3439; Umeshaweza magumu zaidi

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Mambo ambayo umeshajifunza na kuweza kufanya kwenye maisha yako ni magumu kuliko yale ambayo unayakwepa sasa.

Hebu fikiria wakati unapelekwa shuleni, hujui kusoma, wala kuandika au kuhesabu.
Walimu walihangaika na wewe sana mpaka ukaweza kusoma, kuandika na kuhesabu.

Leo hii unafanya hayo kwa urahisi sana, lakini ukijaribu kukumbuka wakati unajifunza hayo, ilikuwa kazi kubwa.

Hebu kumbuka wakati unafundishwa kuandika namba 8, au hesabu za kugawanya kwa njia ndefu.

Sasa unaweza kufanya hayo bila hata ya kufikiri mara mbili.

Tunachojua hayupo mtu alizaliwa akiwa anajua kusoma, kuandika wala kuhesabu.
Lakini karibu wote tunaweza kufanya hayo, kwa sababu tumejifunza na kufanyia kazi.

Huwezi kumsikia mtu akisema yeye siyo wa kujua kusoma, kuandika wala kuhesabu.

Lakini inapokuja kwenye mambo mengine muhimu ya kujifunza kwenye maisha, kama fedha, mauzo na biashara, watu wanaanza kujiwekea ukomo.

Utawasikia watu wakisema wazi na kwa kujivunia kabisa kwamba hayo siyo mambo yao. Au hawapo vizuri kwenye hayo na kadhalika.

Wengi wanaona kujifunza mambo hayo ili waweze kuyafanya kwa usahihi ni vigumu na hawawezi.
Wakati kila wanachofanya kwenye maisha kwa sasa walijifunza huko nyuma.

Kama ambavyo ulijifunza kusoma, kuandika na kuhesabu, ndivyo pia unavyoweza kujifunza;

1. Kujenga biashara yenye mafanikio makubwa kwa kuanzia chini kabisa.

2. Kufanya mauzo makubwa na kuongeza kipato.

3. Kujenga utajiri na uhuru wa kifedha kwenye maisha yako.

4. Kuwa na afya bora na kuishi miaka mingi.

Hayo yote unaweza kujifunza vizuri kabisa hata kama hakuna unachojua.
Ushahidi ni ulishaweza kujifunza mengi magumu zaidi na ukaweza.
Hivyo hata hayo utayaweza kama utaweka juhudi sahihi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe