3438; Rahisi na ngumu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Sehemu kubwa ya mafunzo na ushauri wa mafanikio imejikita kwenye upande chanya wa kuwatia watu moyo na kuwaonyesha kwamba inawezekana.
Lengo likiwa ni zuri kabisa, kuwafanya watu wajisukume zaidi ili kufanya makubwa.

Lakini uhalisia umekuwa ni tofauti kabisa na kile kilichotarajiwa.
Licha ya watu kupewa moyo sana na kuonyeshwa jinsi ilivyo rahisi na kuwezekana, bado watu wamekuwa wanashindwa na kuacha.

Kumbe basi hilo la mambo kuelezwa kwa uchanya na urahisi imekuwa inachangia sana kwa watu kukata tamaa haraka.

Pale mtu anapoambiwa kwamba kitu ni rahisi, lakini kwenye ufanyaji wake akakutana na ugumu ambao unafanya kitu kisiwe rahisi kwake, anaacha kufanya.
Anaacha kwa sababu anaona kama kitu ni rahisi kama kinavyoelekezwa, ila kwake kinakuwa changamoto, basi yeye ndiye ambaye hawezi.

Kwa upande mwingine, mtu anapoambiwa kitu anachokwenda kufanyia kazi ni kigumu na kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa, anadumu kwenye kufanya.
Anadumu kwa sababu aliingia akijua kabisa kwamba kitu siyo rahisi, hivyo kujiandaa kuweka juhudi kubwa zaidi ili kukipata.
Anapokutana na ugumu anajua ni kitu ambacho alitarajia na hivyo kuendelea bila ya kukata tamaa.

Kutokana na haya tuliyojifunza hapa, hatupaswi kuangalia upande rahisi wa mambo peke yake.
Bali tunapaswa kuangalia upande mgumu wa kitu ili unapoingia, uwe umejipanga vyema kabisa.

Na pia kwa watu wa karibu na unaoshirikiana nao, usiwaonyeshe tu urahisi wa kitu, pali pia waonyeshe ugumu wake.
Wafanye wapate hasira ya kutaka kuvunja magumu yote ili kuleta matokeo ya tofauti.
Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kuwapata wale ambao wamejitoa kweli kufanikiwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr. Makirita Amani
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe