Rafiki yangu mpendwa,
Jim Rhon aliwahi kunukuliwa akisema; “Unalipwa kulingana na thamani unayopeleka sokoni.”
Hiyo ni kauli ambayo mtu ukiielewa na kuiishi kwa uhalisia wake, utaweza kulipwa kiasi chochote kile unachotaka.
Kabla ya kuangalia hilo la thamani, turudi kwenye mazoea ambayo wengi wanayo.
Inapokuja kwenye kulipwa, watu huwa wanadhani malipo zaidi yanatokana na muda zaidi kwenye kile wanachofanya. Matokeo yake ni wanakaa kwenye kitu kwa muda mrefu, lakini malipo yao yanakuwa ni madogo.

Hili linaonekana wazi kwa watu ambao wameajiriwa na kukaa kwenye ajira kwa muda mrefu lakini kipato chao hakiongezeki. Wanaweza kuwalaumu sana waajiri wao kwa kutokuwaongezea mshahara licha ya kuwa kwenye kazi kwa muda mrefu.
Wanachoshindwa kujua ni kwamba mwajiri haangalii muda ambao mtu amemfanyia kazi, bali thamani gani ambayo anampa. Kwa kutegemea muda ulete ongezeko la kipato imewafanya wengi kubaki na kipato duni.
SOMA; Ongeza Thamani Yako Ulipwe Zaidi Kwa Kufanya Jambo Hili Kila Siku.
Halafu kuna upande wa pili, wa malalamiko ya watu kwamba mabosi wanalipwa sana wakati hawafanyi kazi ngumu kama wafanyakazi wa chini.
Ukienda kwenye taasisi yoyote kubwa, unakuta bosi wa juu analipwa mshahara mkubwa sana, zaidi hata ya mara 10 ya mshahara wa mfanyakazi wa kawaida. Wakati huo huo mfanyakazi wa kawaida anaweza kuwa anafanya kazi ngumu na kwa muda mrefu kuliko bosi.
Ambacho hawaelewi wale wanaolalamikia hilo ni kwamba bosi anakuwa anatoa mchango mkubwa kwenye taasisi kuliko ule unaotolewa na mfanyakazi wa chini.
Na hivyo ndivyo thamani ambayo mtu unatoa inavyopelekea uingize kipato kikubwa.
Kipato unacholipwa sasa, iwe umeajiriwa au unafanya biashara, kinatokana na thamani unayotoa sasa.
Kama unataka kuongeza kipato chako zaidi, mahali pa kuanzia ni kuongeza thamani unayoitoa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekuonyesha jinsi unavyoweza kuongeza thamani yako kwa ukubwa na haraka ili uweze kulipwa zaidi ya unavyolipwa sasa. Njia nilizokushirikisha ni za uhakika na zinafanya kazi haraka kama utazifanyia kazi. Fungua hapo chini ujifunze na uweze kuingiza kipato kikubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.