Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Kwa kuwa lengo kuu la biashara ni kutengeneza wateja na wateja wa biashara wanapatikana maeneo mbalimbali, biashara inapaswa kutumia kila fursa inayoweza kuwafikia watu kuhakikisha inawafikia.

Hilo linaanza kwa kujua ni wapi wateja wa biashara huwa wanatumia muda wao wa siku nzima. Lengo ni kuhakikisha wanapokuwa kwenye maeneo hayo, wanajua kuhusu biashara na kushawishika kununua.

Moja ya maeneo ambayo watu huwa wanatumia muda wao wa siku ni kwenye kusafiri, kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Kila mtu huwa anafanya zoezi hili la kusafiri, iwe ni karibu au mbali.

Kwenye kusafiri pia, watu huwa wanatumia vyombo mbalimbali, kuanzia miguu ya mtu mwenyewe, vyombo vya miguu miwili, miguu mitatu, miguu minne, vya zaidi ya miguu minne, vya kuelea na vya kupaa. Hizo zote ni njia ambazo watu wamekuwa wanatumia kutoka eneo moja kwenda jingine.

Usafiri unatoa fursa kwa biashara kujitangaza na kuwafikia wateja wengi zaidi. Na hilo linafanyika kwa kuweka matangazo kwenye vyombo vya usafiri ili walengwa waweze kuyaona na waijue biashara pamoja na kushawishika kununua.

Kwenye kutumia vyombo vya usafiri kutangaza na kuwafikia wateja, kuna pande mbili za kuangalia; matangazo na vyombo vya usafiri.

Mambo ya kuzingatia kwenye matumizi ya vyombo vya usafiri.

Ili kuweza kuwafikia wateja wengi kwa kutumia vyombo vya usafiri, mambo haya yanapaswa kuzingatiwa kwenye kuchagua vyombo vya habari na kuweka matangazo kwa usahihi.

1. Kwa vyombo binafsi vya usafiri, matangazo yanapaswa kuwa nje ya chombo cha usafiri. Inaweza kuwa chombo kizima kuwa na matangazo au sehemu tu kuwa na matangazo. Kama chombo ni mali ya biashara, kinapaswa kuwa na matangazo kote, kwa sababu hakuna gharama kubwa ya kulipa. (Isipokuwa kuna kodi zinaweza kutozwa na mamlaka ya kodi au halmashauri kwa aina hii ya matangazo).

2. Kwa vyombo vya usafiri vya umma, matangazo yanapaswa kuwa nje ya chombo kwenye maeneo ambayo yanaonekana vizuri na pia ndani ya vyombo kwa sababu watu wanakaa ndani ya vyombo hivyo kwa muda mwingi.

3. Matangazo yanayowekwa ndani ya vyombo vya usafiri vya umma, yanaweza kuwa ya picha, sauti na hata video. Vyombo vingi vina mifumo ya sauti na video, hivyo matangazo yanaweza kuonyeshwa kwa njia zote na yakawafikia watu kwa uhakika zaidi. Kwa mfano mabasi ya mikoani ambayo yanasafiri kwa muda mrefu na yana TV ambazo abiria wanaangalia, tangazo linapotokea kwenye TV hizo, mara kwa mara kwenye safari, watu wanaliona na kuelewa zaidi.

4. Kuweka vipeperushi ndani ya vyombo vya usafiri, hasa mbele ya viti vya watu ni njia nyingine ya kuwafikia wateja kwa kutumia vyombo hivyo.

5. Matangazo kuwa sehemu ya vitu vya vyombo hivyo vya usafiri. Mfano matangazo kuwa kwenye tiketi ambazo abiria wanapewa au kuwa kwenye stika ambazo zinaweka vitu mbalimbali kwenye chombo husika cha usafiri.

6. Kuongea na watu moja kwa moja kwenye vyombo vya habari, hasa vinavyokuwa na watu wengi na safari ndefu. Njia hii imekuwa inatumiwa sana na wauzaji wa dawa za asili na virutubisho lishe, japo pia inafaa kwa biashara nyingine. (Njia hii imeanza kukatazwa kisheria kwa kuonekana ni usumbufu kwa abiria).

Kwa kuzingatia hayo kwenye upande wa vyombo vya habari, vinaweza kutumika vizuri kuwafikia watu wengi, ambao wanatumia vyombo hivyo kila siku na hata wale ambao wanakuwa barabarani na kuona matangazo yaliyo nje ya vyombo hivyo vya usafiri.

SOMA; Kufikia Wateja Wengi Kwa Kutumia Matangazo Ya Kuchapa.

Mambo ya kuzingatia kwenye matangazo ya kuweka kwenye vyombo vya usafiri.

Ili matangazo yanayowekwa kwenye vyombo vya usafiri yawafikie watu wengi na kuwashawishi kuchukua hatua ya kuja au kuwasiliana na biashara, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa.

1. Kwa matangazo ya picha, yanapaswa kuwa na picha yenye mvuto, maandishi makubwa yanayosomeka kwa mbali na mawasiliano yanayoonekana kirahisi. Matangazo, hasa ya nje ya vyombo vya usafiri huwa hayaonekani kwa muda mrefu, hivyo yanapaswa kunasa umakini wa mteja kwa picha inayovutia, maelezo yanayoshawishi na mawasiliano ya kuchukua hatua.

2. Matangazo ya sauti na video yanapaswa kuwa ya kujirudia rudia ili kunasa umakini wa watu na hata kueleweka. Tangazo kusikika au kuonekana mara moja tu haliwezi kuwa na ufanisi. Kwani watu huwa hawana utulivu mzuri wanapokuwa safarini. Lakini tangazo linapojirudia rudia, ndiyo linawaingia watu kwa kulielewa na kuweza kuchukua hatua.

3. Matangazo ya mauzo ya moja kwa moja kwenye vyombo vya usafiri yanapaswa kuwa na ofa ambayo mteja hawezi kuipata mahali pengine na hivyo kushawishika kuchukua hatua mara moja. Ofa inapaswa kuelezwa wazi ili watu waone wananufaika kwa kununua mara moja badala ya kusubiri.

Zingatia hayo kwenye kuandaa na kuweka matangazo kwenye vyombo vya habari ili kuwafikia wateja wengi na kuwashawishi kuja kwenye biashara.

Njia ya kutumia vyombo vya habari kuwafikia wateja wengi inafanya kazi vizuri kwa sababu watu wanakuwa kwenye vyombo hivyo kwa muda mrefu, hasa kwa mabasi ya safari ndefu. Angalia fursa ya biashara yako kuwa na matangazo kwenye vyombo vya usafiri kulingana na wateja unaowalenga na kuifanyia kazi ili kufikia wateja wengi zaidi na kuwashawishi kununua.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.