Mafanikio katika mauzo yanategemea sana uwezo wa kucheza na saikolojia za wateja, kuangalia mazingira, pamoja na matukio yanayojitokeza.
Wauzaji wenye mafanikio makubwa wanafuatilia kwa kina kila tukio linaoendelea kwenye mazingira yao na kutumia kama fursa ya kuuza.

Mojawapo ya eneo wanaloweka mtego na kunasa wateja wengi zaidi ni kuweka bei za msimu(pricing seasons)
Bei za msimu ni bei ambazo unaziweka kuendana na tukio fulani linalotokea katika kipindi husika.
Bei hizi huwa ni za muda mfupi, lakini zenye matokeo makubwa kimauzo. Hasa ukizipangilia vizuri.
Unapoweka bei hizi, maana yake ni kwamba, unakuwa na sababu ya kumshawishi mteja kulingana na tukio husika.
Ambapo unaweza kufanya kwa malengo ya kuuza bidhaa zilizokaa ndani kwa muda mrefu, kupata faida ndogo ndogo au kuuza bidhaa nyingi kwa wakati mmoja.
Maeneo unayoweza kutengeneza bei za msimu ni kama yafuatayo;
Moja; Sherehe za kitaifa
Kwa mfano hapa Tanzania unaangalia sherehe zinazosherekewa na watu wote, mfano Mei mosi, Sabasaba, Nyerere day, Karume day, Muungano, Uhuru na Nane nane.
Mbili; Sherehe za dini
Mfano Christmas, pasaka, idd elfitr.
Uzuri wa sikukuu hizi zinatokea katika vipindi tofauti, hali inayokufanya ujifanyie tathimini zaidi.
Tatu; Sikukuu ya kuzaliwa kwako
Hapa unatumia siku hii kutoa bei za ofa, punguzo la bei au kutoa zawadi.
Rejea mfano kwenye ZAWADI YA KOCHA kutoka kwa Kocha Dr Makirita Amani wakati wa kusherekea sikukuu ya kuzaliwa (mei 28).
Hivyo, unafanya maandalizi mapema kabla ya siku yenyewe, ili siku inapofika iwe rahisi kuwatangazia wateja bei hizo.
Nne; Sikukuu za kimataifa
Hapa unaagalia matukio yanayosherekewa dunia nzima mfano, Mwaka mpya au siku ya wanawake duniani na zingine.
Unapopangilia bei hizi waambie wateja wako nini watakosa, ikiwa hawataweza kununua kwa sababu ni bei za muda mfupi.
Msimu unapoisha au tukio kuisha bei zinarudi katika hali yake ya kawaida.
Uwepo wa bei za msimu unasaidia wateja kufuatilia biashara yako kwa kina kwa muda mrefu.
Pia, inawafanya wateja kuikumbuka biashara milele kwa sababu matukio haya yataendelea kuwepo maisha yote.
Hatua za kuchukua leo; Weka mpango vizuri matukio husika ndani ya mwaka mzima kisha angalia namna nzuri kuyatumia kukuza mauzo yako.
SOMA; Tumia Nguvu Ya Ofa Kuuza Bidhaa Zingine
Je, ni tukio lipi unatumia kuwashawishi wateja wako?
Wako Wa Daima
Lackius Robert
Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na mwandishi.
0767702659 / mkufunzi@mauzo.tz
Karibu tujifunze zaidi