Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi kwenye maisha wamekuwa ni wasemaji kuliko watendaji.
Lakini ambacho kitamjengea mtu sifa siyo maneno yake, bali matendo yake.
Kwa kifupi watu huwa wanapuuza yale unayosema na kushika yale unayofanya.
Unaweza kuwapigia watu kelele sana, lakini watakachoondoka nacho ni kile unachofanya.

Huwa kuna usemi kwamba vitendo vyako vinapiga kelele sana, watu hawasikii maneno yako.
Hivyo ndivyo Aliyekuwa mwanafalsafa na mtawala wa Roma ya kale, Marcus Aurelius alivyoandika kwenye kitabu chake cha Meditations.
Marcus alisema hatupaswi kupoteza muda mwingi kueleza mtu mwema anapaswa kuwaje, badala yake tunapaswa kuwa watu wema.
Kwa maneno mengine ni tusiwe watu wema kwa nadharia, kueleza nini kinapaswa kufanyika. Badala yake tunapaswa kuwa watu wema kwa vitendo, kwa kufanya yale yanayopaswa kufanyika.
Marcus anaeleza wema wetu unaanza kwa kujitambua sisi wenyewe na nafasi yetu kwenye dunia, kisha kuishi hivyo. Sisi binadamu tuko hapa duniani kwa wajibu maalumu, hivyo wajibu wetu ni kujua wajibu huo na kuutimiza. Kadiri unavyojua hilo na kuliishi, kwa namna ambayo unakuwa na mchango mzuri kwa wengine, ndivyo unavyonufaika.
Lakini pia wema unatutaka kuwachukulia wengine kwa usahihi kwa yale wanayofanya. Pale watu wanapokosea, tunapaswa kuwarekebisha kwa usahihi. Lengo ni kuhakikisha wanafanya kwa usahihi. Na kama hilo litatushinda, basi hatupaswi kuwalaumu watu hao. Bali tunapaswa kuangalia namna ya kuendana nao au kuachana nao kabisa. Hii haimaanishi tuvumilie uzembe au makosa ya wengine, bali tusikubali yale wanayofanya wengine yakatuvuruga.
SOMA; Falsafa Ya Ustoa; Chanzo Cha Mateso Ni Kupuuza Fikra Zako.
Kuwa mwema pia kunahusisha kuishi kwa sifa ambazo umeshawaonyesha wengine. Kwa namna unafanya mambo yako, watu wanakupa sifa fulani. Kwa zile sifa ambazo ni nzuri, unapaswa kuhakikisha unazitunza, kwa kuendelea kufanya yale yaliyopelekea wengine wakusifie. Na pale unapoteleza na kwenda kinyume na sifa hizo, unapaswa kujirekebisha na kurudi kwenye sifa zako. Hilo litapelekea uaminike na kutegemewa na wengine kupitia sifa ambazo unazo na umezitunza.
Wema ni kupokea mabadiliko yote kwa usawa, bila ya kulalamika wala kulaumu. Unajua kwamba kila kitu kinabadilika, lakini pale mabadiliko yanapokuumiza ni rahisi kuona siyo sahihi. Unakuwa mtu mwema pale unapopokea mabadiliko, hata kama yanakuumiza wewe moja kwa moja. Unapopokea yale ya asili kwa namna yanakuja kwako, inakupa utulivu na kutunza sifa zako kwa wengine.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri juu ya kuwa mtu mwema kwa vitendo na siyo maneno pekee. Karibu ujifunze zaidi kwenye kipindi hicho na uweze kuweka hayo unayojifunza kwenye vitendo ili maisha yako yaweze kuwa bora.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.