Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye sehemu ya kwanza ya somo la kutumia soko la hisa kujenga utajiri mkubwa, tuliweza kupata uelewa wa soko la hisa. Tuliona tabia ya soko la hisa kupanda na kushuka mara kwa mara na kama mtu unataka kufanikiwa kwenye uwekezaji unapaswa kuwa imara na kuhimili mitikisiko hiyo ya soko.

Mwandishi J L Collins kwenye kitabu chake kinachoitwa THE SIMPLE PATH TO WEALTH ameshirikisha njia ya uhakika ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha na maisha ya uhuru na utajiri.

Karibu kwenye masomo haya ya kutoka kwenye kitabu cha THE SIMPLE PATH TO WEALTH ili ujifunze na kuchukua hatua kujiimarisha kifedha. Kupata mfululizo wa masomo yote ya kitabu hicho, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kwenye sehemu hii ya pili tunakwenda kujifunza mambo ya kuzingatia kwenye kuwekeza kwenye soko la hisa na njia za kuwekeza na kunufaika na soko hilo la hisa. Karibu ujifunze na uende kuchukua hatua ili kujenga utajiri kwa uhakika.

Mambo Ya Kuzingatia Kwenye Uwekezaji Wa Soko La Hisa.

Kwenye kufanya maamuzi ya kuwekeza kwenye soko la hisa, unapaswa kuzingatia mambo makuu matatu;

Moja ni hatua uliyopo kwenye uwekezaji.

Uwekezaji una hatua mbili;

Ya kwanza ni hatua ya kukusanya uwekezaji. Huu ni wakati ambapo mtu bado unafanya shughuli za kukuingizia kipato na unawekeza. Katika hatua hii unapaswa kuingiza kipato kikubwa na kuwekeza kwa ukubwa.

Hatua ya pili ni kutunza uwekezaji. Huu ni wakati ambapo hufanyi tena shughuli za kukuingizia kipato na hivyo unaishi kwa kutegemea uwekezaji ambao ulishafanya. Hapa unapaswa kuwa na kiwango sahihi cha kutoa ili uweze kwenda na uwekezaji huo kwa muda mrefu.

Mbili ni uwezo wako wa kuhimili hatari.

Watu tunatofautiana kwenye uwezo wa kuhimili hatari. Kuna watu ambao hatari kidogo tu inatosha kuwasumbua. Na kuna ambao wanaweza kuhimili hatari kubwa na wakawa tulivu.

Kama huwezi kuhimili hatari kubwa, fanya uwekezaji ambao hatari yake ni ndogo. Na kama unaweza kuhimili hatari kubwa, huku umri wako ukiwa bado unaruhusu kufanya kazi, unaweza kuchukua hatari kubwa.

Lakini kwa ujumla unapaswa kutambua kila uwekezaji una hatari. Hakuna uwekezaji wowote ambao hauna hatari kabisa.

Tatu ni kipindi cha uwekezaji.

Uwekezaji unaweza kufanyika kwa vipindi vya aina mbili.

Moja ni uwekezaji wa muda mfupi, huu ni wa chini ya miaka kumi na ni uwekezaji ambao haupati ukuaji mkubwa.

Mbili ni uwekezaji wa muda mrefu, huu ni wa zaidi ya miaka kumi na huwa unapata ukuaji mkubwa.

Wewe unapaswa kuwa na uwekezaji wa muda mrefu, kama bado hujafikia umri wa kustaafu.

Zingatia hayo matatu ili uweze kufanya uwekezaji sahihi kwako.

SOMA; #NjiaYaUtajiri; Tumia Soko La Hisa Kujenga Utajiri Mkubwa – Sehemu I

Zana Kuu Tatu Za Uwekezaji.

Kwenye kuwekeza huwa kuna aina nyingi sana za uwekezaji. Lakini mwandishi kwenye kitabu hiki ameshirikisha zana kuu tatu ambazo mtu yeyote akizitumia atanufaika sana na uwekezaji.

Zana ya kwanza ni HISA.

Uwekezaji kwenye hisa ndiyo nyenzo kuu ya kuwekeza na ambayo ina matokeo mazuri. Hapa huwekezi kwenye hisa moja kwa moja, bali kwenye mifuko ya pamoja inayowekeza kwenye soko la hisa.

Zana ya pili ni HATIFUNGANI.

Uwekezaji kwenye hatifungani huwa una hatari ndogo kuliko kwenye hisa, japo faida yake pia huwa ni ndogo. Hivyo huu unakuwa uwekezaji mzuri kwa wale ambao hawawezi kustahimili hatari kubwa. Uwekezaji huu wa hatifungani nao pia utaufanya kupitia mifuko ya pamoja na siyo hatifungani moja moja.

Zana ya tatu ni FEDHA.

Kuwa na fedha, iwe ni taslimu au kwenye akaunti maalumu za benki au uwekezaji ni zana nyingine ya uwekezaji. Lengo la kuwa na uwekezaji ambao ni fedha ni kuweza kukabiliana na dharura mbalimbali ambazo mtu unakutana nazo. Kwa kuweza kuwa na uwekezaji ambao ni rahisi kuwa fedha, unazuia kuvuruga uwekezaji wako mkuu. Fedha unapaswa kuwa nayo kiasi kwa sababu huwa inashuka thamani kutokana na mfumuko wa bei. Sehemu kubwa ya utajiri wako inapaswa kuwa kwenye uwekezaji wa hisa na hatifungani.

Kwa kuzingatia haya uliyojifunza hapa, unaweza kupangilia na kufanya vizuri uwekezaji na kuweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako. Chukua hatua kwenye haya uliyojifunza ili uweze kupata matokeo ya tofuati kwenye maisha yako.

Kupata mfululizo wa masomo yote ya kitabu THE SIMPLE PATH TO WEALTH, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu cha THE SIMPLE PATH TO WEALTH ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.