Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wanaposikia soko la hisa, huwa wanadhani ni kitu kikubwa na kigumu sana ambacho hakiwahusu wala hawawezi kukielewa.

Lakini huo siyo ukweli, soko la hisa ni kitu rahisi kueleweka na kutumika na kila mtu kwenye kujenga utajiri na uhuru wa kifedha.

Mwandishi J L Collins kwenye kitabu chake kinachoitwa THE SIMPLE PATH TO WEALTH ameshirikisha jinsi ambavyo soko la hisa ndiyo nyenzo muhimu ya kujenga utajiri. Karibu tujifunze hilo hapa na hatua za kuchukua ili kulitumia soko la hisa vizuri.

Karibu kwenye masomo haya ya kutoka kwenye kitabu cha THE SIMPLE PATH TO WEALTH ili ujifunze na kuchukua hatua kujiimarisha kifedha. Kupata mfululizo wa masomo yote ya kitabu hicho, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Mambo Muhimu Ya Kujua Kuhusu Soko La Hisa.

Watu wengi wamekuwa wanakwama kunufaika na soko la hisa kwa sababu kuna mambo muhimu wanakuwa hawayajui. Hapa kuna mambo muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuyajua kuhusu soko la hisa ili kunufaika nalo.

1. Anguko la soko la hisa ni kitu cha kutegemewa. Soko la hisa limepitia maanguko mbalimbali huko nyuma na litapitia maanguko mengine siku zijazo.

2. Soko huwa linapanda baada ya anguko. Hii ni uhakika na mara zote. Soko huwa halianguki na kubaki chini, bali huwa linapanda baada ya muda. Na kama itatokea soko la hisa lianguke na lisirudi tena, uchumi mzima utakuwa umeanguka, hakuna kitakachobaki salama.

3. Soko mara zote huwa linakua. Kwa muda mrefu, thamani ya soko la hisa huwa inakua. Kwa muda mfupi litaonyesha kupanda na kushuka, lakini kwa muda mrefu kunakuwa na ukuaji mzuri.

4. Soko la hisa ndiyo uwekezaji unaofanya vizuri sana kuliko uwekezaji mwingine wowote. Ukilinganisha mtaji unaowekezwa, muda na majukumu ya mtu kwenye uwekezaji, soko la hisa ni bora.

5. Miaka 10, 20, 30, 40, na 50 kutakuwa na maanguko mengi ya soko la hisa kama ilivyokuwa huko nyuma. Hakuna anayeweza kutabiri kwa usahihi ni lini anguko litatokea, lakini linatokea.

6. Unapaswa kuwa imara wakati wa anguko la soko, ili uwe tulivu na upuuze kelele za wale wanaokuambia uuze uwekeaji wako. Ukiweza kuendelea kuwekeza pale soko linapoanguka, utajenga uwekezaji mkubwa zaidi.

7. Ili uweze kuwa imara, unapaswa kujua kihisia kabisa kwamba nyakati ngumu zitakuumiza sana. Unachopaswa ni kuvumilia na hilo litapita.

8. Wakati wa anguko la soko ndiyo wakati mzuri wa kununua uwekezaji, maana unaupata kwa bei rahisi sana.

Muhimu zaidi ni kuwa imara nyakati zote na kutotaharuki kwa sababu lolote linalotokea siyo mwisho wa dunia.

SOMA; #NjiaYaUtajiri; Pata Pesa Ya ‘Kafie Mbali’ Na Fikiri Sahihi Kifedha.

Kwa Nini Watu Wanapoteza Pesa Kwenye Soko La Hisa.

Pamoja na soko la hisa kuwa nyenzo nzuri ya kila mtu kuweza kutumia kujenga utajiri mkubwa, bado watu wengi wamekuwa wanapoteza fedha kwenye soko la hisa. Zipo sababu ambazo zimekuwa zinapelekea hilo. Na baadhi ni kama ifuatavyo;

1. Wanafikiri wanaweza kulivizia soko, kwamba watanunua hisa zikiwa bei chini na kuuza zikiwa bei ya juu ili wapate faida. Ni rahisi kinadharia, lakini kwenye uhalisia ni ngumu sana, wengi hawawezi.

2. Wanaamini wanaweza kuchagua hisa moja moja kwa ubora. Kwa mwekezaji wa kawaida kuwekeza kwenye hisa moja moja ni vigumu sana kuweza kuchagua kwa ubora. Hiyo ni kwa sababu soko la hisa linakuwa na makampuni mengi na kujua ipi bora siyo rahisi. Hivyo njia sahihi ni kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja inayowekeza kwenye soko la hisa badala ya hisa moja moja.

3. Wanaamini wanaweza kuchagua mfuko wa pamoja wenye usimamizi bora. Kuna mifuko ya pamoja ya uwekezaji ambayo huwa inajaribu kulivizia soko, na hiyo huishia kupata hasara. Kuwekeza kwa kutumia mifuko ya aina hiyo ni kupata hasara. Ni vyema kuchagua mifuko inayowekeza kwenye soko zima na yenye gharama kidogo.

4. Wanahangaika na povu badala ya bia yenyewe. Mfumo mzima wa uwekezaji ni sawa na kumimina bia kwenye glasi, ukimimina haraka, povu linakuwa juu na bia inakuwa chini. Unachotumia siyo povu, bali bia yenyewe. Kwenye uwekezaji, bia ni thamani ya kampuni husika na povu ni kupanda na kushuka kwa bei ya hisa. Wewe usihangaike sana na mwenendo wa soko, bali angalia thamani ya kampuni husika, kama ipo vizuri, wekeza.

Kwenye somo hili tumepata uelewa wa msingi wa soko la hasa kupanda na kushuka na kuepuka kupoteza.

Kupata mfululizo wa masomo yote ya kitabu THE SIMPLE PATH TO WEALTH, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu cha THE SIMPLE PATH TO WEALTH ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.