Tupo kwenye zama ambazo kadiri siku zinavyokwenda mambo yanazidi kuwa mengi na muda
unazidi kuwa mchache.

Kwenye mambo hayo hayo mengi na muda mchache, kuna watu wanauza na wanaoshindwa kuuza zaidi.

Unaweza kujiuliza wanaouza zaidi wanatumia mbinu ipi?

Wauzaji hawa huzingatia vipaumbele wanavyoweka, bila kuruhusu sababu yoyote.

Vipaumbele kwa lugha rahisi ni kipi kianze kufanyika na kipi kusubiri kufanyika.

Kama muuzaji bora kuwahi kutokea, ili ufanikiwe kuweka vizuri vipaumbele na kuona matokeo yake kuna kanuni ya A, B, C, D na E unapaswa kuifuata kama nilivyoelezea hapa chini;

A. Muhimu na haraka.
Ni majukumu yenye matokeo makubwa ukiyafanya na yenye madhara makubwa usipoyafanya.

Mfano, mteja kulipia pesa. Sio jambo la kusubiri, ni muhimu na haraka, maana pesa ni moyo wa biashara.

B. Muhimu, lakini sio haraka.
Haya ni majukumu yenye matokeo ya kawaida. Inaweza kuwa kazi ya ziada katika maisha yetu.

Mfano, kuchati na marafiki, kuingia kwenye mitandao.

Majukumu B yasifanyike kama  majukumu A hayajamalizika.

C. Haraka, lakini sio muhimu.
Haya majukumu yasiyo na matokeo yoyote katika utendaji wako. Mfano, kuwapigia simu marafiki, kutazama habari au mpira wakati wa kazi.

D. Sio haraka, wala muhimu.
Haya ni majukumu unayoweza kuwapa watu wengine wafanye kwa niaba yako.

Mfano, umemkamilisha mteja na kuna nafasi ya kutuma kwa gari tuma. Fanya mambo mengine wasiliana na mteja baadaye kujua kama amepokea mzigo wake.

E. Eliminate (Acha )
Haya ni majukumu ambayo hupaswi kuyafanya wakati wa kazi. Unaweza kuyafuta kabisa na usipate tatizo lolote.

Mfano, kwenda sehemu ambazo hazikusogezi karibu na kuuza au kukaa kijiweni.

Namna nzuri kutumia sheria hii ni kwamba, huwezi kufanya jukumu B kabla ya A, C kabla ya B, D kabla ya C na E kabla ya D.

Hivyo, fanya jambo moja likiisha nenda katika jambo lingine.

Epuka kujipa sababu yoyote ile, katika utendaji wako. Kama jambo linapaswa kufanywa na wewe, lifanye usiliache.

Ukitaka kuliacha jiulize kwanini ulianza kufanya jambo hilo. Hii itakusaidia kujipa hamasa kulifanya.

Hatua za kuchukua leo; Weka vipaumbele, kisha fanyia kazi. Usiangalie washindani wanaendeshaje biashara zao, jali vipaumbele, malengo na mahitaji ya biashara yako.

SOMA; Ongeza Ufanisi Katika Huduma Kutumia Kanuni Ya 5S

Nashukuru kwa kuwa pamoja nami, naamini unaenda kuchukua hatua sasa ili upate matokeo makubwa.

Wako Wa Daima

Lackius Robert

Mkufunzi Wa Mauzo na Mwandishi

0767702659/ mkufunzi@mauzo.tz

Karibu tujifunze zaidi.