3425; Siyo NINI, bali VIPI.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Uwepo wa watu waliofanikiwa, kwenye tasnia yoyote ile, unapaswa kufurahiwa na kutumiwa vizuri na wengine ili nao wafanikiwe.
Hata kama wale waliofanikiwa wapo kwenye tasnia nyingine na wanaotaka kufanikiwa wapo kwenye sekta tofauti kabisa, bado wanaweza kujifunza.
Hilo linawezekana kwa sababu wanachopaswa kujifunza watu ili kufanikiwa siyo NINI walichofanya wale waliofanikiwa bali wanapaswa kujifunza VIPI wamefanya hivyo.
Kama unataka kufanikiwa, usiige kile ambacho waliofanikiwa wanakifanya (NINI), badala yake iga jinsi wanavyofanya (VIPI).
Hiyo inafanya kazi kwa sababu mafanikio kwenye kila eneo la maisha huwa yanaathiriwa na vitu vya msingi ambavyo vinagusa msingi mzima wa mafanikio ya kitu.
Vitu vya msingi ambavyo vinaathiri mafanikio ya kila eneo ni mtu kujua hasa nini anachotaka kupata, kujua gharama anayopaswa kulipa ili kupata anachotaka na kisha kuamua kujitoa hasa kulipa gharama ili kupata anachotaka.
Haijalishi mtu anataka nini, kwa kujua gharama na kuwa tayari kuilipa, inarahisisha kupata kile ambacho mtu anataka.
Kilicho muhimu siyo kile ambacho mtu anafanya, bali jinsi anavyofanya kitu hicho.
Hivyo unapotaka kujifunza kitu, usiangalie watu wanafanya NINI, bali angalia wanafanya VIPI.
Pale VIPI inapozingatia misingi sahihi ya mafanikio, inakuwa ni uhakika kwa mtu anayefuata kufanikiwa.
Haijalishi unachofanya ni nini, huwa ni rahisi kupiga hatua kubwa kwa kuangalia jinsi ya kufanya na kufanikiwa kwenye njia hiyo.
Kuiga kile wanachofanya waliofanikiwa imekuwa haifanyi kazi kwa sababu mambo yanatofautiana sana.
Kitu kuleta mafanikio kwa mtu mmoja, haimaanishi kinakuwa na uhakika wa kuketa mafanikio kwa mwingine anayekifanya.
Hiyo ni kwa sababu watu wanatofautiana kwenye mengi.
Lakini njia ya kupata matokeo mazuri, huwa inaweza kutumiwa kwenye kila jambo na ikaleta matokeo mazuri.
Hivyo hupaswi kuhangaika na NINI waliofanikiwa wanafanya na kuhangaika na VIPI wamefanya mpaka kufanikiwa.
Ukiweza kurudia hiyo VIPI yao kwenye jambo lolote, mafanikio huwa ni ya uhakika.
Kila mara angalia VIPI unafanya ili kuboresha na kupata matokeo bora ya mafanikio.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe