Habari njema Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Hii ni programu maalumu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa vitendo ili kujenga utajiri na kufikia uhuru wa kifedha.
Kwenye somo lililopita tulijifunza jinsi ya kufikia uhuru wa kifedha ndani ya miaka 15 kwa uwekezaji mdogo mdogo. Tuliona njia ya kufanya hivyo ni kuweza kuishi kwenye nusu ya kipato chako na kuwekeza nusu inayobakia.
Kwa kufanya hivyo unakuwa umetumia njia mbili ambazo zinakufikisha kwenye uhuru wa kifedha haraka. Moja unakuwa unaweka akiba kiasi kikubwa na hivyo ukiwekeza vizuri, ukuaji unakuwa mkubwa. Mbili unakuwa umefanya gharama zako za maisha kuwa chini sana na hivyo hutahitaji muda mrefu ili kufikia uhuru wa kifedha.

Mrejesho wa somo hilo ulikuwa ni mtu ueleze kama unaweza kuishi kwa nusu ya kipato chako cha sasa. Kulikuwa na majibu ya aina mbili, kwa wale ambao bado hawajawa na majukumu makubwa ya maisha walijibu wanaweza. Hao wanapaswa kuanza mara moja.
Upande wa pili wa mrejesho ulikuwa ni wa wale ambao tayari wana majukumu makubwa kwenye maisha yao, ambao walieleza wazi kwamba hawawezi kuishi kwa nusu ya kipato chao cha sasa.
Hilo linakuwa linaeleweka kabisa, kwamba kwa kuna majukumu ya maisha ambayo mtu hawezi kuyaacha. Mfano mahitaji ya msingi ya familia.
Lakini pia hupaswi kuahirisha zoezi la kujijengea uhuru wa kifedha kwa sababu ya majukumu makubwa ya maisha. Miaka 10 ijayo utakuwa bado una majukumu makubwa na hutakuwa umepiga hatua kwenye kufikia uhuru wa kifedha.
Hivyo licha ya kuwa na majukumu makubwa uliyonayo sasa, bado pia unapaswa kufanyia kazi mkakati wa kufikia uhuru wa kifedha. Na mkakati rahisi wa kila mtu kufanyia kazi ni wa kuwekeza nusu ya kipato ambacho mtu anaingiza, ili kati ya miaka 10 mpaka 15 uwe umefikia uhuru wa kifedha.
Najua bado inakushangaza kwamba kipato tumeshakubali hakitoshi kwa sababu ya majukumu makubwa, hapo tunafanyaje. Na hilo ndiyo somo letu la leo.
Kwa wote ambao mlikuwa na mrejesho kwamba majukumu ni makubwa na hamuwezi kuishi nusu ya kipato, hatua ya kuchukua ni KUKUZA KIPATO CHAKO MPAKA KUFIKIA HATUA YA KUWEZA KUISHI NUSU YA KIPATO HICHO.
Kwa maneno mengine rahisi ni kwamba, kwa sababu kipato ulichonacho sasa tayari kinafanya maisha yaweze kwenda, kikuze mara mbili. Yaani ingiza kipato mara mbili ya unavyoingiza sasa.
Kabla hujasema ni kiasi kikubwa sana na haiwezekani, nikuhakikishie bila ya shaka yoyote kwamba inawezekana kabisa. Ushahidi ni mwingi wa wengi ambao wameshaweza kutimiza hilo. Ni wewe uamini inawezekana na kuchukua hatua sahihi za kutekeleza hilo.
Katika kutekeleza mpango huu wa kukuza kipato mara mbili, tunaenda kuangalia pande mbili za walioajiriwa na wanaofanya biashara.
SOMA; Hatua Za Kujijengea Uhuru Wa Kifedha.
KUKUZA KIPATO MARA MBILI KWENYE AJIRA.
Kwa wale ambao njia kuu ya kuingiza kipato ni ajira, inawezekana kabisa kukuza kipato mara mbili. Lakini hilo halitakuwa ndani ya ajira ambayo mtu unafanya. Utaweza kufanya hilo kwa kuwa na njia nyingine ya kuingiza kipato nje ya ajira.
Kuna shughuli nyingi ambazo mtu unaweza kufanya ukiwa bado unaendelea na ajira yako na ukaingiza kipato cha ziada. Lakini shughuli nyingi zinachukua muda mrefu mpaka zilete matokeo na kipato chake kinakuwa kidogo.
Ipo njia moja ya kuweza kuingiza kipato kikubwa na ambayo haitachukua muda mrefu inayoweza kutumiwa na wale walioajiriwa. Njia hiyo ni kufanya kazi ya mauzo. Mauzo ni kazi inayolipa vizuri sana kama mtu ataweka juhudi kubwa kwenye kuifanya.
Hii ndiyo njia ninayowashauri wale wote walioajiriwa na wanataka kufikia uhuru wa kifedha ndani ya miaka 15. Hapa unachofanya ni kuchagua bidhaa au huduma ambayo tayari wewe mwenyewe unaitumia na unaikubali sana. Kisha kuongea na watengenezaji au wasambazaji wa bidhaa au huduma hiyo na kuwaambia unaweza kuuza kwa wingi na wakupe mpango wa kukulipa kwa kamisheni.
Ukishapata mpango huo, unaweka juhudi kubwa za kuwa vizuri kwenye kuuza na unakaa kwenye mchakato wa mauzo. Ukijipa muda wa kujifunza na kuwa bora kwenye mauzo na ukaweka juhudi kubwa, unaweza kufanya vizuri ndani ya muda mfupi.
Napendekeza njia hii kuliko nyingine kwa sababu mtu unahitaji kuanza kuingiza kipato mapema na siyo kusubiri kwa muda mrefu. Na kwa sababu tayari mtu una kipato cha ajira, kiasi chote unachopata kutoka kwenye mauzo unapeleka kwenye kuwekeza.
Njia ya mauzo ina fursa nyingi kwa sababu kila biashara inataka mauzo zaidi. Biashara nyingi zina changamoto ya mauzo, hivyo ukiwa mzuri kwenye kuuza, fursa ni nyingi sana.
Na uzuri unaanza kwa kuuza kitu ambacho tayari wewe mwenyewe unakitumia, hivyo unakielewa vizuri na kuwashawishi wengine haiwezi kuwa kazi ngumu kwako.
Ukishachagua kukuza kipato kwa mauzo, fanyia kazi hatua tano zilizopo kwenye kipengele cha kukuza kipato kwa biashara hapo chini.
KUKUZA KIPATO MARA MBILI KWENYE BIASHARA.
Kama unafanya biashara, uko kwenye eneo zuri sana la kukuza kipato chako mara mbili kwa kuanzia hapo hapo ulipo sasa. Huhitaji hata kubadili biashara yako, bali unapaswa kubadili juhudi unazoweka.
Ili kukuza kipato chako mara mbili kwenye biashara na kwa uhakika, kuna vitu vitano unavyopaswa kuvifanyia kazi kwa wakati mmoja;
Moja Ni Kufikia Wateja Wapya Wengi Zaidi.
Kikwazo chako kikuu cha mapato kwenye biashara ni kutokujulikana. Unaweza kuwa na bidhaa au huduma nzuri sana, lakini wengi ambao wangenufaika wakawa hawajui hata kama upo.
Unachopaswa kufanya hapa ni kuitangaza sana biashara yako kwa kila aina. Weka matangazo ya kila namna kwa njia mbalimbali, za bure na za kulipia, mitandaoni na mitaani na ana kwa ana au mawasiliano. Hakikisha kila wakati kuna watu wasioijua biashara yako wanaisikia.
Mbili Ni Kuwashawishi Kununua Kwa Mara Ya Kwanza.
Kwa wale ambao wanaisikia biashara yako kwa mara ya kwanza, hakikisha unapata njia ya kuweza kuwasiliana nao. Hapa unapaswa kuwa na mawasiliano na wale wote ambao wamesikia kuhusu biashara yako na wanakuwa na uhitaji, hata kama ni wa baadaye. Ni kupitia mawasiliano hayo ndiyo unaendelea kuwafuatilia ili kuwashawishi waweze kununua.
Manunuzi ya mara ya kwanza ya wateja ndiyo huwa magumu zaidi. Yanakutaka uwe na ufuatiliaji endelevu na wa mara kwa mara ndiyo watu washawishike kununua.
Kuwa na orodha ya wateja ambao bado hawajanunua na unawafuatilia na mara zote hakikisha unawafikia bila kuchoka. Ukifanya hivyo kila wakati, kuna ambao watakuwa wanashawishika na kununua. Hivyo unakuwa unapanda na kuvuna kama mkulima, au kupandisha na kushusha kama daladala.
Tatu Ni Kuwafanya Warudi Tena Kununua.
Wateja wote ambao walishawahi kununua kwako angalau mara moja, hakikisha wanarudi tena kununua. Hapo unapaswa kuwa na mawasiliano ya wateja wote ambao wameshanunua kwako na kuendelea kuwafuatilia mara kwa mara ili kuwashawishi warudi tena kununua.
Mteja akishanunua kwako, usikubali kumpoteza, mfuatilie na kumshawishi arudi tena kununua. Huwa ni rahisi zaidi kuwauzia wateja ambao walishanunua kuliko ambao hawajawahi kununua kabisa.
Nne Ni Kuwashawishi Wanunue Zaidi Ya Walivyopanga.
Wateja wanapokuja kununua kwenye biashara yako, hakikisha unawazuia vitu vya ziada kuliko walivyokuwa wamepanga kununua. Kwa kila mauzo unayoyafanya kwa wateja wako, wapendekezee vitu vingine vinavyoendana na mauzo hayo. Ukiwa na ushawishi mzuri, utaweza kuwafanya wateja wanunue zaidi ya walivyokuwa wamepanga.
Hakikisha kwa kila bidhaa na huduma unayouza, kuna ambazo zinaendana nayo ambapo kila mteja anaponunua anashauriwa kununua na cha ziada. Kama kila mteja ataambiwa kuhusu kununua cha ziada, hawatakubali wote, lakini pia hawatakataa wote.
Tano Ni Kuongeza Kiwango Cha Faida.
Pamoja na kufanya mauzo makubwa, kama kiwango cha faida ni kidogo, bado utabaki pale pale kwenye kipato kidogo. Kwenye biashara, kipato chako ni faida na siyo mauzo. Hivyo hakikisha unakuza kiwango cha faida.
Maeneo ya kufanyia kazi ili ukuze kiwango cha faida ni kudhibiti matumizi na kuuza vitu vyenye kiwango kizuri cha faida. Angalia pande zote mbili za matumizi na mauzo ya faida kubwa ili ubaki na kipato kizuri.
Mambo hayo matano yakifanyiwa kazi moja moja yana nguvu ya kuleta matokeo mazuri. Lakini miujiza huwa inakuja pale yanapofanyia kazi kwa pamoja. Hapo ndipo mauzo yanapokua zaidi ya mara mbili ndani ya muda mfupi.
Yote ni mambo yanayowekezana kwa kila anayeuza, iwe unafanya biashara pekee au umeajiriwa na ukaamua pia kufanya mauzo. Chukua hatua ili ukuze kipato chako kwa uhakika.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;
1. Je unaamini unaweza na upo tayari kujitoa kukuza kipato chako mara mbili?
2. Zipi shughuli zako kuu za kuingiza kipato kwa sasa?
3. Kama upo kwenye ajira pekee, chagua ni kitu gani unaona unaweza kukiuza vizuri na kukuza kipato chako mara mbili. Eleza kwa nini umechagua kitu hicho.
4. Shirikisha mkakati wako wa hatua tano za kukuza mauzo mara mbili kama ulivyojifunza kwenye somo hili?
5. Karibu kwa maswali, maoni na mapendekezo kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.