaliana na wewe.
Kabla hujamtaka mtu afanye kitu chochote kile, jiweke kwanza kwenye nafasi yake, jua nini kinaweza kumsukuma afanye unachotaka afanye. Iwe ni kitu unauza au mchango unaomba, usifikirie wewe unataka nini, bali yule unayemshawishi anataka nini. Kwa kujiweka kwenye nafasi yake, na kuwa na mtazamo wake, utapata njia sahihi ya kumshawishi afanye unachotaka afanye.
Hatua ya kuchukua leo; kama utaondoka na kitu kimoja hapa ni hiki; mara zote fikiria kwa kujiweka kwenye nafasi na mtazamo wa mtu mwingine, ona vitu kama anavyoona yeye na kisha kama unavyoona wewe, na hilo litakusaidia kwenye kuwashawishi watu na kupata unachotaka.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504