Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Hii ni programu maalumu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa vitendo ili kujenga utajiri na kufikia uhuru wa kifedha.

Kwenye somo lililopita tulijifunza jinsi ya kukokotoa kiasi ambacho mtu unapaswa kuwekeza ili kufikia uhuru wa kifedha. Katika kukokotoa kiasi hicho, tulizingatia umri ambao mtu unao sasa, umri unaotaka kuwa umefikia uhuru wa kifedha na gharama za maisha kwenye kipindi hicho.

Kwa kuzingatia taarifa hizo, majibu ya kiasi cha kuwekeza kwa wengi kimekuwa ni kikubwa kuliko walivyotegemea. Kwa wengi kiasi kimekuwa kikubwa mno kuliko ambavyo wanaweza kumudu kwa sasa.

Sababu zilizopelekea kiasi cha kuwekeza kila mwezi kuwa kikubwa ni gharama kubwa za maisha katika kipindi hicho kijacho ambazo watu wameweka na muda mfupi wa kufikia uhuru wa kifedha. Kadiri gharama zinavyokuwa kubwa na muda kuwa mfupi, ndivyo kiasi cha kuwekeza kinavyohitajika kikubwa.

Tuangalie mifano mitatu ili kuelewa vizuri;

Mfano wa kwanza ni makadirio ya gharama za maisha ya Tsh milioni 5 na muda wa kufikia kuwa miaka 10, kiasi cha kuwekeza kinachohitajika kila mwezi kinakuwa ni Tsh milioni 11.

Mfano wa pili ni makadirio ya gharama za maisha ya Tsh milioni 2 na muda wa kufikia kuwa miaka 20, kiasi cha kuwekeza kinachohitajika kila mwezi kinakuwa ni Tsh milioni moja na laki 9. Hapa kiasi kimepungua na muda kuongezeka.

Mfano wa tatu ni makadirio ya gharama za maisha ya Tsh milioni 5 na muda wa kufikia kuwa miaka 40, kiasi cha kuwekeza kinachohitajika kila mwezi kinakuwa Tsh milioni 1 na laki 3.

Angalia mfano wa kwanza na wa tatu, kiasi cha kufikia ni kile kile, ambacho ni milioni 5 kwa mwezi, lakini muda ni tofauti, kwa miaka 10 mtu atahitajika kuwekeza milioni 11, wakati kwa miaka 40 mtu anatakiwa kuwekeza milioni moja na kidogo. Unaona jinsi muda ulivyo na nguvu hapo.

SOMA; Ngazi Ya Juu Ya Usimamizi Wa Kujenga Utajiri; Staafu Na Uhuru Wa Kifedha.

TUNACHUKUA HATUA GANI ILI KUENDELEA NA LENGO LA KUFIKIA UHURU WA KIFEDHA?

Rafiki, lengo la kila mmoja wetu kufikia uhuru wa kifedha haliwezi kuachwa au kuwekwa pembeni sasa kwa sababu majibu tuliyopata ni makubwa kuliko uwezo wetu.

Ni lazima tuchukue hatua sasa ili kuweza kufikia lengo la uhuru wa kifedha kama ambavyo tunataka. Kujiambia tusubiri mpaka tuweze kumudu, haitafanya kazi. Maana kadiri muda unavyokwenda, gharama za maisha zinapanda.

Hivyo wakati bora kuanza kufanyia kazi lengo la uhuru wa kifedha ni sasa na siyo wakati mwingine wowote.

Kwa kuwa tumeona sababu za kiasi cha kuwekeza kuwa kubwa ni MUDA na GHARAMA za maisha, hayo ndiyo maeneo mawili ya kufanyia kazi.

KUFANYIA KAZI MUDA.

Tukianza na kufanyia kazi muda, hapa muda unapaswa kuongezwa sana ili kiasi kinachohitajika kuwekwa kila mwezi kiweze kupungua. Kadiri muda unavyokuwa mkubwa, ndivyo kiwango kinavyopungua.

Lakini muda una ukomo, kwa wale ambao umri umeshaenda, hawana uwezo wa kupata muda zaidi. Muda unaweza kufanyiwa kazi vizuri na walio na umri usizidi miaka 30. Hawa wanaweza kuwa na miaka 30 na zaidi ya kuwa na uzalishaji mkubwa na hivyo kuwekeza kwa ukubwa.

Kwa ambao miaka ya uzalishaji mkubwa imebaki chini ya 20, yaani wenye miaka 40 na kuendelea, muda unaweza usiwe sehemu nzuri ya kuongeza.

KUFANYIA KAZI GHARAMA.

Kufanyia kazi gharama za maisha kwa kipindi unachopanga kuwa umefikia uhuru wa kifedha ni kuzipunguza sana. Kwa kupunguza sana gharama za maisha, inafanya lengo kuwa dogo na hivyo kiasi cha kuwekwa kila mwezi kupungua pia.

Kanuni rahisi ya kufanyia kazi gharama ni kuchagua kuishi kwa nusu ya kipato unachoingiza sasa na kuwekeza nusu. Kama ukiweza hilo, muda wa kuwekeza ili ufikie uhuru wa kifedha, unakuwa kati ya miaka 10 mpaka 15, hautazidi hapo.

Iko hivi, unapopunguza gharama za maisha yako sasa, unaongeza kiasi cha kuwekeza. Lakini wakati huo huo, kiasi unachohitaji ili ufikie uhuru wa kifedha, kwa kutumia unachoishi nacho sasa kinakuwa ni kidogo.

Hapo ndipo pa kuanzia kwenye kufanyia kazi gharama, punguza sana gharama za maisha yako ya sasa ili uishi kwenye nusu ya kipato chako na nusu uiwekeze. Kisha ndani ya miaka 10 mpaka 15 utakuwa umefikia uhuru wa kifedha.

JE NITAISHI DUNI MAISHA YANGU YOTE?

Kitu ambacho utakuwa umeona hapo ni kwamba kupunguza sana gharama za maisha yako, kutafanya uishi maisha ambayo unaweza kuona ni duni. Kwa sababu kuna matumizi mengi ambayo utalazimika kuachana nayo ili ufikie lengo la uhuru wa kifedha.

Ambacho watu wanakuwa na wasiwasi wao ni kama wataenda na maisha hayo duni kwa kipindi chote kilichosalia cha maisha yao. Jibu ni siyo kweli, kwa sababu kuna mambo mawili yanayoweza kurudisha maisha kuwa juu.

Jambo la kwanza ni kuendelea kuongeza kipato chako wakati wote ili ile nusu unayoendesha nayo maisha iendelee kukua na kuyapa maisha yako hadhi unayopata. Kama kipato chako ni milioni na unatumia laki tano na laki tano nyingine unawekeza, ukikikuza na kufika milioni 2, milioni 1 unatumia na milioni 1 unawekeza. Hakuna wa kukuzuia kwenye hilo ila wewe mwenyewe.

Jambo la pili ni ukishafikia uhuru wa kifedha na kuacha uwekezaji uliofanya ukue kwa miaka mingine 10 bila kuugusa, utakuwezesha kuendesha maisha yako kwa gharama ya juu zaidi. Yaani kwa kuishi nusu ya kipato na kuwekeza nusu, baada ya miaka 15 utakuwa umefikia uhuru wa kifedha. Hapo hata ukiamua kurudi kwenye kuishi kwenye kipato chako kizima bila kuwekeza nusu, miaka 10 baadaye uwekezaji uliofanya utakuwa umekua kiasi cha kukuwezesha kuendelea kuishi kwa kiwango hicho bila kupunguza. Hili linahitaji muda, lakini linawezekana.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Kwa majibu ya awali ya kiasi cha kuwekeza ili kufikia uhuru wa kifedha, je kiasi ulichopata unaweza kukiwekeza mara moja kuanzia sasa?

2. Ili uanze kufanyia kazi lengo la kufikia uhuru wa kifedha sasa, unaweza kuanza kufanyia kazi njia ipi kati ya MUDA na GHARAMA?

3. Je kwa kipato unachoingiza sasa, ukilazimika kuishi kwa nusu yake tu, maisha yako yataweza kuendaje? Vitu gani itabidi uviache? Je unaweza kuanza mara moja?

4. Karibu kwa maswali, maoni na mapendekezo kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.