Rafiki yangu mpendwa,
Kumekuwa na kasumba mbaya sana kwenye jamii zetu. Kasumba hiyo ni kwamba watu hawawezi kuishi bila kukopa.
Imekuwa ni hali ya kusikitisha sana jinsi ambavyo watu wameaminishwa na kuamini kuwa na madeni ndiyo njia ya maisha.
Kitu ambacho watu wengi wamekuwa hawaonyeshwi ni kwamba madeni ndiyo kaburi la utajiri. Hakuna mtu anayeweza kujenga utajiri kwa kutumia madeni.
Na hapa nazungumzia madeni binafsi, pale ambapo mtu anakopa fedha kwa ajili ya matumizi. Sizungumzii madeni ya biashara ambapo mtu anakopa fedha kwa ajili ya kwenda kuzalisha faida zaidi kwenye biashara.
Japo pia madeni ya biashara yanaweza kuwa mabaya kama hayatatumika vizuri kwenye kuzalisha faida.

Kwa sababu hapa tunazungumzia USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI, mjadala wetu utajikita kwenye madeni binafsi. Pale unapokopa fedha kwa ajili ya kula, sherehe, kulipa ada, kodi na gharama nyingine za maisha ambazo hazizalishi moja kwa moja.
Kama uko makini na fedha zako na unataka kufikia utajiri na uhuru wa kifedha, hupaswi kuwa kwenye madeni kabisa. Kama upo kwenye madeni, unapaswa kuondoka haraka sana. Yaani kabla hujafanya kingine chochote, unapaswa kuondoka kwenye madeni kwanza.
Kwa sababu hata uwekeze kiasi gani, huwezi kunufaika, kwa sababu riba ya madeni huwa ni kubwa kuliko marejesho ya uwekezaji. Chukua mfano umewekeza milioni 1 na kwa mwaka unapata riba ya asilimia 10, hivyo kwa mwaka unapata laki 1. Lakini wakati huo huo una deni la milioni moja na unalipa riba ya asilimia 18, hapo kwa mwaka unalipa laki 1 na elfu 80. Ukiangalia, unakuwa umepoteza elfu 80 kwenye kulipa riba. Hivyo ni bora milioni 1 ukaipeleka kulipa deni ili uache kupoteza fedha kwenye kulipa riba za madeni.
Ili kuondoka kwenye madeni kwa uhakika, fuata hatua hizi tano;
Moja; Jua Madeni Yote Uliyonayo.
Jumlisha madeni yote uliyonayo ili uweze kujua ni kiasi gani unachodaiwa. Kumbuka unataka kuondoka kwenye madeni yote kabisa, hivyo jumlisha yote bila kuacha hata moja.
Mbili; Weka Mpango Wa Kulipa.
Kwa madeni yote uliyonayo, pangilia jinsi utakavyolipa. Kuna njia mbili za kulipa, moja ni kulipa madeni yenye riba kubwa kwanza na mbili ni kulipa madeni madogo madogo kwanza. Chagua njia itakayokufaa, lakini nzuri ni kulipa yenye riba kubwa kwanza ili upunguze gharama.
Tatu; Omba Punguzo La Riba.
Ongea na wale wanaokudai na waombe wakupe punguzo la riba kwa kuwaahidi kulipa kwa wakati. Kwa kuwa wengi wanataka kulipwa, watakuwa tayari kukupa punguzo. Na kama watakataa kukupa punguzo la riba, basi punguza muda wa kulipa, unapolipa deni kwa muda mfupi, kiasi cha riba unacholipa kinapungua pia.
Nne; Jua Fedha Ya Kulipa Inakotoka.
Ukishaweka mpango wa kulipa madeni, unapaswa kujua fedha ya kulipa madeni hayo inatoka wapi. Kuna njia mbili hapa; moja ni kupunguza sana gharama na sehemu kubwa ya kipato kwenda kwenye kulipa madeni. Na mbili ni kuongeza kipato na kinachoongezeka kwenda kwenye kulipa madeni. Fanyia kazi njia zote mbili ili uondoke kwenye madeni yako haraka zaidi.
Tano; Usirudi Tena Kwenye Madeni.
Kuna watu huwa wanahamisha madeni, wanakopa sehemu moja kwenda kulipa sehemu nyingine, hivyo wanazidi kubaki kwenye madeni. Lakini pia wapo ambao wanayalipa madeni, lakini kwa sababu ya tabia mbaya za kifedha, wanajikuta wamerudi tena kwenye madeni. Wewe ukishatoka kwenye madeni, jizuie usirudi tena. Hivyo hakikisha matumizi yanakuwa chini ya kipato na unakuwa na akiba ya dharura ili lolote linapotokea usijikute unarudi tena kwenye madeni.
Fanyia kazi hatua hizo tano na utaweza kuondoka kwenye madeni yanayokuwa kikwazo kwako kujenga utajiri.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ujifunze kwa kina hatua hizo tano za kuondoka kwenye madeni na jinsi ya kuzitekeleza kwa uhakika.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.