Rafiki yangu mpendwa,

Hadithi za kulala masikini na kuamka tajiri zimekuwa zinapendwa sana na watu wengi.

Wengi hudhani kuna njia ya mkato ya kupata utajiri, ambayo wakiweza kuipata tu basi wanakuwa wameagana na umasikini kabisa.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna utajiri mkubwa wa kudumu unaojengwa kwa njia yoyote ya mkato na haraka. Kila unayemwona ameweza kujenga utajiri mkubwa, imemchukua muda, kudhamiria kweli na kuongozwa kwa malengo.

Mwandishi Chris Hogan kwenye kitabu chake kinachoitwa EVERYDAY MILLIONAIRES ameonyesha jinsi watu wa kawaida kabisa walivyoweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao na jinsi hata wewe unaweza kufanya hivyo.

Kitabu hicho ni matokeo ya utafiti uliofanywa kwa mamilionea zaidi ya elfu 10 na kuweza kupata taarifa nyingi sana kuwahusu. Utafiti huo uligusa kila eneo la matajiri, kuanzia mitazamo, fikra, shughuli wanazofanya, mahusiano, familia n.k.

Kupitia matokeo ya utafiti huo, Hogan aliweza ameweza kuainisha SIFA KUU SITA ambazo matajiri wanazo ila masikini wamekuwa hawana. Kupitia masomo haya utajifunza sifa hizo na hatua za kuchukua ili na wewe uweze kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

SURA YA 7; FANYA KWA MAKUSUDI (KUISHI CHINI YA KIPATO).

Utajiri siyo kitu kinachotokea kama ajali, bali ni kitu kinachotokea kwa makusudi. Kufanya kwa makusudi ni mtu kudhamiria kweli na kuchukua hatua ili kupata matokeo anayokuwa anayataka.

Watu wengi wamekuwa wanajiendea na maisha vile yanavyoenda, wakiwa hawajadhamiria chochote, halafu wanakuja kushangaa pale wanapokuwa wameishia.

Matajiri hawaishi maisha yao kwa kubahatisha, badala yake wanajua kabisa ni nini wanachotaka kupata na hivyo kuchukua hatua za makusudi za kuhakikisha wanafika wanakotaka.

Moja ya vitu ambavyo wale wanaojenga utajiri wamekuwa wanavifanya kwa makusudi kabisa ni kuishi chini ya kipato chao. Kwa kipato chochote ambacho wanaingiza, huwa wanahakikisha matumizi wanayofanya hayazidi kipato hicho.

Matajiri wote huwa wana bajeti ya matumizi ya kipato chao. Na huwa wanaendelea kuishi kwa bajeti hata baada ya kuwa wameshapata utajiri na hawalazimiki tena kufanya hivyo.

Masikini huwa hawapendi kusikia neno bajeti. Huwa wanaona kuwa na bajeti ni kujinyima na kujitesa. Matokeo yake ni wamekuwa wanatumia kipato chao chote na hata kuzidisha kwa kukopa na hilo kuwafanya wabaki kwenye umasikini.

Hatua ya kuchukua;

Weka bajeti ya kipato unachoingiza ili matumizi unayofanya yawe chini ya kipato hicho. Kwa kila kipato hakikisha kuna sehemu ambayo unaweka akiba na kuiwekeza kwa ajili ya kujenga utajiri.

Epuka sana madeni binafsi ambayo unayalipa kwa riba. Kwani hayo yanakudidimiza kwenye umasikini na kuifanya safari yako kuwa ngumu zaidi. Kwa kuchagua kuishi chini ya kipato chako, utazuia kuingia kwenye madeni. Na kama tayari ulishaingia kwenye madeni, ondokana na madeni hayo ili uweze kujenga utajiri.

SOMA; Amini Na Wajibika Binafsi Kujenga Utajiri Mkubwa.

SURA YA 8; KUFIKIRI MBELE (KUONGOZWA NA MALENGO).

Kujenga utajiri mkubwa ni kitu kinachochukua muda mrefu. Njia pekee ya mtu kuweza kufanya hivyo kwa muda mrefu ni kuwa na malengo yanayomwongoza.

Watu wengi huwa hawadumu kwenye safari ya kujenga utajiri kwa sababu hawawezi kuvumilia kwa muda mrefu. Wanafikiria vitu vya karibu pekee. Matajiri wanadumu kwenye safari hii kwa sababu wanafikiri kwa muda mrefu na kuweka malengo ambayo ndiyo yanawaongoza.

Malengo wanayoweka matajiri siyo ya kubahatisha, bali ni yanayoeleweka vizuri. Malengo yanakuwa SMART, yaani Mahususi (Specific), Yanayopimika (Measurable), Yanayofikika (Attainable), Yanayoendana (Related) na yenye Ukomo wa Muda (Timely).

Kuweka malengo ambayo hayana mchanganuo huo hayawi malengo, bali kujifurahisha tu.

Kwenye kuweka malengo ya kifedha, unapaswa kuyaweka kwa hatua hizi saba;

1. Kuweka akiba ya dharura ambayo ni kuanzia milioni moja na kuendelea.

2. Kulipa madeni yote madogo madogo uliyonayo, isipokuwa madeni makubwa na yeye riba ndogo.

3. Kuwa na akiba ya kuweza kuendesha maisha yako kwa miezi 6 mpaka 12 hata kama huna kipato kabisa.

4. Kuwekeza angalau asilimia 15 ya kipato chako kwa ajili ya baadaye.

5. Kuweka akiba ya mipango mikubwa ya baadaye kama manunuzi makubwa na elimu ya watoto.

6. Kulipa madeni makubwa uliyonayo kwa muda mfupi kuliko ilivyopangwa. Mfano deni la nyumba la miaka zaidi ya 10, lipa chini ya miaka 10.

7. Jenga utajiri na wasaidie wenye uhitaji.

Hatua za kuchukua;

Weka malengo yako ya kifedha kwa kufuata hatua saba ulizojifunza hapo juu. Angalia ni wapi hujafika kisha weka lengo la kuanzia hatua hiyo kwenda mbele. Kama huna akiba yoyote ya dharura, anza na hilo kama lengo. Ukikamilisha nenda hatua nyingine na endelea hivyo.

Kwa kuamua kwamba unataka kujenga utajiri na ukaweka malengo ambayo utayafanyia kazi kwa muda mrefu bila kuacha, unajiweka kwenye nafasi ya kujenga utajiri mkubwa na kwa uhakika.

Hapa tumejifunza sifa mbili kati ya sita walizonazo matajiri na zinawatofautisha na masikini. Karibu upate UCHAMBUZI KAMILI wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRES kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRE ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.