Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye mwendelezo wa masomo ya NJIA KUMI ZA KUJENGA UTAJIRI kutoka kitabu kinachoitwa THE TEN ROADS TO RICHES kilichoandikwa na Ken Fisher.
Kwenye somo lililopita tulijifunza njia ya kwanza na ya pili ya kujenga utajiri. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza njia ya tatu na ya nne katika njia 10 za kujenga utajiri. Karibu ujifunze.

NJIA YA TATU; KUUNGANA NA WENYE MAONO MAKUBWA.
Kama uko vizuri kwenye kujua watu ambao wanaweza kupata ushindi mkubwa na hutaki kuwa kiongozi au bosi, basi njia ya kuwa msaidizi wa wenye maono makubwa itakufaa.
Kwenye njia hii unakuwa msaidizi wa karibu wa kiongozi wa juu wa biashara, ambaye unaaminiwa na kupewa majukumu makubwa. Japokuwa wanaotumia njia hii huwa hawawi viongozi wakuu, bado huwa wanapata utajiri mkubwa kwa sababu ya muda mrefu wanaokaa kwenye taasisi na uwekezaji wanaokuwa wamefanya ndani yake.
Wasaidizi hao huwa wanakuwa ni watu muhimu na wa kutegemewa sana kwenye biashara, na huwa wanatekeleza majukumu muhimu ambayo mkurugenzi mkuu wa biashara hawezi kuyatekeleza kutokana na nafasi yake kuwa ya wazi kwa umma.
Msaidizi huyu anakuwa ni mbia muhimu, ambapo CEO hawezi kutekeleza majukumu yake bila yeye.
Kufanikiwa kwenye njia hii, mtu unapaswa kuchagua vizuri tasnia, kampuni na CEO. Kwa sababu ni njia inayotaka mtu kufanya kazi kwa muda mrefu na kuonyesha uwezo ili kuaminiwa.
Njia hii inataka mtu awe na uaminifu wa hali ya juu sana. Kutiliwa mashaka kwenye uaminifu ni kitu ambacho kitamkwamisha mtu kwenye njia hii.
Anayechagua nafasi ya usaidizi ni lazima ajitoe sana kwa kuwa na mtazamo wa NAFANYA na siyo NIKIWEZA. Yaani anapoambiwa afanye kitu, anasema NAFANYA hata kama hajui kitu hicho kinafanywaje.
Ni uwezo wao wa kukamilisha majukumu muhimu kwa ukuaji wa biashara ndiyo unawapa fursa ya kuaminika na kuweza kujenga utajiri mkubwa sana.
Safari ya usaidizi kwa kiongozi mkuu wa biashara ni safari ya maisha, safari inayomtaka mtu ajitoe sana, kuliko hata anavyofanya kwenye ndoa.
JINSI YA KUTUMIA NJIA HII;
Kama unataka kujenga utajiri mkubwa lakini hutaki kuanzisha biashara au kuwa kiongozi mkuu, tafuta biashara unayoikubali na yenye kiongozi ambaye unamkubali sana. Kisha tafuta kazi kwenye biashara hiyo na fanya kazi kwa juhudi kubwa huku ukiwa mwaminifu sana. Panda madaraja ya kazi kwenye biashara hiyo mpaka kufika kuwa msaidizi wa kiongozi mkuu. Na hapo utapewa majukumu makubwa pamoja na kipato kikubwa pia.
Kazi nzuri ya kuanza nayo ni ya mauzo, kila biashara inataka wateja zaidi na mauzo zaidi. Ukiweza kujifunza na kuwa muuzaji bora, kisha ukaleta mapinduzi ya mauzo kwenye biashara, utapata fursa ya kupewa majukumu zaidi na kulipwa zaidi.
SOMA; Kujenga Utajiri Kupitia Kuanzisha Biashara Na Kuwa CEO.
NJIA YA NNE; KUTUMIA UMAARUFU.
Kama unapenda umaarufu na hujali kupoteza faragha yako, njia ya umaarufu inaweza kukufaa kwenye kujenga utajiri.
Watu wengi wanaposikia mafanikio na utajiri, huwa wanawafikiria watu maarufu wanaojulikana na wengi. Lakini matajiri wengi, ambao wana utajiri mkubwa, huwa siyo maarufu.
Njia ya umaarufu huwa inapendwa na wengi, lakini ndiyo yenye mchango mkubwa kwenye kuwafanya watu kuwa na utajiri mkubwa. Watu wengi maarufu huwa wanakuwa na kipato kikubwa, lakini pia matumizi yao yanakuwa makubwa na hilo kupelekea washindwe kujenga utajiri.
Njia ya umaarufu kwenye kujenga utajiri ina fursa mbili;
Fursa ya kwanza ni kutumia kipaji.
Hapa mtu anatumia kipaji chake kujenga umaarufu, hasa kupitia michezo na sanaa. Njia hii inapaswa kuanza kufanyiwa kazi kwenye umri mdogo kama mtu anataka kufanikiwa.
Watu wengi wakishavuka miaka 20 hawajaanza kufanyia kazi njia hii ya kipaji, nafasi yao ya kujenga utajiri kwa kipaji inakuwa imepita. Hiyo ni kwa sababu mafanikio ya kipaji huwa ni kwenye umri mdogo na bado mtu anatakiwa kuweka miaka mingi.
Mwandishi anasema kama unasoma hapa, njia ya kipaji imeshakupita, huwezi kutajirika kwa njia hiyo.
Fursa ya pili ni umiliki wa vyombo vya habari na burudani.
Hii ni njia ya umaarufu ambayo ipo wazi kwa wale ambao umri umeenda na wanataka kujenga utajiri kwa kutumia umaarufu wao. Kwa njia hii mtu anapata umaarufu kwa kumiliki vyombo vya habari na burudani kama redio, tv, magazeti, studio, timu za mpira n.k.
Njia hii pia inahitaji ujuzi wa biashara kwa sababu mtu anapaswa kujenga na kusimamia vizuri vitu anavyokuwa anamiliki. Umaarufu wao ndiyo unaowafanya kupata fedha zaidi kwenye vitu wanavyokuwa wanamiliki.
Njia ya umaarufu haina matajiri wengi na wakubwa na pia ni njia inayotegemea bahati zaidi kuliko juhudi. Na kwa upande wa umaarufu kwa vipaji, muda ni mfupi sana wa kuwa kwenye umaarufu na kipato kikubwa.
Lakini kama ambavyo tumeona kuna njia nyingi, anayeshindwa kwenye njia hii anaweza kurudi kwenye njia ya kwanza na kuanzisha biashara yenye mafanikio. Hivyo ndivyo wengi wanaoshindwa kwenye njia ya umaarufu wanafanya. Wanaenda kuanzisha biashara na kuweza kujenga mafanikio huko.
JINSI YA KUTUMIA NJIA HII;
Kwanza achana na njia ya kipaji, maana umri umeshakutupa mkono, labda uanze kuwaandaa watoto wako na kama wana umri wa chini ya miaka 15.
Unaweza kufanyia kazi upande wa umiliki wa vyombo vya habari na burudani, lakini ni kama kweli unapenda maisha yako kuwa wazi na kufuatiliwa na kila mtu. Vinginevyo, njia ya kujenga biashara ni bora kuliko hii, kwa sababu kuna fursa kubwa ya mafanikio na hupotezi faragha yako.
Kwenye somo hili tumeona njia ya tatu na ya nne ya kujenga utajiri kwa uhakika. Masomo ya njia zote kumi za kujenga utajiri kutoka kitabu THE TEN ROADS TO RICHES yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.
Tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Karibu uweze kusikiliza kipindi hicho ujifunze mengine mengi ambayo yapo kwenye kitabu ila hapa hayajapata nafasi. Pia usikie maoni ya wengine juu ya njia hizi za kujenga utajiri.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.