Biashara ni kauli. Kama ni kauli, basi ni mlango wa kuingilia katika biashara yako. Sababu kubwa ni kuwa, kauli inabeba maneno unayomtamkia mteja wako.

Maneno unayomtakia mteja wako yanamfanya afurahie au achukie huduma. Yanamfanya aendelee kuongea na wewe au aache.

Mteja asipokusikiliza, hatoshawishika. Kama hashawishiki, basi hutomuuzia. Kama hutouza, biashara haitakua.

Kauli nzuri humfanya mteja ashawishike kununua bidhaa yako. Kauli mbaya inazuia mazungumzo kuwa mazuri na kukaribisha mapingamizi.

Nikumbushe kuwa; mteja ni kama mpenzi, anahitaji kauli nzuri. Au ni kama ndege, anahitaji kutua sehemu salama.

Hivyo, ukimtamkia kauli mbaya atakuacha na kwenda katika sehemu nyingine salama kwake.

Chunga sana maneno unayotamka mbele ya mteja wako. Waswahili wanasema, fikiri kabla ya kutenda.

Hata Napoleon Hill aligusia kwa kusema, “Fikiri kabla ya kusema, kwa sababu maneno yako yanaweza kupandikiza mbegu ya mafanikio au chuki katika fikra za watu.”

Kama muuzaji bora kuwahi kutokea unatakiwa kuwa na kauli nzuri kwa mteja ili na  kesho arudi.

Katika hili wasemee vizuri washindani wako, usipandikize fikra mbaya. Mteja akisema mbona fulani ananiuzia bei nzuri, mwambie hongera sana.

Lakini hapa nataka nikuonyeshe thamani, ofa au hadhi kubwa utakayopata baada ya kutumia bidhaa zetu.

Faida za kuwa na kauli nzuri mbele ya mteja;

Moja; Inakutofautisha na wauzaji wengine.

Mbili; Inamfanya mteja ajione yupo sehemu salama kuliko sehemu nyingine. Hivyo kushawishika kununua.

Tatu; Inapunguza hali ya mapingamizi kuwa mengi

Kumbuka, kwenye mauzo kila kitu kinahesabika. Upe breki mdomo wako. Hakika utawashawishi wengi kununua.

Hatua za kuchukua; Jifanyie tathimini kwa wateja 100 uliohudumia siku za karibuni.

Jiulize juu ya kauli au namna ulivyozungumza nao.

Kwa walionunua, angalia namna ulivyowafanya wachukue hatua, kisha boresha hapo na uanze leo kuwahudumia wateja wako vizuri.

SOMA; Watu Hukunua Wewe Kabla Ya Bidhaa Yako; Jiuze Wewe Kwanza

Je, ni kauli ipi uliwahi kuongea kwa mteja akashindwa kununua?

Shirikisha hapa tujifunze zaidi.

Wako Wa Daima

Lackius Robert

Mkufunzi Wa Mauzo na Mwandishi

0767702659| mkufunzi@mauzo.tz

Karibu tujifunze zaidi.