Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa nakushirikisha mara kwa mara udhaifu mkubwa ambao watu wengi wanao kwenye eneo la USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI.
Wengi wana mazoea ya PATA PESA, TUMIA PESA. Ni mazoea hayo ndiyo yamekuwa yanapelekea mtu anafanya kazi au biashara kwa miaka mingi, anaingiza kipato lakini anazeeka akiwa masikini.
Ukweli ni kwamba kila mtu anayefanya shughuli yoyote ya kuingiza kipato, anayo fursa kubwa ya kujenga utajiri. Anachohitaji ni kuwa na mpango sahihi ambao anaufanyia kazi kwa msimamo bila kuacha ili kunufaika nao.
Mpango sahihi wa utajiri unaanza na mpango sahihi wa matumizi ya fedha. Kwa sababu bila ya mpango mzuri wa matumizi, fedha haiwezi kutumika kujenga utajiri. Mtu ataishia kutumia kipato chote anachoingiza na kusingizia hakitoshi.

Iko hivi rafiki, kipato hakijawahi kumtosha mtu yeyote. Kama unasubiri mpaka kipato kitosheleze ndiyo uanze mpango wa kujenga utajiri, kamwe hutaweza kupata utajiri.
Anza kwa kuweka mpango sahihi wa matumizi ya fedha zako ili ujenge utajiri huku ukiendelea na maisha yako.
Kwa kipato unachokuwa unaingiza, unapaswa kukigawa kwenye mafungu matano.
Moja; Matumizi (60%).
Matumizi ndiyo kundi kubwa linalochukua kipato. Ili mambo mengine yaweze kwenda, matumizi yako hayapaswi kuzidi asilimia 60 ya kipato. Kwa kudhibiti hilo ndiyo utaweza kubaki na fedha kwa ajili ya mambo mengine muhimu.
Matumizi yanahusisha mambo yote ya msingi unayopaswa kuyalipia ili maisha yako ya kila siku yaweze kwenda. Kila mtu ana matumizi ya msingi ambayo akiyazingatia kulingana na kipato chake anaweza kutumia kiasi hicho. Matumizi yasiyo muhimu ndiyo yamekuwa yanawasumbua zaidi watu.
Mbili; Akiba (10%).
Kwenye kila kipato unachoingiza, asilimia 10 inapaswa kwenda kwenye akiba maalumu unayokuwa unajiwekea. Akiba hiyo inakuwa kwa malengo uliyonayo, inaweza kuwa ni mfuko wa dharura au shughuli za maendeleo kama ujenzi, ununuzi wa gari na mengine.
Jua mipango yako ya mbele kisha anza kuifanyia maandalizi kwa kuiwekea akiba maalumu kutoka kwenye kila kipato. Weka akiba hiyo mahali ambapo siyo rahisi kuitumia.
Tatu; Uwekezaji (10%).
Uwekezaji ni kwa ajili ya kipato cha baadaye, uweze kuingiza kipato bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Ni kupitia uwekezaji ndiyo unajijengea uhuru wa kifedha, ambapo unaweza kuingiza kipato hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.
Kwa kila kipato unachoingiza, unapaswa kuwekeza angalau asilimia 10. Fanya hivyo kwenye kila kipato bila kuacha na utaweza kujenga uwekezaji mkubwa na unaokupa uhuru wa kifedha.
SOMA; Jinsi Ya Kudhibiti Matumizi Yako Na Bado Ukawa Na Maisha Bora.
Nne; Kujifurahisha (10%)
Wewe kama mtu unayejisukuma kufanya shughuli za kukuingizia kipato, kuna vitu ambavyo huwa unapenda kufanya au kuwa navyo. Pamoja na kwamba unapaswa kudhibiti matumizi yako, hupaswi kujinyima hivyo vitu unavyopenda.
Hivyo kwenye kila kipato chako, tenga angalau asilimia 10 kwa ajili ya kupata vile vitu unavyopenda zaidi. Kufanya hivyo inakupa msukumo wa kuendelea na shughuli zako za kuingiza kipato. Hapa iwe ni vitu unavyopenda wewe kutoka ndani yako na siyo kuiga watu wengine.
Tano; Sadaka (10%)
Kulingana na imani yako, unapaswa kutoa sadaka au misaada kwa wale wenye uhitaji. Huo ni wajibu wako kama mwanadamu ambaye umepewa uwezo wa kufanya shughuli za kukuingizia kipato, ili kuwa na mchango mzuri kwa watu wengine.
Kwenye kila kipato unachoingiza, tenga asilimia 10 kwa ajili ya sadaka na misaada ambayo unawapa wale wenye uhitaji. Utoaji wa aina hiyo huwa unakutengenezea fursa za kuingiza kipato zaidi.
Tengeneza mpango sahihi wa matumizi ya fedha zako kama ulivyojifunza hapa ili uweze kuwa na USIMAMIZI MZURI WA FEDHA BINAFSI na kujenga utajiri na uhuru wa kifedha kwenye maisha yako.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua kwa kina mpango huo wa matumizi kwa namna unayoweza kufanyia kazi. Karibu ujifunze na ukachukue hatua mara moja.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.