Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye mwendelezo wa masomo ya NJIA KUMI ZA KUJENGA UTAJIRI kutoka kitabu kinachoitwa THE TEN ROADS TO RICHES kilichoandikwa na Ken Fisher.

Kwenye masomo yaliyopita tumejifunza njia nne kati ya 10 za kujenga utajiri. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza njia ya tano na ya sita katika njia 10 za kujenga utajiri. Karibu ujifunze.

NJIA YA TANO; KUOA/KUOLEWA NA TAJIRI.

Kuwa tajiri ni sawa na kuwa mrembo, japo watu huwa wanasema hawaoi au kuolewa kwa sababu ya mwonekano, unapokuwa mzuri inapendeza. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye ndoa na fedha, japo watu huwa wanasema hawaoani kwa sababu ya fedha, lakini uwepo wake huwa una mchango mkubwa.

Tafiti zinaonyesha kwamba vijana wengi, wa kike kwa wakiume wanazingatia uwezo wa kiuchumi wa mwenza kabla ya kufanya maamuzi ya ndoa. Hivyo hata kama siyo kwa ngazi ya utajiri mkubwa, kuangalia uwezo wa kifedha ni kigezo cha kufanya maamuzi ya ndoa.

Wapo watu ambao wameweza kupata utajiri mkubwa kupitia kuoa au kuolewa na watu wenye utajiri. Utajiri huo waliupata kwa kuwezeshwa na wenza wao, kupata mgawo baada ya talaka au kurithi baada ya mwenza kufa.

Kwa wengi, njia ya kuoa au kuolewa na tajiri ili kupata utajiri inaweza kuonekana siyo njia sahihi. Lakini kuna ambao ni njia sahihi kwao na wanaifanyia kazi kwa uhakika.

Njia hii siyo rahisi, kwa sababu wenye utajiri mkubwa sana ni wachache na wengi wao tayari wameshaoa au kuolewa. Lakini kama ilivyo kwenye njia nyingine, mtu anapodhamiria na kuweka juhudi, anafanikiwa.

Mwandishi anashirikisha baadhi ya mambo ya kuzingatia kwenye kutumia njia hii;

Moja ni kujua sheria za ndoa, talaka na mirathi kwa eneo ulipo kama unataka kutumia njia hii. Hiyo itakuwezesha kujua ni kiasi gani cha fedha unachoweza kupata.

Mbili ni kujua maeneo ambayo matajiri wanapatikana ili na wewe kuwa kwenye maeneo hayo. Matajiri wakubwa huwa wamejikusanya kwenye maeneo fulani, kuanzia makazi, shughuli zao na mengine. Kwa kuwa maeneo ambayo ni rahisi kukutana na matajiri, inarahisisha zoezi la kuwapata.

Tatu ni kufanya shughuli ambazo matajiri wanafanya ili iwe rahisi kukutana nao. Matajiri wengi huwa wanatumia muda wao wote kwenye shughuli zao. Hivyo kukutana na watu wengi, hasa ambao hawajuani nao siyo rahisi. Lakini pale shughuli zako zinapokukutanisha na matajiri, inakuweka kwenye nafasi nzuri.

SOMA; Kujenga Utajiri Kupitia Usaidizi Na Umaarufu.

JINSI YA KUTUMIA NJIA HII.

Kwa tulio wengi, hatuwezi kutumia njia hii, kwa sababu ya ugumu na changamoto zake. Lakini pia njia nyingine ni za uhakika na heshima zaidi kuliko hii. Lakini bado kuna kitu tunaweza kujifunza na kufanyia kazi kwenye njia hii ili tunufaike.

Pale unapokuwa unaanzia chini kabisa, yaani ukiwa masikini, watu wengi watakupuuza. Hata kwenye ndoa, kuna watu ungependa kuwa nao kwenye ndoa, lakini kwa hali yako duni ya kiuchumi, watakukataa. Lakini ukishapata utajiri, kila mtu ataonekana anakupenda na kutaka ndoa na wewe. Hata kama tayari una ndoa au mahusiano mengine, bado watu wenye kutaka kunufaika na utajiri wako watakutega uweze kuingia nao kwenye mahusiano.

Hivyo somo la kuondoka nalo ni ukishajenga utajiri, kuwa makini sana na wale wanaoonyesha wanakupenda na wanataka ndoa au mahusiano na wewe. Wengi hawaji kwako na upendo wa kweli, bali wana lengo la kunufaika na utajiri wako.

Pia kama unakuja kuingia kwenye ndoa baada ya kuwa umeshajenga utajiri, ingia makubaliano na mwenza wako kwamba mali ulizokuwa umechuma kabla ya ndoa hazitahusika kwenye kugawana ikitokea mmeachana. Hii ni mada muhimu ambayo wengi hawapendi kuijadili kabla ya ndoa, lakini huwa inaishia kuwaumiza wengi pale ndoa zinapovunjika.

NJIA YA SITA; KESI ZA MADAI.

Kama umekuwa unatamani kuwanyang’anya wengine utajiri wao bila ya kuvunja sheria basi njia ya kesi za madai itakufaa.

Hii ni njia ya kuwafungulia kesi za madai watu wenye utajiri mkubwa kwa lengo la kuwafanya wawe tayari kulipa ili kesi isiendelee au kama kesi ikiendelea basi kulipwa fidia.

Njia hii imekuwa inatumika zaidi na wanasheria wa kesi za madai, ambao huwa wanawatafuta watu wanyonge ambao wanaonekana kuonewa kwa namna yoyote ile na wale wenye mafanikio. Kisha wanafungua kesi ya madai makubwa, lengo likiwa siyo haki ipatikane, bali kulipwa fidia.

Kazi ya kawaida ya sheria ni ngumu na kujenga utajiri mkubwa kwa kufanya kazi za kawaida za sheria ni jambo gumu zaidi. Hiyo ni kwa sababu wanasheria wengi wanalipwa kwa masaa wanayofanya kazi na hilo huwa kikwazo kikubwa kwao.

Wanasheria wanaotumia njia ya kesi za madai huwa wanapata malipo makubwa kuliko hata wale watu wanaokuwa wanawatetea. Hilo limefanya wanasheria wengi wanaoshindwa kufanikiwa kwenye kazi za kawaida za sheria kutumia njia hii ya kesi za madai.

Pamoja na njia hii kutokuvunja sheria, lakini ni wizi kama wizi mwingine. Kwa sababu imekuwa inatumia madhaifu ya watu kuwaumiza na wakati mwingine madhara yake kuwa makubwa kuliko inavyoonekana.

JINSI YA KUTUMIA NJIA HII.

Kama wewe siyo mwanasheria, huwezi kunufaika na njia hii. Na hata kama ni mwanasheria, kuna njia nyingine unazoweza kutumia kwa amani kuliko hii. Lakini kuijua njia hii inatusaidia kuwaepuka wale ambao wanataka kujinufaisha na utajiri wako.

Iko hivi, kila mtu huwa kuna sheria anazokuwa anavunja, iwe ni kwa kujua au kutokujua. Lakini hatuadhibiwi kwa hayo kwa sababu yanakuwa hayana madhara sana. Hivyo mtu akiamua kumchunguza mtu yeyote, lazima atapata tu mahali ambapo amewahi kuvunja sheria.

Kadiri tunavyojenga utajiri, tunapaswa kuwa na mfumo wa kujilinda na wale wanaokuja kwa lengo la kujinufaisha na utajiri wetu. Hivyo tunapaswa kufanya mambo yetu kwa kuzingatia sheria. Kuepuka sana kufanya mambo ambayo yanavunja sheria wazi wazi.

Lakini pia tunapaswa kuwa na wanasheria wazuri ambao watatushauri kwa usahihi juu ya amshauri mbalimbali yatakayofunguliwa dhidi yetu. Huwezi kuwa tajiri mkubwa na ukose kesi kabisa. Kitendo tu cha kuwaajiri watu, kadiri unavyofanya kwa ukubwa, utakutana na wafanyakazi ambao siyo sahihi na utakapowafukuza kazi, wanakwenda kushitaki. Hilo linatosha kukusumbua kwa muda mrefu.

Kuwa na maandalizi sahihi inakusaidia uweze kukabiliana vizuri na changamoto hizo pale zinapokuja kwako.

Kwenye somo hili tumeona njia ya tano na ya sita ya kujenga utajiri kwa uhakika. Masomo ya njia zote kumi za kujenga utajiri kutoka kitabu THE TEN ROADS TO RICHES yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Karibu uweze kusikiliza kipindi hicho ujifunze mengine mengi ambayo yapo kwenye kitabu ila hapa hayajapata nafasi. Pia usikie maoni ya wengine juu ya njia hizi za kujenga utajiri.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.